Vita katika sanduku la kura CCM, majimbo haya hapatoshi

Dar es Salaam. Kinyang’anyiro cha kuisaka tiketi ya kugombea ubunge wa majimbo kupitia Chama cha Mapinduzi (CCM), kimefikia katika sanduku la kura za maoni, huku mchuano mkali ukitarajiwa Makambako, Iringa Mjini, Kibamba, Namtumbo na Kinondoni.

Majimbo hayo ni machache kati ya mengi yanayotarajiwa kuwa na mchuano mkali wa kura za maoni, kutokana na kile kinachoelezwa na wachambuzi wa siasa kuwa, watia nia wake wanawiana nguvu ya ushawishi na kukubalika ndani ya CCM.

Kwa mujibu wa wachambuzi hao, mchuano huo utakuwa kati ya wabunge wanaotetea nafasi zao dhidi ya wabunge wa zamani, waliowahi kuwa viti maalumu dhidi ya wanaotetea nafasi zao na wanaotetea nafasi zao dhidi ya watendaji maarufu serikalini.

Kinyang’anyiro hicho cha kesho, Jumatatu, Agosti 4, 2025, kinakuja baada ya kukamilika kwa mchakato wa kura za maoni kwa nafasi za ubunge na uwakilishi wa viti maalumu kupitia makundi mbalimbali na washindi wake wanasubiri uamuzi wa vikao kuthibitishwa.

Hata hivyo, baada ya kura za maoni za watiania wa ubunge wa majimbo, vitasubiriwa vikao vya kitaifa vya chama hicho, kuthibitisha jina moja, litakalopewa fursa ya kupeperusha bendera ya CCM katika nafasi ya ubunge Oktoba mwaka huu.

Vikao hivyo vitaanza Jumanne, Agosti 5, kuanzia kamati za siasa za kata kwa madiwani na jimbo kwa wabunge, hadi Halmashauri Kuu ya CCM (NEC), itakayokutana Agosti 22, 2025, kwa ajili ya kupitisha na kufanya uteuzi wa mwisho.

Mchuano kati ya watiania hao, unatarajiwa kusababishwa na uhalisia kuwa, kuna uwiano wa nguvu na kukubalika ndani na nje ya chama hicho miongoni mwao.

Ingawa mchuano unatarajiwa kwa watiania wawili kati ya wengi katika jimbo moja, yapo baadhi ya maeneo kunakotarajiwa kuwa na mchuano wa zaidi ya watiania wawili, kutokana na ushawishi walionao.

Katika Jimbo la Iringa Mjini lenye watiania sita ambao ni Moses Ambindwile, Jesca Msambatavangu, Mchungaji Peter Msigwa, Fadhili Ngajilo, Edward Chengula na Islam Huwel, mchuano mkali unatarajiwa kushuhudiwa kati ya Jesca na Mchungaji Msigwa ambao wote kihistoria wamewahi kuwa wabunge wa jimbo hilo.

Jesca anawania kutetea nafasi yake, huku Msigwa akiwania kuliongoza jimbo hilo baada ya kufanya hivyo kwa miaka 10 tangu 2010 hadi 2020, kwa tiketi ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema).

Wawili hao wanafanana nguvu ya ushawishi wa kisiasa kutokana na historia zao, hivyo imebaki kwa wajumbe kuamua. Hata hivyo, lolote linaweza kutokea kwa watiania wote sita, ingawa nafasi kubwa wanapewa hao wawili.

Mchuano mwingine upo Jimbo la Makambako lenye watiania wawili ambao ni Deo Sanga, maarufu Jah People, anayewania kutetea nafasi yake, na Daniel Chongolo.

Nguvu ya Jah People inajengwa na historia yake bungeni, akiwawakilisha wananchi tangu mwaka 2010 wakati jimbo hilo likiitwa Njombe Kaskazini.

Chongolo naye si wa kawaida. Anabebwa na historia ya utumishi serikalini na ndani ya CCM, akiwa miongoni mwa wanasiasa waliowahi kuwa wakuu wa wilaya na mkoa.

