Muujiza mtoto aliyenusurika baada ya kupigwa risasi ya kichwa

Palestina. Unaweza kusema ni muujiza, miongoni mwa maelfu waliouawa Gaza, mtoto wa Kipalestina, Lana Al-Basous amepigwa risasi kichwani lakini risasi hiyo haijamuua wala kumtoa damu.

Lana kutoka Gaza, amenusurika kwa njia ya kushangaza baada ya kupigwa risasi iliyorushwa na drone ya Israel, ambapo risasi hiyo ilisimama kati ya fuvu lake na nywele bila kuvunja mfupa wa fuvu.

Taarifa ya muujiza huu, imekuja wakati idadi ya watu waliouawa na kujeruhiwa katika mashambulizi ya Israel huko Gaza ikiendelea kupanda kwa kasi kubwa.

Vyombo vya habari nchini humo, vimeripoti kuwa madaktari wamefanikiwa kuiondoa risasi hiyo.

Kwa mujibu wa takwimu zilizotolewa Agosti Mosi, 2025 na Wizara ya Afya ya Gaza, Wapalestina wapatao 60,249 wameuawa katika vita vya Israel dhidi ya Ukanda wa Gaza tangu Oktoba 2023.

Katika saa 24 zilizopita za siku hiyo, miili 111 ilifikishwa katika hospitali za Gaza, huku watu 820 wakijeruhiwa, na kufanya idadi ya jumla ya majeruhi kufikia 147,089 kutokana na mashambulizi ya Israel.

Msichana huyo mdogo wa Kipalestina alipigwa risasi hiyo kichwani na vikosi vya Israel.

Takwimu za kusikitisha zaidi ni zile zinazoonyesha mauaji ya Wapalestina wakati wakijaribu kupata msaada wa kibinadamu.

Tangu Mei 27, jumla ya watu 1,330 waliuawa na 8,818 kujeruhiwa wakati wakijaribu kutafuta mahitaji ya msingi ya kuishi kikiwamo chakula na maji.

Vikosi vya Israel vimeendelea na mashambulizi yake katika Ukanda wa Gaza tangu Machi 18, licha ya makubaliano ya kusitisha mapigano na kubadilishana wafungwa yaliyofikiwa Januari.

Kwa mujibu wa takwimu za Serikali ya Palestina, Wapalestina 9,071 wameuawa na 34,853 kujeruhiwa tangu wakati huo.