Wanaoutaka urais Tanzania, Zanzibar kupitia CUF kuhojiwa kesho

Dar es Salaam. Watiania wa urais wa Tanzania na Zanzibar kwa tiketi ya Chama cha Wananchi (CUF), kesho Jumatatu Agosti 4, 2025 wanatarajia kuanza kuhojiwa na kamati ya uongozi ya chama hicho kujiridhisha iwapo watakuwa wamekidhi sifa stahiki.

Hatua hiyo ni baada ya kamati ya uongozi kuketi kwa siku mbiliĀ  jana na leo Jumapili, Agosti 3, 2025 kuandaa mazingira ya kuwahoji pamoja na kufanya maandalizi ya mkutano mkuu wa Baraza la Kuu la Uongozi la chama hicho utakaofanyika Jumatano Agosti 6 na 7, 2025 wa kumpata mgombea urais wa Tanzania na Zanzibar.

Watiania wa urais wa Tanzania wanaotarajiwa kuhojiwa makao makuu ya chama hicho, Buguruni jijini Dar es Salaam wapo watatu ambao ni Rose Kahoji, Kiwale Mkungutila na Gombo Samandito huku jina la Chief Lutalosa Yemba likiondolewa baada ya kushindwa kurejesha fomu.

Vilevile, kwa urais wa Zanzibar wapo watiania watatu.

Akizungumza na Mwananchi, Mkurugenzi wa Utawala wa Chama hicho, Maole Ruchilingulo amesema maandalizi ya kamati ya uongozi kuwahoji katika mchakato wa kumpata mgombea mwenye sifa zilizokamilika kushindana na vyama vingine yamekamilika.

“Kesho kuanzia saa 2:00 asubuhi shughuli ya kuwahoji itaanza na wagombea wote watafika hapa ofisi za makao makuu ya chama Buguruni, ambapo atakuwa anaitwa mmoja baada ya mwingine,” amesema Ruchilingulo.

Shabaha ya kuwahoji, Ruchilingulo amesema wanajua wagombea wote ni wazuri lakini kulingana na unyeti na upekee wa nafasi wanayohitaji ni lazima wapate mtu mmoja bora kati ya waliojitokeza.

“Tutakuwa na wagombea sita kati ya hao wanaowania kupitishwa kugombea urais wa Tanzania wapo watatu, ingawa waliochukua fomu walikuwa wanne lakini mmoja hakurejesha kwa hiyo hatakuwa sehemu ya wanaohojiwa, lakini Zanzibar wapo watatu pia kwa hiyo kesho atakuwa anaitwa mmoja baada ya mwingine kuhojiwa,” amesema Ruchilingulo.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Mawasiliano wa chama hicho, Mohamed Ngulangwa amesema hatua ya kuwahoji watiania hao ni moja ya maandalizi ya mkutano Mkuu wa Baraza Kuu la chama utakaofanyika Agosti 6 na 7, 2025.

“Tunataka hadi kufikia Agosti 9, 2025 tuwe tumeshampata mgombea wa urais atakayepeperusha bendera ya chama chetu kwa kushindana na vyama vingine kwenye Uchaguzi Mkuu 2025,” amesema Ngulangwa.

CUF wanaanza mchakato huo wakati baadhi ya vyama vimekwisha wapata wagombea wa urais na makamu kwa Tanzania raba na Zanzibar, vikiwamo CCM, TLP na NCCR- Mageuzi.