Katikati ya hapo, Chongolo alikuwa Katibu Mkuu wa CCM, ikiwa ni miongoni mwa nafasi tatu za juu na zenye uamuzi wa mwisho ndani ya chama hicho tawala.

Vita ya wawili hao inapiganwa kwa turufu ya uzoefu na kujulikana ndani ya chama.

Katika Jimbo la Kibamba lenye watiania nane ambao ni Angellah Kairuki, Issa Mtemvu, Joseph Chikongowe, Dk Alphonce Temba, Mwamini Mwambo, Consolatha Rweikiza, Dk Nestory Yamungu na Dk Angelo Nyonyi, napo hapatoshi.

Ukiacha watiania wengine, mchuano mkali unatarajiwa kushuhudiwa kati ya mbunge anayetetea nafasi yake, Mtemvu, dhidi ya Kairuki, mwenye uzoefu katika utumishi bungeni na serikalini.

Wawili hao wanatarajiwa kuchuana kutokana na nguvu ya ushawishi waliyonayo kwa wajumbe kutokana na historia ya utendaji wao katika nafasi walizohudumu, kuanzia bungeni hadi serikalini.

Kinondoni napo hapatapoa, ushindani unatarajiwa kushuhudiwa kati ya mbunge anayemaliza muda wake, Abbas Tarimba dhidi ya aliyewahi kuliongoza jimbo hilo, Iddi Azzan. Kando yao yupo Michael Wambura, ambaye naye anazidisha joto katikati yao.

Vita nyingine zinazotarajiwa kushuhudiwa ni kati ya Aggrey Mwanri na Dk Godwin Mollel (Siha). Katika uchaguzi uliopita, mwaka 2020, Mollel alimshinda Mwanri aliyekuwa akitetea nafasi hiyo kwa kura moja. Je, sasa hali itakuwaje? Wajumbe wataamua.

Katika Jimbo la Nyamagana, Stanslaus Mabula anayetetea nafasi hiyo anachuana vikali na aliyekuwa mbunge wa jimbo hilo na aliyewahi kuwa Waziri wa Mambo ya Ndani, Lawrence Masha.

Kwingineko ni Shinyanga Mjini, ambako Stephen Masele licha ya kuongeza kura za maoni mwaka 2020.

Nyingine ni kati ya Charles Kajege na Kangi Lugola (Mwibara), Eric Shigongo na Charles Tizeba (Buchosa), Hamis Tabasamu na William Ngeleja (Sengerema), Constantine Kanyasu na Upendo Peneza (Geita Mjini), Stella Manyanya na John Nchimbi (Nyasa) na Jumanne Sagini na Charles Mahera (Butiama).

Michuano mingine ni kati ya Dk Juma Homera na Vita Kawawa (Namtumbo), Nusrat Hanje na Miraj Mtaturu (Singida Mashariki), Mussa Sima na Yagi Kiaratu (Singida Mjini), Dk Charles Kimei na Enock Koola (Vunjo).

Kinyang’anyiro kingine ni Isimani, kati ya William Lukuvi na Festo Kiswaga, Lazaro Nyalandu na Ramadhan Ighondo (Ilongero), Nwaru Maghembe na Joseph Ananisya (Mwanga), Michael Kembaki na Robert Chacha na Esther Matiko (Tarime Mjini).

Kwingine kutakaposhuhudiwa mchuano mkali ni kati ya Mwita Waitara na Nyambari Nyangwine (Tarime Vijijini), Juma Nkamia, Hamis Mkotya na Kunti Majala (Chemba), Salim Kikeke, Victor Tesha na Profesa Patrick Ndakidemi (Moshi Vijijini).

Pia, Revocatus Chiponda ‘Babalevo’, Baruani Muhuza na Kirumba Ng’enda (Kigoma Mjini), Jerry Muro na Saasisha Mafuwe (Hai), Nape Nnauye na Jemedari Said (Mtama) na Mary Nagu na Samwel Xaday (Hanang), huku Kambarage Wasira, Robert Maboto na Esther Bulaya wataumana (Bunda Mjini).

