Dar es Salaam. Kada nguli wa Chama cha Mapinduzi (CCM) na mfanyabiashara maarufu, Rostam Aziz amepongeza mchakato mpya wa chama hicho katika kupitisha wagombea wa ubunge akisema unatoa nafasi ya haki na uwazi kwa watiania.
Akizungumza leo, Jumapili Agosti 3, 2025 jijini Dar es Salaam katika mahojiano maalumu, Rostam amesema amewahi kupitia michakato mingi ya chama hicho ikiwa ni pamoja na kutumikia nafasi za ubunge kwa miaka 18, uanachama wa Halmashauri Kuu (NEC), kamati kuu na Mweka Hazina wa Taifa, lakini hajawahi kuona utaratibu bora kama wa mwaka huu.
“Mchakato huu unaruhusu watiania kujaza fomu, kufanya tathmini ya kina kwa kila mgombea na kisha kurudishwa kwa wananchi kupigiwa kura. Mshindi wa kura za maoni ndiye anapeperusha bendera ya CCM isipokuwa awe amefanya kosa kubwa. Hii ni tofauti na zamani ambapo mshindi wa kura angeachwa na kuchukuliwa mgombea mwingine, jambo ambalo halikuwa la haki,” amesema Rostam.
Ameongeza kuwa utaratibu huu mpya ni wa haki na unapaswa kuendelezwa kwa kuwa unajenga imani ya wanachama na umma kwa chama hicho.