BAADA ya timu ya taifa ya Tanzania, Taifa Stars kuanza vyema fainali za Ubingwa wa Mataifa Afrika kwa Wachezaji wa Ligi za Ndani (CHAN), kocha wa kikosi hicho, Hemed Suleiman ‘Morocco’, amesema huo ni mwanzo tu, ingawa mambo mazuri zaidi yanakuja.
Morocco amezungumza hayo baada ya timu hiyo kuanza vyema michuano hiyo kwa kuifunga Burkina Faso mabao 2-0 katika mechi ya ufunguzi iliyopigwa juzi kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa jijini Dar es Salaam, hivyo kuandika rekodi nyingine mpya.
Akizungumza na Mwanaspoti baada ya mechi hiyo, Morocco alisema michuano hiyo kufanyika katika ardhi ya nyumbani ni jambo nzuri kwa wachezaji, mashabiki na benchi la ufundi, kwani inaongeza morali ya kupambana zaidi tofauti na miaka ya nyuma.
“Tulicheza vizuri na tulistahili kushinda na hii ni kutokana na wachezaji bora na maandalizi tuliyofanya tangu mwanzoni, kwetu ni heshima kama taifa japo bado tunahitaji kuona kile tulichokifanya leo (juzi) tunaendelea kukionyesha,” alisema.
Katika mechi hiyo, mabao ya Stars yalifungwa na Abdul Suleiman ‘Sopu’ aliyefunga kwa penalti dakika ya 45 baada ya beki wa timu ya Burkina Faso, Franc Tologo kumchezea vibaya mshambuliaji nyota wa Stars, Clement Mzize kwenye eneo la hatari.
Kipindi cha pili Stars ikaendelea kutengeneza nafasi nyingi za kufunga ambapo iliichukua hadi dakika ya 71 kupata bao la pili lililofungwa na, Mohamed Hussein ‘Tshabalala’, aliyefunga kwa kichwa akimalizia krosi safi ya Idd Seleiman ‘Nado’.
Ushindi huo wa Stars umeifanya kuandika rekodi mpya ya kushinda mechi ya kwanza ya michuano hiyo, kwani mara zote mbili ilizoshiriki haijawahi kufanya hivyo, ikianza ile ya mwaka 2009, ilipoanza kwa kichapo cha bao 1-0, dhidi ya Senegal.
Katika fainali hizo ambazo DR Congo ilitwaa taji baada ya kuifunga Ghana mabao 2-0, Stars ilipangwa kundi A na timu za Zambia, Senegal na wenyeji wa michuano, Ivory Coast, ambapo kikosi hicho kilimaliza kikiwa nafasi ya tatu na pointi nne.
Stars ikashiriki mara ya pili mwaka 2020 na kuishia tena hatua ya makundi, ikimaliza ya tatu kundi D na pointi zake nne, nyuma ya Guinea iliyoongoza na pointi tano sawa na Zambia iliyomaliza ya pili, huku Namibia ikiwa ya nne na pointi moja.
Fainali hizo za 2020 zilifanyika Cameroon na bingwa wa michuano hiyo ilikuwa ni Morocco iliyoichapa Mali mabao 2-0, katika mechi ya fainali na kutetea tena ubingwa huo, baada ya kikosi hicho kufanya hivyo mwaka 2018 ikiwa ndio wenyeji.
Stars kwa sasa katika kundi B la michuano hiyo ina pointi tatu, huku Burkina Faso iliyochapwa juzi ikiburuza mkiani, zikifuatiwa na Madagascar na Mauritania ambazo jana zilikuwa zinacheza, sawa na kikosi cha Jamhuri ya Afrika ya Kati.