Atupele Mwakibete atachuana vikali na Thobias Andengenye (Busokelo), Richard Kasesela na Anthon Mwantoma (Rungwe), Dk Stephen Kebwe na Dk Amsabi Mrimi (Serengeti), Dk Raphael Chegeni na Simon Lusengekile (Busega) na Dkt Toba Nguvila, Festo Sanga na Profesa Norman Sigalla watachuana vikali (Makete). Profesa Sigalla alishindwa na Sanga katika uchaguzi wa mwaka 2020.

Akizungumzia hilo, mchambuzi wa siasa na uongozi, Dk Faraja Kristomus, amesema ushindani mkali utashuhudiwa kati ya watiania wanaotetea nafasi zao na wale waliowahi kuwa wabunge wa majimbo hayo zamani.

“Ushindi wa yeyote kati ya hao utategemea utendaji au udhaifu wa aliyemaliza muda wake na wajumbe watawalinganisha na waliowahi kuwa wabunge huko nyuma.

“Yawezekana wabunge wa sasa wakawa hawatoshi na hivyo wakaamua kuwarudisha wa zamani,” ameeleza.

Dk Kristomus amesema hali hiyo itashuhudiwa zaidi katika majimbo ya Makete, kati ya Profesa Norman Sigalla na Festo Sanga, Iringa Mjini kati ya Jesca Msambatavangu na Mchungaji Peter Msigwa, na Kinondoni kati ya Abbas Tarimba na Idd Azan.

Mwanazuoni huyo wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), amesema hali kama hiyo itashuhudiwa pia katika majimbo ya Nyamagana, kati ya Stanslaus Mabula na Lawrence Masha, na Siha, kati ya Aggrey Mwanri na Dk Mollel.

Ushindani mwingine, amesema ni kati ya wabunge wa zamani wa viti maalumu walioamua kuwania majimboni na wabunge wanaotetea nafasi zao.

“Tutashuhudia mtifuano kati ya Constantine Kanyasu na Upendo Peneza kule Geita Mjini, pia kati ya Benaya Kapinga na Judith Kapinga kule Mbinga Vijijini,” amesema.

Kundi la tatu la ushindani, amesema ni kwa majimbo yanayohusisha watiania maarufu serikalini dhidi ya wanaotetea nafasi zao.

 “Hapa tutashuhudia ushindani kati ya aliyewahi kuwa Katibu Tawala Mkoa wa Dar es Salaam, Dk Toba Nguvila, na Festo Sanga huko Makete. Thobias Andengenye atamhenyesha Atupele Mwakibete huko Busokelo. Pia, Juma Homera atamhenyesha Vita Kawawa, Namtumbo,” amesema Dk Kristomus.

Mchambuzi wa siasa, Gabriel Mwang’onda, amesema mchuano wa kura za maoni utakuwa mkali kwa kuwa baadhi ya wanaopambana wana nguvu na uzoefu.

 “Sijajua utaratibu utakuaje, maana mwaka 2020 aliyeshinda alipigwa chini na kuchukuliwa nafasi ya pili au tatu, sasa hivi itakuaje? Ni mchakato mzuri utakaokuwa na ushindani, lakini sijui itakuaje.

“Pamoja na mambo mengine nimependa namna ushindani uliopo kati ya wagombea waliorejeshwa majina yao. Pia, nimependa namna CCM ilivyowarejesha wagombea wanne hadi watano au sita katika jimbo moja, hii inaongeza wigo wa demokrasia,” amesema Mwang’onda.

Mwang’onda amesema kitendo cha wagombea wengi kurejeshwa kimesaidia hata wale waliokata tamaa ya majina yao kukatwa ngazi ya chini kupata matumaini katika mchakato wa kura za maoni.

“Narudia tena, ushindani utakuwa mkubwa miongoni mwa wagombea, kazi itakuwa kwa wajumbe kuamua nani wa kwenda naye. Kuna baadhi ya majimbo wagombea wengine walikuwa mawaziri, sijui itakuaje wakishindwa kuibuka kidedea kwenye kura za maoni,” amesema, na kuongeza:

“Kuna sehemu kutakuwa na mtiti mkubwa kutokana na uzito wa wagombea, mfano wa jimbo la Makambako, Kwimba, Bunda Mjini, Busokelo, Mbeya Mjini, Iringa Mjini, Shinyanga Mjini, Nyamagana na Tarime Mjini.”

