Utaratibu kura za maoni CCM zitakavyopigwa

Dar es Salaam. Wakati kesho Jumatatu Agosti 4, 2025 Chama cha Mapinduzi (CCM) kikiendesha kura za maoni za udiwani, ubunge na uwakilishi kwa Zanzibar, imeelezwa mchakato utafanyika kwa kila kata kutokana na marekebisho mbalimbali ya katiba ya CCM ya mwaka 1977.

Katika marekebisho hayo yaliyofanyika katika Mkutano Mkuu wa CCM uliofanyika Januari 18-19, 2025 yaliwezesha kuongeza idadi ya wajumbe wa mkutano mkuu wa kata/wadi, jimbo na wilaya ili kupiga kura za maoni kuwapendekeza wanachama wanaowania udiwani, ubunge au uwakilishi wa eneo husika.

Katika mchakato wa ndani wa kura za maoni uliofanyika mwaka 2020 watiania ubunge walikuwa wakikusanywa eneo moja, kwa ajili ya kujinadi na kuomba kura papo hapo, mbele ya wajumbe wa CCM waliokuwa wakitoka maeneo mbalimbali.

Lakini kutokana na marekebisho hayo ya Katiba ya CCM, hivi sasa kura za ubunge zitapigwa kwenye kata za jimbo husika, kisha matokeo yake yatakusanywa na kuwasilishwa CCM wilayani kwa ajili ya majumuisho na kutangazwa mshindi.

Kwa lugha nyepesi mabadiliko hayo yaliyowezeshwa kuwa na ongezeko la wajumbe wa CCM watakaowachagua watiania udiwani na ubunge, yamezigeuza kata kuwa vituo vya kupigia kura tofauti na mwaka 2020.

Hata hivyo, matokeo ya udiwani yatatangazwa katika kata husika. Kwa maana hiyo wajumbe watakaowapigia madiwani ndio haohao watakaowachagua watiania wa ubunge.

Mmoja wa watiania ubunge (jina limehifadhiwa), ameliambia Mwananchi leo Jumapili Agosti 3, 2025 kuwa,” katika kila kata kutakuwa na mawakala wangu watakaoniwakilisha kwenye mchakato wa upigaji wa kura.”

Shughuli ya wagombea wote wa udiwani, ubunge na uwakilishi kwa Zanzibar kujitambulisha kwa wajumbe kwenye kata zote ilianza Julai 30 ambapo walikuwa wanakwenda pamoja na wanahitimisha leo Jumapili, Agosti 3, 2025.

Baada ya kumalizika kwa kura za maoni, vitaanza vikao vya uchujaji kuanzia kamati za siasa za kata kwa madiwani na jimbo kwa wabunge na wawakilishi.

Vikao hivyo vitaendelea kwa ngazi za mikoa, madiwani wao inaishia Agosti 13, 2025 ambapo Halmashauri Kuu za CCM za mikoa vitafanya uteuzi wa mwisho wa wagombea udiwani mmoja kwa kila Kata/Wadi iliyopo mkoani na udiwani wa viti maalumu.

Kwa wabunge na wawakilishi wao uteuzi wao utafanyika Agosti 22, 2025 ambapo kikao cha Halmashauri Kuu ya CCM chini ya uenyekiti wa Rais Samia Suluhu Hassan kitakutana ku­fikiria na kufanya uteuzi wa mwisho wa majina ya wanachama wanaoomba nafasi ya ubunge na uwakilishi wa jimbo na viti maalumu.

Baada ya hapo sasa, itafuatia ratiba ya Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC) ya uchukuaji na urejeshaji fomu. Kampeni za Uchaguzi Mkuu zitaanza Agosti 28 hadi Oktoba 28, 2025 na Jumatano ya Oktoba 29, 2025 itakuwa siku ya upigaji kura.