Sabri asaini mitatu Sweden, ajipanga

ALIYEKUWA kiungo wa Singida Black Stars Sabri Kondo ametambulishwa katika klabu ya BK Häcken ya Ligi Kuu ya Sweden, baada ya kusaini mkataba wa miaka mitano.

Subri ambaye msimu uliopita alicheza Coastal Union kwa mkopo, awali alienda katika timu hiyo inayokamata nafasi ya 10 katika msimamo wa ligi hiyo ya Sweden, ikicheza mechi 17 na ina pointi 22.

Kiungo huyo aliyewahi pia kukipiga KVZ ya Zanzibar kabla ya kusajiliwa na Singida Black Stars mwaka 2024 alisema hatamani kuishia kutambulishwa pekee bali kuonyesha kiwango kikubwa na kupata nafasi ya kucheza kikosi cha kwanza.

“Namshukuru Mungu na nimefurahi kusajiliwa na timu kubwa Ulaya. Lengo ni kufika mbali zaidi na kuipeperusha bendera ya Tanzania kimataifa na nitadhihirisha kwa nini nilipata nafasi ya kusaini mkataba na BK Häcken,” alisema Sabri na kuongeza:

“Sikufanya majaribio pekee, lakini nilisajiliwa baada ya kuonekana kwenye mechi za ligi na jana nilicheza mechi yangu ya kwanza.”

Sabri anakuwa mchezaji wa pili kusajiliwa klabuni hapo baada ya mwaka 2023, Aisha Masaka kutambulishwa kwa upande wa wanawake akitokea Yanga Princess.

Chama la kinda huyo (19), linashiriki mechi za mtoano ya kufuzu michuano ya UEFA Europa League na Jumatano timu hiyo itacheza mechi ya raundi ya tatu dhidi ya Brann.