Beki Mtanzania ajumuishwa Morocco | Mwanaspoti

ALIYEKUWA nahodha wa Simba Queens, Violeth Nickolaus amejumuishwa kwenye kikosi cha FC Masar ambacho kipo Morocco kwa ajili ya maandalizi ya msimu mpya wa Ligi Kuu ya Wanawake ya Misri.

Hadi sasa Masar haijamtambulisha nyota huyo wa timu ya taifa ya wanawake, Twiga Stars, licha ya yeye mwenyewe kubadilisha utambulisho wake kwenye mitandao ya kijamii akiliweka chama hilo.

Kwa mujibu wa wakala wa mchezaji huyo, Amosi Mlandali, tayari Violeth amesaini mkataba wa miaka miwili, kilichobaki ni timu yenyewe kumtambulisha.

“Alishasaini mkataba ndiyo maana anaonekana mazoezini na timu, kilichobaki ni wao wenyewe na michakato yao, ila tulishafanya biashara,” alisema Mlandali.

Beki huyo anaungana na Mtanzania mwenzake, Hasnath Ubamba, ambaye alikuwa kikosini hapo kwa takribani misimu mitatu mfululizo akitokea Fountain Gate Princess.

Kijumla hadi sasa kuna wachezaji wanne wa Kitanzania wanaokipiga Ligi ya Misri wakicheza na kuonyesha kiwango bora, Ubamba, Violeth, Suzana Adam, na Maimuna Hamis ‘Mynaco’.