Uchumi wa buluu unavyoinua uchumi ukilinda mazingira

Tanzania imeanza kuchukua hatua madhubuti kuelekea mageuzi ya kiuchumi kwa kuwekeza katika uchumi wa buluu, ikiwa ni sehemu ya mpango wa muda mrefu ulioainishwa kwenye Dira ya Maendeleo ya Taifa 2050.

Dira hiyo inatambua sekta ya uchumi wa buluu kama moja ya nguzo muhimu za kimageuzi zinazoweza kuongeza kasi ya maendeleo endelevu, kupunguza umaskini na kuboresha maisha ya wananchi, hususan wale wanaoishi katika ukanda wa pwani.

Tanzania ina zaidi ya kilomita 1,400 za pwani pamoja na eneo la uchumi wa bahari lenye ukubwa wa takriban kilomita za mraba 223,000.

Rasilimali hii kubwa ya bahari ni msingi muhimu wa shughuli za kiuchumi kama vile uvuvi endelevu, usafirishaji wa baharini, utalii wa pwani, nishati ya baharini, pamoja na uvunaji wa viumbe wa baharini kwa njia rafiki wa mazingira.

Takwimu zilizopo zinaonyesha kuwa sekta ya uvuvi inatoa ajira kwa watu zaidi ya milioni 2.5 nchini na huchangia asilimia 1.5 ya Pato la Taifa.

Hata hivyo, pamoja na kuwa na fursa hizo lukuki, bado matumizi yake hayajafikia kiwango cha kuridhisha, hasa katika maeneo ya Bara, tofauti na Zanzibar ambako zaidi ya asilimia 80 ya fursa za uchumi wa buluu zinatumika ipasavyo kutokana na sera za wazi na utekelezaji madhubuti unaofanywa na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar.

Katika juhudi za kubadili hali hiyo, Tanzania Bara imeanza kutekeleza miradi ya uhifadhi na urejeshaji wa mazingira ya pwani, hususan Bahari ya Hindi, kupitia mradi mkubwa wa kimkakati uitwao Bahari Mali. Mradi huu unalenga si tu kulinda mazingira bali pia kuchochea uchumi wa buluu kwa kushirikisha jamii, taasisi za kiraia, na wadau wa kimataifa.

Mradi huu unatekelezwa kwa ushirikiano kati ya Serikali, Shirika la Kimataifa la Uhifadhi wa Mazingira na Uasilia (IUCN), pamoja na jamii za wavuvi na wakazi wa maeneo ya pwani. Utekelezaji wa mradi unaendelea katika wilaya za Mkinga na Pangani mkoani Tanga, pamoja na Micheweni na Mkoani visiwani Pemba.

Katika maeneo haya, kazi ya kupanda tena majani ya baharini (seagrass) na mikoko inaendelea kwa kasi, ikiwa ni hatua ya kurejesha uoto wa asili wa bahari na kuimarisha mfumo wa ikolojia ambao ni muhimu kwa uzalishaji wa samaki, utunzaji wa maji ya bahari, na kupunguza athari za mabadiliko ya tabianchi.

Manufaa ya mradi kwa mazingira na jamii

Meneja wa Programu ya Ustahimilivu wa Pwani na Bahari wa IUCN, Joseph Olila, amesema kuwa kupitia mradi wa Bahari Mali, wananchi wanajengewa uwezo wa kuendesha shughuli za kiuchumi baharini kwa njia endelevu kama vile kilimo cha mwani, unenepeshaji wa kaa, ufugaji wa samaki na uvunaji wa majongoo bahari.

“Lengo letu ni kuwainua wananchi kiuchumi huku tukihakikisha kuwa shughuli zao haziathiri mazingira. Tunawafundisha njia mbadala na rafiki za matumizi ya bahari ili kuwawezesha kuboresha maisha yao bila kuharibu vyanzo vyao vya kipato,” alisema Olila.

Ameongeza kuwa pamoja na shughuli hizo, mradi pia unahusisha urejeshaji wa mikoko, ambayo kwa miaka mingi imekuwa ikikumbwa na uharibifu mkubwa kutokana na ukataji holela wa kuni, ujenzi wa nyumba na kutengeneza mitumbwi.

