Moshi. Chama cha Mapinduzi (CCM), kimetoa ilani yake ya uchaguzi 2025–2030 na moja ya ahadi ni kumalizia mchakato wa kuandika Katiba mpya, ambayo ni ndoto ambayo haijakamilika tangu Tanzania iingie katika mfumo wa vyama vingi, mwaka 1992.
Safari rasmi ya kuanza kuandika Katiba mpya ilianza mwaka 2011, baada ya Rais wa awamu ya nne, Jakaya Kikwete, kutangaza kuwa nchi inahitaji Katiba mpya itakayojali masuala mbalimbali ya kijamii, kisiasa na mabadiliko ya kiuchumi.
Kikwete alitoa salamu zake za mwaka mpya, akisema anataka awaachie Watanzania kumbukumbu inayoishi (legacy), kwa kuhakikisha Katiba mpya inaandikwa kuchukua nafasi ya Katiba ya sasa, iliyoandikwa mwaka 1977.
Aprili 2014, Kikwete akatangaza kuunda Tume ya Mabadiliko ya Katiba chini ya uenyekiti wa Jaji Joseph Sinde Warioba, na ikapewa miezi 18 kukamilisha kazi ya kukusanya maoni, kazi waliyoifanya kwa weledi na uzalendo.
Bunge Maalumu la Katiba likaundwa mwaka 2014, ambapo wajumbe walipitia, kujadili, kurekebisha, kufuta na kuandika upya ibara za Rasimu ya Katiba ya Jaji Warioba, na kuja na Katiba Inayopendekezwa, ikifuta baadhi ya maoni ya wananchi.
Kutokana na kukosekana kwa maridhiano ya kisiasa na ya kitaifa, mchakato wa Katiba mpya haukufika hatua ya kupiga kura ya “Ndiyo” au “Hapana,” na tangu mwaka huo 2014, imekuwa ni mfupa uliomshinda fisi.
CCM, kupitia ilani yake ya mwaka 2015–2020, ikatoa ahadi ya kukamilisha mchakato wa Katiba mpya, lakini alipoingia Rais wa awamu ya tano, John Pombe Magufuli (marehemu), akaiweka pembeni ahadi hiyo, akisema si kipaumbele chake.
Msimamo huo wa Serikali ulijidhihirisha katika Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya 2020–2025, ambapo katika kurasa 303 za ilani hiyo, suala la kumalizia mchakato wa Katiba mpya halikuwepo. Lakini Juni 22, 2022, CCM ikabadili gia angani, ambapo Katibu wa Itikadi na Uenezi wa wakati huo, Shaka Hamdu Shaka, aliutangazia umma kwamba chama hicho tawala kimekubali mchakato wa Katiba mpya uangaliwe kwa maslahi ya Taifa.
Pengine ni kutokana na msimamo huo mpya, CCM katika ilani yake ya 2025–2030, katika kifungu cha 47(ii) cha Utawala Bora, imeingiza suala la mchakato wa kuandikwa kwa Katiba mpya.
Katika kifungu hicho, CCM inasema katika miaka mitano ijayo, itaielekeza Serikali kuhuisha na kukamilisha mchakato wa Katiba mpya, ahadi ambayo wanazuoni na wachambuzi wa kisiasa wanaitilia shaka kama kweli itatekelezwa.
Demokrasia, mapambano ya rushwa
Katika ilani hiyo, Serikali ya CCM imeahidi kuimarisha misingi ya demokrasia kwa kuboresha mazingira wezeshi ya wananchi kushiriki katika shughuli mbalimbali za kijamii, kiuchumi na kisiasa kwa kuzingatia maadili na sheria za nchi.
Imeahidi pia kuimarisha mapambano dhidi ya rushwa na ufisadi, kwa kuzuia na kudhibiti vitendo vya rushwa na kuchukua hatua kali za kisheria na kinidhamu dhidi ya viongozi na watumishi wa umma wanaojihusisha na vitendo hivyo.
Pia, imeahidi kuendelea kuimarisha taasisi za utawala bora, maadili na uwajibikaji, kama vile Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi katika Utumishi wa Umma, Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa Tanzania (Takukuru), na Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora Tanzania.
Lengo ni kuhakikisha taasisi hizo zinaendelea kuimarisha Serikali za mitaa kama nyenzo ya demokrasia na maendeleo ya wananchi, na kuendelea kuimarisha uhuru wa asasi za kiraia na vyombo vya habari kama taasisi muhimu katika kuimarisha uwajibikaji. Katika kuimarisha taasisi za kitaaluma katika kuishauri Serikali na wadau wengine wa maendeleo, itatungwa sheria ya kuundwa kwa bodi za kitaaluma na Baraza Jumuishi la Kitaaluma, ambazo zitakuwa na jukumu la kuishauri Serikali.
Haki jinai ilivyokumbukwa
Katika kuimarisha mnyororo wa haki jinai, na kwa kuzingatia mapendekezo ya Tume ya Rais ya Haki Jinai, CCM itaielekeza Serikali kuchukua hatua mbalimbali, ikiwemo kuhuisha mfumo wa nyumba kumi kisheria.
Mbali na hilo, itaimarisha matumizi ya mitandao katika malipo na uhamishaji wa fedha kimtandao, na udhibiti wa matumizi ya fedha taslimu, pamoja na kuimarisha matumizi ya kamera za ulinzi (CCTV) na Tehama katika kubaini na kuzuia uhalifu na wahalifu.
