Dar es Salaam. Uwekezaji katika elimu ya awali ni msingi muhimu wa maendeleo ya mtoto na Taifa kwa ujumla.
Katika hatua hii ya maisha, watoto hujifunza stadi za msingi kama vile mawasiliano, ushirikiano na fikra bunifu, ambazo huakisi mafanikio yao ya baadaye kitaaluma na kijamii.
Elimu ya awali huchochea ukuaji wa ubongo, huandaa watoto kwa elimu ya msingi na hupunguza changamoto za kiakili na kitabia baadaye.
Licha ya kuwapo kwa faida hizo, uwekezaji zaidi unahitajika katika ngazi hiyo ya elimu, kwani walimu wanaofundisha madarasa hayo bado wanakabiliwa na mzigo mkubwa wa wanafunzi katika darasa moja.
Hiyo ni kwa sababu hadi mwaka 2024, mwalimu mmoja wa awali alikuwa akifundisha wanafunzi 120 ndani ya darasa moja, ikiwa ni idadi mara nne zaidi ya wanafunzi anaotakiwa kufundisha.
Hiyo ni kwa sababu mwalimu mmoja wa awali anatakiwa kufundisha wanafunzi 25 pekee ndani ya darasa moja, kwa mujibu wa uwiano uliowekwa na Serikali.
Takwimu hizo za Kitabu cha Hali ya Uchumi wa Taifa cha mwaka 2024 kilichotolewa na Ofisi ya Rais – Mipango na Uwekezaji, kinaeleza mwaka 2024 walimu walikuwa 13,042, ikiwa ni ongezeko kutoka walimu 9,608 mwaka 2023.
Idadi hiyo ya walimu ni sawa na ongezeko la asilimia 35.7. Hata hivyo, kati ya walimu waliokuwapo, 10,348 pekee ndiyo walikuwa wenye sifa za kufundisha elimu ya awali, sawa na ongezeko la asilimia 30 ikilinganishwa na walimu 7,958 mwaka 2023.
Uwiano wa wanafunzi 120 kwa mwalimu ni pungufu ikilinganishwa na wanafunzi 163 waliokuwa wakifundishwa mwaka 2023.
Kuimarika huku kwa uwiano, kwa mujibu wa Serikali, kulitokana na ajira za walimu zilizotolewa ili kukabiliana na upungufu wa walimu katika shule za awali za Serikali.
Uwiano huo unatokana na wanafunzi walioandikishwa katika elimu ya awali katika shule za Serikali kuwa 1,558,549 ikilinganishwa na wanafunzi 1,562,286 walioandikishwa mwaka 2023.
Pia, wanafunzi walioandikishwa katika shule zisizo za Serikali waliongezeka na kufikia 118,010 mwaka 2024 ikilinganishwa na wanafunzi 117,256 walioandikishwa mwaka 2023.
Mdau wa elimu, Ochola Wayoga, amesema kuna umuhimu mkubwa wa kuwekeza katika elimu ya awali na inapaswa kutambuliwa kama sekta inayojitegemea badala ya kuunganishwa katika ngazi nyingine za elimu.
Amesema bila kufanya uwekezaji katika eneo hilo, matokeo chanya hayawezi kuonekana kwa wanafunzi, kwani ngazi hiyo ndiyo ambayo watoto hujifunza vitu vingi, ikiwemo mawasiliano, kuumba maneno, kujifunza kusoma na kuandika.
“Tafiti nyingi zilizowahi kufanywa zinaonesha kuwa kuna matokeo chanya makubwa kwa watoto waliopitia elimu ya awali ikilinganishwa na wale ambao hawajasoma kabisa, ndiyo maana nchi nyingi zilizoendelea zimeweka nguvu katika elimu hiyo,” amesema.
Amesema elimu ya awali pia hujenga tabia chanya za watoto, kwani wanachofundishwa watakiishi maisha yao yote, akitolea mfano wa nchi kama China ambapo jamii yake haina tabia mbaya kutokana na msingi waliowekewa.
“China wanavyowekeza kwenye elimu ya awali na kuwafundisha watoto, wanayaishi maisha yao yote. Wakija huku wanaingia katika mifumo yetu, lakini ukiwa China huwezi kukuta tabia za ajabu. Unaweza kulala mlango wazi na hakuna wa kuvunja,” amesema.
Amesema matunda ya kuwekeza kwenye elimu hiyo ni makubwa kuliko kuwekeza sekondari na vyuo, na ndiyo sehemu msingi mzuri unapoweza kujengwa.
Amesema uwekezaji katika elimu ya awali unapaswa kuanzia katika madarasa wanayotumia watoto, ambayo yameelekezwa kwa mujibu wa taratibu.
Madarasa hayo ni yale yanayozungumza, ambayo yanawawezesha wanafunzi kujifunza kwa urahisi kulingana na umri walionao, kwani ni tofauti na yale yanayotumiwa na wanafunzi wa shule ya msingi.
Kauli yake inaungwa mkono na mwalimu wa zamani wa madarasa ya awali, Frednanda Komba, anayesema darasa hilo lina nguvu katika kuamua hatima ya mtoto katika elimu ngazi za juu.
Amesema uwepo wa walimu waliobobea katika ngazi hiyo kutawafanya wanafunzi kupata maarifa stahiki, na hata wanapoingia darasa la kwanza walimu wanakuwa hawana mzigo mkubwa wa kufundisha.
“Wakitoka kwetu wanajua kuumba maneno, kuhesabu, kuandika. Akili ya mtoto inakuwa imeshajiandaa kwa ajili ya mambo makubwa mbele. Hii iliweka tofauti sana na wale ambao hawajapita darasa hili la awali,” amesema.
Amesema hayo yalienda sambamba na utumiaji wa mbinu mbalimbali za ufundishaji, ikiwemo kuandika chini, nyimbo, michezo; hali iliyowafanya watoto kukumbuka kwa urahisi kile walichofundishwa.
Katika hilo, Ofisi ya Rais – Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), kupitia bajeti yake kwa mwaka 2025/26, ilieleza wanaendelea kutekeleza utoaji wa elimu ya awali katika shule za msingi kwa ufanisi kupitia mazingira na miundombinu iliyoboreshwa.
Kupitia jitihada zilizofanyika hadi sasa, zimechangia kuongeza idadi ya wanafunzi wa darasa na shule zenye madarasa ya awali.
“Hadi sasa shule zimeongezeka kutoka 16,355 hadi 18,011, sawa na asilimia 10.12. Pia kupitia uratibu, usimamizi na uendeshaji wa elimu ya awali, msingi na sekondari nchini kupitia mamlaka za Serikali za Mitaa, nako shule zenye madarasa ya awali za Serikali zipo 18,011,” alisema Waziri wa Tamisemi, Mohammed Mchengerwa.