Mwanza yapaa Kriketi Kanda ya Ziwa

JITAHADA za Chama cha Kriketi kuhakikisha mchezo huo una vipaji bora nchi nzima zinazidi kuzaa matunda na hivi karibuni mchezo huu umejenga mizizi mikoa ya Kanda ya Ziwa,

Ligi ya Vijana chini ya miaka 17 ndiyo shuhuda wa mafanikio ya kriketi kanda hii na mbabe wa michuano akiwa Mkoa wa Mwanza.

Taarifa ya Chama cha Kriketi nchini, TCA ilisema michuano hii iliyomalizika wikiendi iliyopita, imetoa vipaji vingi ambavyo ni tumaini kubwa la timu ya taifa kwa siku zijazo.

Katika ligi hiyo, timu ya wavulana ya Mwanza ilibuka mshindi wa jumla wakati Kombaini ya Geita ilishika nafasi ya pili baada ya kupoteza dhidi ya Mwanza katika fainali.

Kwa upande wa tuzo binafsi mrushaji bora (bowler) alikuwa ni Ibrahimu Twaha wa Geita, huku  Godfrey Vincent wa timu hiyo akiibuka mpigaji bora (batsman) na mdaka wiketi bora, Joshua Majaliwa.

Vincent alisema “Tunawapongeza wachezaji, makocha na timu zote zilizoshiriki katika ligi hii kwani mafanaikio yaliyopatikana yamesaidia kuiandalia Tanzania  timu bora ya taifa kwa miaka ijayo,” ilsema TCA kupitia msemaji wake, Ateef Salim.

Kutokana na jitihada zake za kuiboresha kriketi kuanzia  wachezaji chipukizi, chama cha Kriketi duniani kimeizawadia Tanzania tuzo maalum ya ICCx Rexona.

Aliyepokea tuzo kwa niaba ya Tanzania ni Makamu Mwenyekiti wa Chama cha Kriketi nchini Ashish Nagewadia. Utoaji wa tuzo ulifanyika katika ukumbi wa ICC uliopo nchini Singapore.