Katika kusikia kilio cha wadau wa haki jinai, CCM itaielekeza Serikali kuanzisha mamlaka mpya na huru ya upelelezi inayojitegemea, itakayojulikana kama Ofisi ya Taifa ya Upelelezi, itakayokuwa na jukumu la kupeleleza makosa yote ya jinai.
Jambo lingine ni kuboresha mishahara na maslahi ya wafanyakazi, wakiwemo askari wa Jeshi la Polisi, Jeshi la Magereza na Uhamiaji, ikiwemo kupitia upya umri wa kustaafu na mafao ya pensheni kwa askari.
Akitoa maoni binafsi juu ya ahadi hizo za CCM, Rais wa Chama cha Mawakili nchini (TLS), Boniface Mwabukusi, amesema ahadi ya kukamilisha mchakato wa Katiba mpya ni ya msingi na ya muda mrefu, na imekuwa kilio cha Watanzania wengi.
“Ilani ya 2015 iliahidi Katiba mpya, lakini mchakato ulizimwa kimya kimya kijeuri tu, na hakuna aliyehoji ndani au nje ya CCM. Hatujaambiwa kwa nini walisitisha kwa wakati ule, na kwa nini wanaona sasa inafaa kufanya hivyo.
“Ili mchakato huu uwe na maana, ni lazima pawe na ushirikishwaji wa kweli wa wananchi, si mchakato wa kuharakishwa au kurudishwa kwenye Katiba Pendekezwa iliyokataliwa na umma mwaka 2014,” amesisitiza Wakili Mwabukusi.
Kuhusu kuanzishwa kwa Ofisi ya Taifa ya Upelelezi wa Makosa ya Jinai, Wakili Mwabukusi amesema hilo linaweza kuwa na manufaa endapo lengo lake si kuunda taasisi nyingine ya kisiasa ya kuminya haki, bali kuondoa siasa ndani ya Polisi.
“Hii itasaidia kuhakikisha upelelezi wa makosa ya jinai unafanywa kitaalamu, kwa weledi na bila upendeleo. Tumeona uundwaji wa Ofisi ya DPP hakujasaidia. Tumeona bado mashauri mengi yenye uonevu na sura ya kisiasa,” amesema.
“Hii itakuwa na maana tu iwapo mfumo wa uendeshaji wake utakuwa huru kutoka kwa mamlaka ya kisiasa, hasa kutoka kwa Waziri wa Mambo ya Ndani au Rais. Vinginevyo, ni kupanua mamlaka ya kiimla chini ya jina jipya tu,” amedai.
Kuhusu kuimarisha misingi ya demokrasia, Wakili Mwabukusi amesema tamko hilo katika ilani linavutia, lakini bila marekebisho muhimu ya Sheria za Uchaguzi, Tume Huru ya Uchaguzi na utendaji wa Jeshi la Polisi, itakuwa ni kazi bure.
“Lazima Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa itoe haki kwa vyama vya upinzani, uhuru wa vyombo vya habari na kusitishwa kwa matumizi ya nguvu kwa waandamanaji. Misingi ya demokrasia haitaimarika kwa kauli au ahadi,” amesema.
Kwa upande wake, Mratibu wa Kitaifa wa Mtandao wa Kutetea Haki za Binadamu (THRDC), Onesmo Ole Ngurumwa, amesema wanashukuru CCM imechukua mambo mengi ambayo waliwaeleza na kuyaingiza katika ilani yao ya 2025–2030.
“Masuala ya Katiba mpya, utawala bora, rushwa — tunaona wameyazingatia. Wamezungumza kuwa Katiba mpya itapatikana baada ya uchaguzi, jambo ambalo ni la kheri. Sisi tulisema siyo vyema kutafuta Katiba na mihemko ya uchaguzi,” amesema.
Wakili David Shilatu, naye amesema, “Kwenye hili la Katiba, nadhani yatupasa kuanza upya kabisa, ili tupate Katiba itakayoandikwa na Watanzania wote. Lakini kama itashindikana, yatupasa kuanzia katika Katiba ya Jaji Warioba.”
Wachambuzi wa siasa wafunguka
Kwa upande wake, mchambuzi wa masuala ya kisiasa, kijamii na kiuchumi, Conrad Kabewa, amesema ,“Ahadi ya Katiba mpya ilitakiwa walau iwekewe na ratiba yake, ili tuone ni kipaumbele gani cha CCM. Tunaweza kujikuta tunapwaga hivyo hivyo hadi 2029 ndipo mchakato uanze, ili kuipa Serikali iliyopo nafasi ya kutawala.”
Mchambuzi mwingine wa masuala ya kisiasa, kijamii na kiuchumi, Edwin Soko, ambaye pia ni Mwenyekiti wa Taasisi ya Vyombo vya Habari Kusini mwa Afrika (MISA–TAN), amesema ilani ya CCM ina mwangaza na inatoa mwelekeo mzuri.
“Nimevutiwa na ahadi na maelekezo ya CCM, kwa sababu nyingi zinaendana na Dira 2050, ambayo inaakisi mambo mengi ya kiuchumi, kisiasa na kijamii. Kwangu ni ilani ambayo imefanyiwa kazi vizuri,” amesema Soko.
Soko amesema hofu yake ni wale watakaoingia katika vyombo vya Dola kama mawaziri, wabunge na madiwani, kama wanaifahamu vyema maana imebeba mambo mazito na inahitaji watu wenye uwezo na maono ya kuitekeleza.