Baadhi ya wawakilishi wa serikali waliohudhuria mkutano huo.
Mkurugenzi wa Uchaguzi wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi, Ndg.Kailima Ramadhani akitoa mada wakati wa ufunguzim wa mkutanio wa Tume na Wazalishaji Maudhui Mtandaoni kuhusu uchaguzi Mkuu wa Mwaka 2025. Kikao hicho cha siku moja kilifanyika jijini Dar es Salaam leo Agosti 03 , 2025.Picha ya pamoja ya washiriki
***********
Na Waandishi wetu, Dar es Salaam
Mwenyekiti wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi, Mhe. Jaji wa Mahakama ya Rufaa Jacobs Mwambegele, amewahimiza wazalishaji wa maudhui mtandaoni kutumia majukwaa yao ya kidijitali kuhamasisha wananchi kujitokeza kwa wingi kupiga kura katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025.
Akizungumza leo tarehe 03 Agosti, 2025, jijini Dar es Salaam wakati wa ufunguzi wa Mkutano wa Kitaifa kati ya Tume na Wazalishaji wa Maudhui Mtandaoni, Mhe. Mwambegele amewapongeza wazalishaji hao kwa ushirikiano walioutoa kwa Tume katika hatua mbalimbali za maandalizi ya uchaguzi.
Mhe. Mwambegele amewasihi wazalishaji hao wa maudhui kuendelea kuwa daraja muhimu kati ya Tume na wananchi kwa kutoa taarifa sahihi na kwa wakati.
“Tuna imani kuwa tutazidi kushirikiana nanyi kwa karibu zaidi, na mtatumia nafasi zenu kuwapatia wananchi taarifa sahihi kuhusu maendeleo ya maandalizi ya Uchaguzi Mkuu wa 2025 na kuwahamasisha kushiriki kikamilifu kwa kupiga kura,” amesema Mhe. Mwambegele.
Amebainisha kuwa Tume inatambua mchango wa wazalishaji wa maudhui mtandaoni katika njia mbili kuu. Kwanza, kama daraja la mawasiliano kati ya Tume na wadau, na pili, kama wadau wa moja kwa moja wa mchakato wa uchaguzi.
“Tume inathamini kazi yenu ya kuandaa, kuchapisha na kusambaza taarifa kupitia majukwaa mbalimbali ya kidijitali kama mitandao ya kijamii, blogu, tovuti na majukwaa ya video kama YouTube,” ameongeza.
Akizungumzia nafasi ya vijana katika uchaguzi, Mhe. Mwambegele amesisitiza umuhimu wa mawasiliano ya kidijitali kwa kundi hilo, akiwahimiza wazalishaji hao wa maudhui kutumia ubunifu wao kwa kutumia michoro, video na ujumbe wenye mvuto ili kuwafikia wapiga kura kwa njia rahisi na ya kuvutia.
Amesema lengo kuu la mkutano huo ni kujadili hatua zilizofikiwa katika maandalizi ya uchaguzi, kubadilishana mawazo, na kusikiliza changamoto zinazowakabili wazalishaji wa maudhui mtandaoni ili kutafuta suluhisho kwa wakati.
“Mkutano huu si wa upande mmoja; ni jukwaa la mawasiliano ya pande mbili ambalo linawapa fursa ya kueleza changamoto zenu na kusaidia kuboresha utekelezaji wa shughuli za uchaguzi,” ameeleza Mhe. Mwambegele.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Uchaguzi Bw. Kailima Ramadhani, amehimiza waandaaji wa maudhui mtandaoni kutumia majukwaa yao kutoa habari sahihi, na zilizothibitishwa na kufanyiwa utafiti.
Ameongeza kuwa majukwaa hayo ya kidijitali yanasaidia kurahisisha upokeaji wa taarifa za Tume na kuwafikia wananchi kwa haraka.
Aidha, Bw. Kailima amewahimiza wazalishaji wa mtandaoni kutoa taarifa za mara kwa mara kuhusu mchakato wa Uchaguzi Mkuu wa 2025, ikiwa ni pamoja na kuitumia kauli mbiu ya uchaguzi “Kura Yako Haki Yako, Jitokeze Kupiga Kura” ili kuhamasisha wananchi kujitokeza kwa wingi tarehe 29 Oktoba, 2025.
Mkutano kati ya Tume na Wazalishaji wa Maudhui Mtandaoni ni mfululizo wa mikutano ya Tume na wadau wa uchaguzi ambayo ilianza tarehe 27 Julai, 2025. Mikutano hiyo inatarajiwa kuhitimishwa tarehe 04 Agosti, 2025 kwa wahariri na waandishi wa vyombo vya habari kupatiwa mafunzo.