Winga akaribia kutua Singida Black Stars

TIMU ya Singida Black Stars inakaribia kumsajili nyota wa Stand United ‘Chama la Wana’, Yusuph Khamis baada ya mabosi wa kikosi hicho kuvutiwa na uwezo wake aliouonyesha kwenye Ligi ya Championship msimu uliopita.

Taarifa ambazo Mwanaspoti imezipata zinaeleza mabosi wa Singida Black Stars wanamfuatilia kwa ukaribu mchezaji huyo, ambaye msimu uliopita akiwa na Stand aliifungia mabao mawili, huku akiisaidia kumaliza nafasi ya tatu kwenye msimamo ikikusanya pointi 61.

Nafasi hiyo ya tatu iliiwezesha kucheza mechi za mtoano kwa ajili ya kusaka tiketi ya kucheza Ligi Kuu Bara msimu ujao 2025-2026, huku ikianza kwa kupambana na Geita Gold iliyomaliza ya nne na pointi 56 na kuiondosha kwa jumla ya mabao 4-2.

Baada ya hapo, Stand ikakutana na Fountain Gate, ambapo ilitolewa kwa kuchapwa jumla ya mabao 5-1, baada ya mechi ya kwanza kupoteza kwa mabao 3-1, huku ile ya marudiano ikachapwa 2-0.

Mtu wa karibu na mchezaji huyo, aliliambia Mwanaspoti hadi sasa mazungumzo ya kujiunga na Singida Black Stars yanaendelea, ingawa bado hakuna makubaliano rasmi yaliyofikiwa, japo muda wowote kuanzia sasa yanaweza kukamilika pia kwa sababu yupo huru.

“Mkataba wake na Stand umeshamalizika na sasa kinachoendelea ni makubaliano binafsi kati ya mchezaji na uongozi tu wa Singida, haiwezi kuleta shida kwa sababu mwenyewe ameonesha utayari wa kubadilisha mazingira,” kilisema chanzo hicho.

Nyota huyo ameonyesha kiwango kizuri kwa msimu wa 2024-2025, katika Ligi ya Championship na sasa Singida Black Stars inamuona ni mtu muhimu wa kuongeza nguvu, ambapo alijiunga na kikosi cha Stand United baada ya kuachana na Pamba Jiji ya Mwanza.