Dar es Salaam. Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan ameivunja bodi ya Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii (NSSF) na kuwateuwa watendaji mbalimbali.
Bodi ya NSSF ilikuwa inaundwa na Mwenyekiti wake, Mwamini Malemi, Makamu, Abdul Zuberi, huku wajumbe ni Juliana Mpanduji, Joseph Nganga, John Kinuno, Henry Mkunda, Fauzia Malik, Lucy Chigudulu na Oscar Mgaya.
Taarifa hiyo, imetolewa leo, Jumapili Agosti 3, 2025 na kusainiwa na Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais Ikulu, Sharifa Nyaga.
Inaeleza mkuu huyo wa nchi, amevunja Bodi ya Wadhamini ya Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii (NSSF). Hata hivyo, taarifa hiyo, haikutoa sababu za kuvunjwa kwake.
Sambamba na hilo, Rais Samia amemteua Dk Khatibu Kazungu kuwa Katibu Tawala wa Mkoa wa Dodoma. Kabla ya uteuzi huu, Dk Kazungu alikuwa Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati.
Katika uteuzi huo, Profesa Ulingeta Mbamba ameteuliwa kuwa Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara Tanzania (Tantrade) kwa kipindi cha pili.
Imeeleza Profesa Aurelia Kamuzora ameteuliwa kuwa Mwenyekiti wa Baraza la Taifa la Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi kwa kipindi cha pili.
Aidha, Balozi Charles Makakala ameteuliwa kuwa Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya Shirika la Mzinga.
Taarifa hiyo inaeleza Balozi Anderson Mutatembwa amepangiwa kuwa Balozi wa Tanzania nchini Japan.