Dk Kusiluka awataka makatibu wakuu kuacha kufanya kazi kwa mazoea

Kibaha. Katibu Mkuu Kiongozi, Dk Moses Kusiluka amewataka makatibu wakuu na naibu katibu wakuu kuacha kufanya kazi kwa mazoea na wahakikishe malengo ya Dira 2050 ikiwamo kuwa na Pato la Taifa (GDP) la Dola 1 trilioni za Marekani linafikiwa.

Dk Kusiluka amesema hayo leo Jumatatu, Agosti 4, 2025 wakati akifungua kikao cha viongozi hao cha siku mbili kinachofanyikia Shule ya Uongozi ya Mwalimu Nyerere, Kibaha, Mkoa wa Pwani.

Kikao hicho kinafanyika takribani wiki mbili zimepita tangu Rais Samia Suluhu Hassan alipoizindua Dira 2050 jijini Dodoma Julai 17, 2025 huku akitoa maelekezo kwa watendaji Serikali kuhakikisha wanaisimamia kwenye utekelezaji wake.

Katika hotuba yake ya ufunguzi wa mafunzo, katibu mkuu huyo amewataka washiriki kufahamu kikamilifu na kuelewa Dira 2050 pamoja na maudhui ya Mpango wa Maendeleo wa Muda Mrefu (LTPP).

Dk Kisiluka amewataka washiriki wote kuchangia kwa dhati ili kuandaa LTPP inayotekelezeka na halisia huku akisisitiza: “ Huu si wakati wa kuendelea na kazi kwa mazoea, kupitia LTPP hiyo, Tanzania inatarajiwa kufikia malengo ya Dira2050 ikiwamo kuwa na Pato la Taifa (GDP) la Dola trilioni moja za Kimarekani ifikapo mwaka 2050.”

Amesisitiza makatibu wakuu wanapaswa kutoa mchango mpana usioishia tu katika wizara zao, bali kwa masilahi ya Taifa zima, kwa kuwa huwa wanabadilishana wizara mara kwa mara.

Kikao hicho pia kimehudhuriwa na Naibu Mwanasheria Mkuu wa Serikali aliyewakilishwa na Mwandishi Mkuu wa Sheria, Onorius Njole, wajumbe wa kikosi kazi cha kuandaa LTPP wakiongozwa na Dk Asha-Rose Migiro, baadhi ya wajumbe wa sekretarieti ya Baraza la Mawaziri, pamoja na watumishi na Menejimenti ya Tume ya Taifa ya Mipango (NPC).

Katibu Mkuu wa Ofisi ya Rais, Mipango na Uwekezaji, Dk Tausi Kida amemshukuru Dk Kusiluka kuchukua muda wake kushiriki kikao hicho muhimu kwa utekelezaji wa Dira 2050 katika kupitia maandalizi ya Mpango wa Maendeleo wa Muda Mrefu wa miaka 25, muda wa kati na mfupi ya miaka mitano na mmoja, mtawalia.

Akitoa maelezo kuhusu utekelezaji wa Dira 2050, Katibu Mtendaji wa NPC, Dk Fred Msemwa amewakumbusha maagizo yaliyotolewa na Rais Samia wakati wa uzinduzi wa Dira 2050 kuwa yazingatiwe kikamilifu wakati wa utekelezaji.

Dk Msemwa ametaja maagizo hayo ni mabadiliko ya mtazamo katika utendaji kazi, kila wizara kufanya uhakiki wa sera zilizopo kama zinaendana na Dira 2050 na kufanyia marekebisho sheria ili ziendane na dira hiyo.

Pia, kushirikisha sekta binafsi kama mhimili mkuu, kuimarisha mifumo ya ufuatiliaji na tathmini, pamoja na kuendesha kampeni ya uelimishaji wa umma ili kila Mtanzania aelewe maudhui ya Dira 2050.