Mkenya apewa masharti Simba | Mwanaspoti

MOHAMED Bajaber ni mali ya Simba, ambapo winga huyo ametua kikosini hapo kwa mkataba wa miaka miwili akitokea Kenya Police FC ya nchini Kenya.

Bajaber aliyezaliwa Machi 15, 2003 jijini Nairobi nchini Kenya, kwa sasa ana umri wa miaka 22 ambapo hadi anajiunga na Simba, klabu hiyo imetoa Dola za Kimarekani 180,000 (Sh458 milioni za Kitanzania).

Chanzo kutoka Simba, kimeliambia Mwanaspoti kwamba, ndani ya mkataba huo wa miaka miwili aliopewa Mkenya huyo, kuna kipengele cha bonasi endapo atafikia malengo aliyowekewa.

Chanzo hicho kilisema Bajaber aliye na uwezo wa kucheza winga ya kushoto, kulia na mshambuliaji wa pili, endapo msimu ujao akihusika na zaidi ya mabao 10, atapewa bonasi ya Sh12 milioni kwa mwaka kama motisha ya kujituma.

“Anachojaribu kukitengeneza kocha Fadlu Davids ni kuandaa timu yenye ushindani mkubwa kwa msimu ujao, ndiyo maana alipendekeza majina ya wachezaji vijana zaidi endapo wakifanya vizuri baadhi yao kuna vipengele vya kuongezewa mkataba na ofa ya pesa,”  kilisema chanzo hicho na kuongeza:

“Mfano katika mkataba wa Bajaber atapewa Sh12 milioni akihusika na zaidi ya mabao 10, hilo litamfanya mchezaji kujituma kwa bidii akijua kuna kitu atakipata mwisho wa msimu, kufanya vizuri kwa mchezaji ndiyo mafanikio ya klabu yetu.”

Chanzo hicho kilisema malengo ya Simba kwa msimu ujao ni kurejesha heshima ya kunyakua mataji mbalimbali, ili kufanikisha hilo viongozi wanafanya umakini mkubwa wa kusajili wachezaji na kuhakikisha wanapata moyo wa kuipambania nembo ya klabu.

“Mfano kama mkataba wa kiungo mkabaji Alassane Kante aliyesaini miaka miwili akitokea CA Bizertin ya Tunisia, akicheza kwa asilimia 70 au zaidi katika mechi zote za msimu basi ataongezewa mkataba mwingine, kwa kifupi Simba inaingia mikataba na wachezaji kwa umakini zaidi,” kilisema chanzo hicho na kuongeza:

“Usajili unaoendelea kufanyika tunahitaji uwe na tija uwanjani, ndiyo maana unaona kila hatua inakuwa na umakini mkubwa, ili mchezaji anufaike na klabu inufaike, kwani kuna vipengele vya kuwabana pia.”

Mbali na Bajaber hadi kufikia jana mchana Simba ilikuwa imetambulisha wachezaji wapya watano ambao ni Rushine De Reuck, Alassane Kante, Morice Abraham, Hussein Daudi Semfuko na Jonathan Sowah.