Sita wakamatwa tuhuma za rushwa, mgombea ubunge atimka

Tabora. Watu sita wanashikiliwa na vyombo vya usalama Mkoa wa Tabora wakidaiwa kupokea rushwa kutoka kwa mmoja wa wagombea ubunge wa Nzega Mjini mkoani humo, huku wengine 40 wakisakwa akiwemo mgombea husika.

Mgombea huyo wa ubunge ambaye jina limehifadhiwa amekimbia na kutelekeza gari katika Mtaa wa Musoma wilayani Nzega Mkoa wa Tabora ambapo ukaguzi uliofanywa na vyombo vya usalama mkoani humo umebaini kuwamo zaidi ya Sh16 milioni ndani ya gari hilo ambazo wajumbe walikuwa wakipewa mmoja baada ya mwingine.

Hayo yamesemwa leo Jumapili Agosti 3, 2025 na Mkuu wa Mkoa wa Tabora, Paul Chacha alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari juu ya tukio hilo likiwahusisha makada hao wa Chama cha Mapinduzi (CCM).

Kesho Jumatatu, Agosti 4, 2025 kunafanyika kura za maoni za udiwani, ubunge na uwakilishi kwa Zanzibar. Ni baada ya kuhitimisha siku tano za wagombea wote kujitambulisha kwa wajumbe. Walianza Julai 30 hadi leo Agosti 3.

Chacha amesema watu hao pamoja na fedha wamekamatwa ndani ya gari la mgombea huyo.

“Waliokuwa wakihisiwa walikuwa zaidi ya 40 lakini wamekamatwa hao sita pamoja na hiyo zaidi ya Sh16 milioni na watu hawa walikuwa wakigawa fedha hizi kwa wajumbe ambao wanadaiwa kuwa wanahusika na uchaguzi wa kesho wa kura za maoni,” amesema Chacha.

Amesema baada ya mahojiano na watu hao waliokamatwa wamemtaja mgombea huyo na kusisitiza vyombo vya usalama vitawakamata na hakuna mzaha na vitendo vya rushwa hasa katika kipindi hiki cha uchaguzi.

“Tumewakamatwa usiku wa manane kifupi huo ni uhalifu kama uhalifu mwingine, kwa sababu usiku ni muda wa kulala na kupumzika, tutashughulika nao kikamilifu, hatuwezi kuchafuliwa sura na sifa njema za mkoa wetu,” amesema.

Chacha ameongeza kuwa: “Na tunazo taarifa usiku wa leo wagombea wengi wamejiandaa kufanya finishi (kuwapa hela za mwishomwisho kuelekea uchaguzi), niwaambie tu kwamba wagombea nawaomba na nawaelekeza wagombea wote mlale mapema, habari za kufanya finishing watafanya finishing na polisi na vyombo vyote vya usalama.”

Hata hivyo, watu hao wanaodhaniwa kuwa ni wajumbe wamesema mgombea huyo walikuwa naye kwenye gari lakini baada ya kuona wamekaribia kukamatwa akakimbia na kuwatelekeza ndani ya gari pamoja na fedha hizo.