DKT MPANGO AWATAKA WANAMICHEZO KULETA USHINDA TANZANIA

:::::

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Philip Mpango ametoa wito kwa wanamichezo kushiriki mashindano ya Jumuiya ya Madola kama washindani wa kweli ambao wataonesha vipaji na kuiletea Tanzania heshima.

 

Makamu wa Rais ametoa wito huo wakati akipokea Kifimbo cha Mfalme wa Uingereza kuelekea Mashindano ya Michezo ya Jumuiya ya Madola itakayofanyika Glasgow Uingereza mwaka 2026. Amesisitiza umuhimu wa taasisi na mashirikisho ya michezo kuibua, kukuza na kuwezesha vipaji hasa miongoni mwa vijana wanaobeba matumaini ya Taifa.

 

Pia Makamu wa Rais ametoa rai kwa wadau wote, wakiwemo wakala wa Serikali, mashirikisho ya michezo, wadau wa maendeleo na sekta binafsi kuungana pamoja kwa ushirikiano wa kimkakati ili kuhakikisha wanamichezo wa Tanzania wanapewa mafunzo, nyenzo na msaada wa kisaikolojia unaohitajika. Amesema ni muhimu kutambua kwamba Michezo ya Jumuiya ya Madola ni zaidi ya tukio la kimichezo kwa kuwa ni sherehe ya historia ya pamoja, maadili, na ushirikiano kati ya mataifa wanachama ambayo yanaunganishwa na historia ya pamoja na ahadi ya kudumu ya amani, demokrasia na maendeleo endelevu.

 

Halikadhalika Makamu wa Rais amesema kuwasili kwa Kifimbo cha Mfalme wa Uingereza ambacho kinabeba ujumbe wa uhifadhi wa mazingira hususani udhibiti wa taka za plastiki baharini kunapaswa kuikumbusha jamii wito wa kuchukua hatua na kuwajibika katika kutunza mazingira. Amesema pia Kifimbo hicho kinatoa fursa ya kutafakari juu ya umuhimu wa maandalizi ya mapema, ya kina na yanayoratibiwa vema katika kuelekea katika Michezo ya Jumuiya ya Madola ya 2026 huko Glasgow.

 

Kwa upande wake Katibu Mkuu Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Gerson Msigwa amesema Wizara kwa kushirikiana na kamati ya olimpiki imeweka mpango mkakati wa kuanza maandalizi mapema ili kushiriki vema mashindano ya Jumuiya ya Madola. Amesema ipo fursa kubwa ya kuweza kupata medali nyingi zaidi hivyo maandalizi ya mapema yatafanyika ili kuandaa vijana katika michezo yote.

 

Amesema Serikali inawekeza kwa kiasi kikubwa katika michezo na kujenga miundombinu ikiwemo ujenzi wa mradi mkubwa wa kuendeleza michezo kama vile ujenzi wa kituo cha kuwawezesha wanamichezo wanaoshiriki Jumuiya ya Madola na Olimpiki mjini Babati. Ameongeza kwamba lengo la ujenzi wa kituo hicho mjini Babati ni kuhakikisha wanamichezo wanafanya maandalizi katika hali ya hewa rafiki kuendana na maeneo mengine Duniani yanakofanyika mashindano hayo.

 

Makamu wa Rais alipokea Kifimbo cha Mfalme wa Uingereza ambacho kilimaliza muda wake nchini Cameroon na amekabidhi Kifimbo hicho ili kiweze kuelekea nchini Ghana.