Mzambia aichomolea Namungo | Mwanaspoti

WAKATI mabosi wa Namungo wakimpigia hesabu za kumrejesha aliyekuwa kocha wa timu hiyo, Mzambia Hanour Janza kwa ajili ya kukinoa kikosi hicho kwa msimu ujao, dili hilo huenda likakwama rasmi baada ya kushindwa kufikia makubaliano mapya.

Janza alikuwa katika mazungumzo na uongozi wa Namungo ili kuja kuchukua nafasi iliyoachwa wazi na kocha Juma Mgunda, aliyeondoka, ingawa hadi sasa dili hilo huenda likakwama baada ya Mzambia huyo kutaka kiasi kikubwa cha fedha kurejea.

Taarifa ambazo Mwanaspoti imezipata, zinasema Janza ametaka kiasi kikubwa cha fedha jambo ambalo limeongeza ugumu wa kumpata, ambapo kwa sasa uongozi unaangalia kocha mwingine atakayekinoa kikosi hicho cha Wauaji wa Kusini msimu ujao.

Akizungumza na Mwanaspoti, Mratibu wa Namungo, Ally Suleiman alisema kama kuna taarifa juu ya suala hilo, watazitolea ufafanuzi kwa mashabiki zao, japo kwa sasa wanaendelea na maboresho ya nyota wapya kwa ajili ya msimu ujao.

Hata hivyo, uongozi wa Namungo unafanya mazungumzo na kocha mmoja kutoka DR Congo kwa lengo la kurithi mikoba ya Mgunda, ambapo Mwanaspoti kwa sasa linaendelea kufuatilia kwa ukaribu ili kupata jina lake kamili na kulichapisha kwa uharaka.

Mgunda aliyewahi kuzifundisha timu mbalimbali zikiwemo Coastal Union, Simba na Simba Queens, alijiunga rasmi na Namungo Oktoba 24, 2024, akichukua nafasi ya Mkurugenzi wa Programu za Soka la Vijana wa kikosi hicho Mkongomani Mwinyi Zahera.

Kwa msimu wa 2024-2025, Mgunda aliiwezesha Namungo kumaliza nafasi ya tisa katika Ligi Kuu Bara na pointi 35, baada ya kikosi hicho cha ‘Wauaji wa Kusini’, kushinda mechi tisa, sare nane na kupoteza 13, kikifunga mabao 28 na kuruhusu 36.

Kwa upande wa Janza aliyefanya mazungumzo na uongozi ili kurejea tena, aliondoka kikosini humo, Desemba 7, 2022, huku akiifundisha timu ya Taifa ya Taifa Stars, kisha baadaye kuteuliwa Mkurugenzi wa Ufundi wa ZESCO United ya kwao Zambia.