Mwisho utumishi wa wabunge leo

Dar es Salaam. Utumishi wa miaka mitano wa wawakilishi wa wananchi katika Bunge la 12 umekoma leo, Jumapili, Agosti 3, 2025, baada ya kuhudumu tangu Novemba 13, 2020.

Hatua ya kukoma kwa Bunge hilo, inatokana na Rais Samia Suluhu Hassan kuwasilisha hati ya kulivunja, kwa mujibu wa Ibara ya 92(2)a ya Katiba ya Tanzania.

Kukoma kwa Bunge hilo, kunafungua milango kwa wanasiasa kuomba ridhaa kupitia vyama vyao, ili wachaguliwe kuwawakilisha wananchi kwa kipindi cha miaka mitano ijayo. Bunge hilo linakoma katika kipindi ambacho vyama vya siasa vipo katika hatua mbalimbali za michakato ya kuwapata wawakilishi watakaoomba ridhaa ya ubunge katika uchaguzi mkuu utakaofanyika Jumatano, Oktoba 29, 2025.

Katika bunge hilo lililokuwa na zaidi ya asilimia 90 ya wabunge wanaotokana na Chama cha Mapinduzi (CCM), tayari zaidi ya 40 hawatakuwa sehemu ya Bunge lijalo, baada ya kutemwa kwenye michakato ya ndani ya chama hicho.

Baadhi ya wabunge maarufu ambao hawakuchukua fomu kuomba tena ridhaa ni pamoja na Kassim Majaliwa (Ruangwa), Askofu Josephat Gwajima (Kawe), Aida Kenani (Nkasi), Kapteni George Mkuchika (Newala) na Halima Mdee (Viti Maalumu).

Upekee wa Bunge la 12, unatokana na kuhutubiwa na wakuu wa nchi wawili: hayati John Magufuli, aliyelizindua Novemba 13, 2020, na Rais Samia Suluhu Hassan, aliyelihutubia Aprili 19, 2021, mwezi mmoja baada ya kuapishwa kuwa Rais.

Samia, akiwa Makamu wa Rais, aliapishwa Machi 19, 2021, kuwa Rais kuchukua nafasi ya Magufuli, alyeifariki dunia Machi 17, 2021, katika Hospitali ya Mzena, Dar es Salaam. Pia, Rais Samia alilihutubia Bunge hilo kwa kuliahirisha Juni 27, 2025.

Tangu kuzinduliwa kwa Bunge hilo, Novemba 13, 2020, hadi leo, Agosti 3, 2025, linapovunjwa ni siku 1,724, sawa na miaka minne, miezi minane, na siku 21.

Pia, Bunge la 12 ndilo lililoongozwa na maspika wawili, akianza Job Ndugai, kabla ya kujiuzulu Januari 6, 2022, na wadhifa huo kuchukuliwa na aliyekuwa naibu wake, Dk Tulia Ackson.

Pamoja na kuvunjwa kwa bunge, Ibara ya 90(4) inampa mamlaka Rais kuitisha mkutano wa Bunge iwapo atagundua kumetokea hali ya hatari na matokeo ya uchaguzi wa wabunge wapya hayajatangazwa.

“Rais aweza kutoa taarifa maalumu ya kuitisha mkutano wa Bunge na kuagiza kwamba Spika na watu wote waliokuwa wabunge mara tu kabla Bunge halijavunjwa wahudhurie mkutano huo wa Bunge, na watu hao pamoja na huyo Spika.

“Watahesabiwa kuwa ndiyo wajumbe wa Bunge kwa madhumuni ya mkutano huo, na watahesabiwa hivyo mpaka usiku wa manane wa siku yatakapotangazwa matokeo ya kura zilizo nyingi za uchaguzi mkuu,” imeeleza sehemu ya ibara hiyo.

Julai 30, 2025, Rais Samia alitoa hati ya kulivunja Bunge, ikiwa ni utekelezaji wa Ibara ya 92(2)a ya Katiba ya Tanzania inayompa Rais mamlaka ya kulivunja Bunge.

Katika hati hiyo, Rais Samia aliandika, “Kwa kuwa, uchaguzi mkuu unatarajiwa kufanyika mwezi Oktoba, mwaka 2025.

“Na, kwa kuwa, kwa mujibu wa kifungu cha 49 cha Sheria ya Uchaguzi wa Rais, Wabunge na Madiwani, Sheria Na. 1 ya Mwaka 2024, uteuzi wa wagombea kwa ajili ya uchaguzi mkuu hauwezi kufanyika isipokuwa kama Bunge limekwishavunjwa.

Kwa mujibu wa hatua hiyo, Ibara ya 90(2)a ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya Mwaka 1977, Rais anaweza kulivunja Bunge iwapo limemaliza muda wa uhai wake wa miaka mitano, kwa mujibu wa Ibara ya 65 ya Katiba, au wakati wowote ndani ya kipindi cha miezi kumi na mbili ya mwisho ya uhai wa Bunge.

 “Hivyo basi, mimi, Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kwa mamlaka niliyopewa chini ya Ibara ya 90(2)(a) ya Katiba, ninalivunja Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kuanzia tarehe 3 Agosti, 2025, ili kutoa fursa kufanyika kwa uteuzi wa wagombea katika uchaguzi mkuu na kufanyika kwa uchaguzi mkuu,” imeandikwa hati hiyo.

Hatua ya kuvunjwa kwa Bunge hilo inakomesha wadhifa wa ubunge kwa wabunge waliohudumu kuanzia mwaka 2020 hadi 2025 na kutoa nafasi ya kupatikana wengine.

Katika bunge hilo, wabunge 10 walifariki dunia ambao ni Atashasta Nditiye (Muhambwe), Elias Kwandikwa (Ushetu), William Ole Nasha (Ngorongoro), Khatib Said Haji (Konde) na Francis Mtega (Mbarali).

Wengine ni Mussa Hassan Mussa (Amani), Ahmed Yahaya Abdulwakil (Kwahani), Dk Faustine Ndugulile (Kigamboni), Irene Ndyamkama (Viti Maalumu) na Martha Jachi Umbula (Viti Maalumu).