CHAMA la kiungo Mtanzania, Charles Mmombwa, Floriana FC imetolewa kwenye michuano ya kufuzu kucheza Europa Conference League baada ya kulazimishwa sare ya bao 1-1 dhidi ya Balkani.
Timu hiyo ilipata nafasi ya kushiriki mechi za mtoano za michuano mikubwa Ulaya baada ya kumaliza nafasi ya tatu kwenye msimamo wa Ligi Kuu ya Malta, maarufu kama Maltese Premier League.
Floriana imeshindwa kuendelea na raundi ya tatu kufuzu michuano hiyo baada ya kutolewa kwa jumla ya mabao 5-3, ikifungwa ugenini mabao 4-2 na sare ya 1-1 nyumbani.
Baada ya kutolewa, Mmombwa alisema, “Safari yetu ya Ulaya imefikia tamati, lakini tunaondoka tukiwa tumeinua vichwa juu, tunajivunia mapambano, ari, na uwezo tuliouonyesha.”
Chama hilo la Mmombwa lilianzia raundi ya kwanza kwa ushindi wa jumla ya mabao 5-3 dhidi ya Haverfordwest, likatinga raundi ya pili na kukutana na Ballkani kabla ya juzi kutolewa.
Mtanzania huyo alicheza mechi zote nne, mbili za raundi ya kwanza na mbili za raundi ya pili, kwa dakika zote 90 akifunga bao moja.