Mikoko ina mchango mkubwa kwa sababu ni mazalia ya samaki na viumbe wengine wa baharini, inazuia mmomonyoko wa udongo, huchuja taka kabla ya kuingia baharini, na hunyonya hewa ukaa (carbon dioxide), hivyo kupunguza joto duniani.

Kwa mujibu wa Olila, kufanikisha upandaji wa zaidi ya hekta 90.4 za mikoko hadi sasa ni mafanikio makubwa yanayoonyesha namna jamii inavyoshirikiana kwa vitendo katika kulinda rasilimali za bahari.

Katika Kijiji cha Moa, kilichopo wilayani Mkinga mkoani Tanga, wananchi wamekuwa mstari wa mbele katika utekelezaji wa mradi wa Bahari Mali. Kwa kushirikiana na wataalamu wa mazingira na wavuvi wa jadi, wamefanikiwa kupanda majani ya baharini kwenye maeneo ya kina kifupi ya bahari.

Ofisa Uvuvi wa wilaya hiyo, Ezra Katete, amesema kuwa maeneo ya pwani yenye urefu wa takriban kilomita 71 yamepangwa kufanyiwa kazi ya kurejesha uoto wa bahari, jambo ambalo linaelezwa kuwa ni muhimu katika kuongeza idadi ya samaki na viumbe wengine wa baharini.

“Samaki wamekuwa wakipungua kwa kasi kutokana na ongezeko la tindikali baharini pamoja na athari za shughuli za kibinadamu kama uvuvi haramu. Majani haya ya baharini husaidia kusafisha maji, kuchukua kaboni na kuchangia kwenye ukuaji wa samaki. Ni mfumo wa kiikolojia unaofaidisha watu na mazingira kwa wakati mmoja,” amesema Katete.

Naye Ofisa wa Suluhu Asilia wa IUCN, Suleiman Mohammed, amesema kuwa mikoko iliyopandwa katika wilaya za Pemba na Tanga haijaleta tu matokeo ya uhifadhi wa mazingira, bali pia imefungua fursa mpya za kiuchumi kwa jamii.

Amebainisha kuwa baadhi ya wanavijiji sasa wanavuna asali ya mikoko, aina ya asali yenye ladha ya kipekee ya chachu-tamu, ambayo inapata umaarufu kwenye masoko ya ndani na ya nje.

“Asali hii ni tofauti na ya kawaida na soko lake linapanuka kwa kasi. Hii ni fursa nyingine ya kiuchumi ambayo inachochewa moja kwa moja na uhifadhi wa mazingira. Inathibitisha kuwa mazingira yanapolindwa ipasavyo, huibua fursa mpya ambazo hazikuwahi kufikiriwa awali,” alisema Mohammed.

Ofisa Maendeleo wa Kijiji cha Moa, Sarah Mwaidasi, amesema kuwa zaidi ya wananchi 1,650 wamenufaika na mradi huo, si tu kwa kipato bali pia kwa kuboresha hali ya mazingira na usalama wa makazi yao. Ameongeza kuwa asilimia 90 ya wakazi wa kijiji hicho wanategemea bahari kama chanzo kikuu cha maisha yao.

“Mradi huu umetusaidia sana. Tumeweza kudhibiti mmomonyoko wa udongo, tumepata ongezeko la samaki na sasa utalii wa bahari umeanza kushika kasi kijijini kwetu. Hili linatuwezesha kuboresha maisha yetu huku tukilinda bahari yetu,” amesema Sarah.

Wito kwa vyombo vya habari

Mkurugenzi Mtendaji wa Chama cha Waandishi wa Habari wa Mazingira Tanzania (JET), John Chikomo, amesisitiza umuhimu wa vyombo vya habari kushiriki kikamilifu katika kuelimisha jamii kuhusu uchumi wa buluu.

Amesema kuwa waandishi wa habari wana nafasi ya kipekee ya kuhamasisha mabadiliko ya kijamii na kuonyesha fursa zilizopo katika rasilimali za baharini.

“Uchumi wa buluu si suala la wataalamu wa mazingira pekee, ni suala la kila Mtanzania. Vyombo vya habari vinaweza kusaidia kuibua mijadala ya kitaifa, kutoa elimu, na kusaidia wadau kufanya maamuzi sahihi. JET itaendelea kutoa mafunzo kwa waandishi ili waielewe vyema sekta hii na kuibeba ipasavyo,” amesema Chikomo.