Kwa upande wa mchambuzi wa masuala ya kisiasa, Hamduny Marcel, amesema anachotarajia kuona ni mabadiliko makubwa katika hatua hiyo, huenda sura zilizozoeleka zikadondoka.

Hilo linatokana na kile alichoeleza, mchakato wa mwaka huu ni mgumu, hasa ukizingatia idadi ya wajumbe imeongezeka tofauti na hapo awali.

Lingine alilosema Marcel, ni kuimarika na umakini wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), hali inayoziba mianya ya vitendo vya rushwa.

Kwa sababu ya mazingira hayo, amesema huenda majimbo yatakayokuwa na mchuano mkali, yakashuhudia vilio na vicheko kwa waliozoeleka kukosa nafasi na wapya wakaingia.

“Waliotabiriwa wanaweza wakakosa nafasi na ukashangaa sura mpya zinakuja zikaingia,” amesema.

Amesema hata wajumbe nao wamekuwa na misimamo mikali kwa kuwa wamepokea wito mbalimbali kutoka kwa raia wema wenye mapenzi mema na wanaohitajika mabadiliko ya kweli.

Amesema hata maneno yanayosemwa na raia mitaani yanaweza kubadilisha misimamo ya wajumbe ambao kwa kiasi fulani hawataki kuonekana kikwazo cha matakwa ya umma.

“Wajumbe hawa wanakaa mitaani wanayasikia na wanayoona na ni miongoni mwa wanaolalamika wabunge hawajafanya mambo fulani kama walivyotarajia na wanataka kukuambia mzigo wa lawama.

“Natarajia kuona majina ya kina mama mengi kwa kuwa wamekuwa wakakamavu na jasiri wa kujenga hoja na kujieleza,” amesema.

Mwanazuoni wa sayansi ya siasa wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Dk Richard Mbunda, amesema kuna uwezekano mdogo wa kupenya kwenye kinyang’anyiro hicho kuliko inavyodhaniwa.

 “Idadi ya wajumbe imeongezeka, mwaka 2020 baadhi ya majimbo idadi ya wajumbe ilikuwa 400 lakini sasa wamefikia hadi 7,000, unakuwa mtihani kweli kweli na wabunge wengi wanaotetea majimbo hawajafanya vizuri, walikuwa wagonga meza tu hawana uhakika,” amesema.

Utaratibu wa kura za maoni

Kutokana na marekebisho mbalimbali ya katiba ya CCM ya mwaka 1977, ikiwamo ya kuongeza idadi ya wajumbe wanaopiga kura za kuteua watiania wa udiwani, ubunge na uwakilishi, hivi sasa mchakato huo utafanyika ngazi za kata.

 Mwaka 2020, watiania ubunge walikuwa wakikusanywa eneo moja, kwa ajili ya kujinadi na kuomba kura papo hapo, mbele ya wajumbe wa CCM waliokuwa wakitoka maeneo mbalimbali.

Lakini kutokana na marekebisho hayo ya katiba ya CCM, hivi sasa kura za ubunge zitapigwa kwenye kata za jimbo husika, kisha matokeo yake yatakusanywa na kuwasilishwa CCM wilayani kwa ajili ya majumuisho na kutangaza mshindi.

Kwa lugha nyepesi, mabadiliko hayo yaliyowezesha kuwa na ongezeko la wajumbe wa CCM watakaowachagua watiania udiwani na ubunge, yamezigeuza kata kuwa vituo vya kupigia kura tofauti na mwaka 2020.

Hata hivyo, matokeo ya udiwani yatatangazwa katika kata husika. Kwa maana hiyo, wajumbe watakaowapigia madiwani ndio hao hao watakaowachagua watiania wa ubunge.

Mmoja wa watiania ubunge (jina limehifadhiwa), ameliambia Mwananchi kuwa, “Katika kila kata kutakuwa na mawakala wangu watakaoniwakilisha kwenye mchakato wa upigaji wa kura.”