Geay aula Berlin Marathon 2025

MWANARIADHA nyota wa kimataifa wa Tanzania, Gabriel Geay ni miongoni mwa mastaa 13 ambao wamepewa mwaliko wa kushiriki mbio za Berlin Marathon 2025, Ujerumani.

Mbio hizo zitafanyika Septemba 21 na Geay anayeshikilia rekodi ya taifa ya mbio ndefu kwa muda wa saa 2:03:00 aliyoiweka katika Valencia Marathon miaka mitatu iliyopita atashiriki kwa mara ya kwanza.

Mwaka 2024, nyota huyo hakufanya vyema kutokana na changamoto ya majeraha yaliyokuwa yanamkabili, lakini 2025 alirudi kwa nguvu katika Daegu Marathon za Korea Kusini zilizofanyika Februari, akimaliza wa kwanza kwa saa 2:05:20.

Tishio kubwa kwa Geay katika mbio hizo ni Milkesa Mengesha wa Ethiopia anayetetea medali ya dhahabu aliyoshinda mwaka jana akitumia saa 2:03:17 na kuweka rekodi binafsi.

Mbali na Mengesha, Geay pia anakabiliwa na upinzani mkali kutoka kwa mshindi wa London Marathon 2025, Sebastian Sawe aliyekimbia kwa saa 2:02:27, pia akitambia rekodi binafsi ya kutumia muda wa saa 2:02:05 mbio za Valencia Marathon 2024 inayomfanya ashike nafasi ya tano katika chati ya wanariadha waliotumia muda mfupi zaidi kumaliza mbio ndefu.

Wengine ni Guye Adola, Daniel Mateiko, Kengo Suzuki, Haymanot Alew, Elfaye Deriba, Abel Kirui, Tadese Takele, Cybrian Kotut, Tesfaye Deriba naHaftu Takelu.

Geay aliliambia Mwanaspoti, anaendelea na mazoezi katika kambi iliyopo Madunga wilayani Babati, Mkoa wa Manyara na lengo lake ni kwenda kushinda na kuweka rekodi katika mbio hizo.

Alisema tayari ameshakusanya taarifa kuhusu njia za mbio hizo, hivyo anafanya maandalizi kutokana mazingira ambayo atakwenda kukimbilia.

“Ingawa ushindani utakuwepo, nimejiandaa kwenda kupambana na niwaambie tu wapenzi wa riadha Tanzania, kwa sasa niko fiti hao wababe nitaenda kushindana nao,” alisema.