Washauriwa kutumia AI kutatua migogoro ya kisheria

Unguja. Wakati matumizi ya Akili Unde (AI) yakiendelea kushika kasi duniani, wasaidizi wa sheria kisiwani hapa wametakiwa kujifunza teknolojia hiyo kwa lengo la kuitumia kutatua migogoro ya kisheria kwa haraka na ufanisi.

Hayo yameelezwa leo, Jumapili, Agosti 3, 2025, na Katibu Mtendaji wa Baraza la Vijana Zanzibar, Ali Haji Hassan, wakati akifungua mafunzo ya Akili Undea kwa wasaidizi wa sheria na maofisa wa msaada wa kisheria yaliyofanyika Mjini Unguja.

“Tuyatumie mafunzo haya kutatua migogoro ya kisheria ndani ya jamii na kutoa huduma kwa makundi yenye mahitaji maalum kwa njia bora, nafuu, na yenye ufanisi. Hivyo, wakati umefika kwa watendaji kutumia teknolojia ya kisasa katika kutatua changamoto za kisheria zinazoikumba jamii,” amesema Haji.

Pia, amesisitiza kuwa matumizi ya AI yatawasaidia wananchi, hasa wale wa vijijini, kupata huduma za msaada wa kisheria bila kusafiri umbali mrefu, kupunguza gharama na muda wa upatikanaji wa haki.

Amefafanua kuwa Akili Unde ni mfumo wa kisasa wa teknolojia unaotumika kusaidia kurahisisha mawasiliano na kutatua changamoto mbalimbali, ikiwa ni pamoja na masuala ya kisheria. Mfumo huo umeelezwa kusaidia kukuza utawala bora na kuongeza uwajibikaji katika taasisi zinazotoa huduma kwa wananchi.

Kwa upande wake, Ofisa Sheria wa Baraza la Mji Kaskazini B, Unguja, Asya Muhammed Mzee, amesema mafunzo hayo yamekuwa na manufaa makubwa kwa wasaidizi wa sheria kwani yamewaongezea uwezo na ujuzi wa kitaaluma katika kushughulikia changamoto za wananchi kwa haraka na kwa njia rafiki.

“Kupitia mafunzo haya, tutaweza kuongeza kasi ya utatuzi wa changamoto za kisheria zinazowakabili wananchi na kuwasaidia kupata haki zao bila kuchelewa,” amesema.

Mafunzo hayo yametolewa na Wizara ya Katiba na Msaada wa Kisheria kupitia Ofisi ya Rais, Katiba, Sheria, Utumishi na Utawala Bora, chini ya ufadhili wa UNDP kupitia Mradi wa Uwezeshaji Wananchi Kisheria Awamu ya Pili (LEAP II).