Hukumu rufaa Kocha Katabazi dhidi ya TFF yasogezwa mbele

Hukumu ya rufaa ya Kocha Listoni Katabazi dhidi ya  Shirikisho la Mpira wa Miguu Nchini (TFF), kupitia bodi yake ya wadhamini, sasa kutolewa Septemba 26, 2025.

Hukumu hiyo ilipangwa kutolewa leo Agosti 4,2025 na Jaji Butamo Phillip aliyesikiliza rufaa hiyo. Hata hivyo imekwama kwa kuwa Jaji Phillip aliyepaswa kuisoma hukumu hiyo hakuwepo.Badala yake imeahirishwa na Naibu Msajili wa Mahakama hiyo mpaka  tarehe hiyo mpya.

Katika rufaa hiyo Kocha Katabazi  anapinga  uamuzi Mahakama ya Hakimu Mkazi, Dar es Salaam,  Kisutu, iliyotupikia kesi yake aliyokuwa anapinga uamuzi wa Kamati ya Maadili ya TFF kumfungia maisha yake yote kujishughulisha na masuala ya soka.

Katabazi ambaye anajitambulisha kuwa ni mdau wa mchezo wa soka na kocha wa mchezo huo mwenye leseni ya daraja C, iliyotolewa na TFF, alifungiwa na TFF kujishughulisha na masuala ya soka ndani na nje ya nchi maisha yake yote, mwaka 2021.

Alifungiwa baada ya kuliandikia BMT barua Juni 15, 2021 akilishtaki TFF kuwa limeshindwa kusimamia mchezo huo kulingana na Sheria, Kanuni na miongozo yake.

Kufuatia barua hiyo, aliitwa katika Kamati ya Maadili, lakini hakuhudhuria badala yake alijibu kuwa yeye si mwanachama wa Chama cha Makocha Tanzania (Tafca) ambacho kiko chini ya usimamizi wa TFF, hivyo yeye si mwanachama wa TFF.

Juni 24, 2021 TFF lilichapisha katika tovuti yao uamuzi wa kumfungia Katabazi maisha kujishughulisha na masuala ya soka ndani na nje ya nchi.

Hata hivyo, mwaka 2024 alifungua kesi Mahakama ya Kisutu dhidi ya TFF na wadhamini wake akipinga uamuzi huo wa kufungiwa.

Katika kesi hiyo ya madai namba 14708/2024, pamoja na mambo mengine alidai kuwa Kamati ya Maadili ya TFF haikuwa na mamlaka ya kutoa uamuzi huo dhidi yake kwa kuwa Kanuni za Maadili za TFF, Toleo la Mwaka 2021, zilizotumika kumfungia si halali.

Alidai kuwa kanuni hizo hazijasajiliwa na BMT kwa mujibu wa matakwa ya Sheria namba 12 ya mwaka 1967 na marekebisho yake, na hivyo kuzifanya kuwa batili kutumika dhidi ya wanachama wake na mtu mwingine yeyote.

Katabazi alidai kuwa amri hiyo iliingilia haki yake ya kufanya kazi katika nyanja ya soka na hivyo kumkosesha fursa ya kupata mshahara na kipato kwa ajili ya kuendeleza maisha yake ya kila siku na familia yake, na kumsababishia maumivu ya kisaikolojia.

Hivyo aliiomba mahakama iiamuru TFF imlipe Sh600 milioni kama fidia ya madhara ya jumla aliyoyapata kutokana na uamuzi huo wa kumfungia maisha uliotolewa kwa maksudi, kimakosa na kwa nia ovu.

Pia aliomba alipwe  Sh100 milioni kama fidia ya adhabu kwa kitendo cha wadaiwa kutoa uamuzi huo wakijua kuwa hawana mamlaka ya kisheria kuchukua hatua hiyo dhidi yake, riba ya kiwango cha Mahakama kwa cha tuzo (fedha ambazo ingeamuriwa alipwe) na gharama za kesi.

Vilevile aliiomba mahakama itoe zuio la matumizi ya Sheria (Katiba) na Kanuni za Maadili za TFF, kwa madai kuwa si vyombo halali kwa kutokusajiliwa kwa utaratibu na unaofaa.

Miongoni mwa vielelezo alivyoviwasilisha  mahakamani ni barua ya BMT ya Juni 13, 2022 iliyothibitisha kuwa yeye si mwanachama wa TFF.

Hata hivyo, Mahakama ya Kisutu iliitupilia mbali kesi hiyo kufuatia pingamizi la awali lililoibuliwa na TFF.

Katika uamuzi wake uliotolewa na Hakimu Mfawidhi wa Mahakama hiyo, Hakimu Mkazi Mkuu,  Franco Kiswaga ilikubaliana na sababu ya pingamizi la TFF kuwa haikuwa na mamlaka ya kuisikiliza kesi hiyo.

Hakimu Kiswaga alisema kuwa hakuna ubishi kwamba  Katabazi ni mwanachama wa TFF.

Hivyo alikubaliana na wakili wa TFF, Rahim Shaaban kuwa kwa mujibu wa Katiba ya TFF mwanachama asiyeridhika na uamuzi wa Kamati ya Maadili anapaswa kukata rufaa katika Kamati ya Rufaa ya Maadili, lakini haukufuata utaratibu huo.

Hakimu Kiswaga alisema kuwa kwa Katiba ya TFF, shirikisho hilo litakuwa na mamlaka ya kushughulikia migogoro yote ya soka ndani na mwanachama asiyeridhika anaweza kupeleka shauri lake katika Mahakama ya Usuluhishi wa Michezo (CAS) baada ya kumaliza hatua zote ndani ya FFF.

Hivyo alisema kuwa mahakama hiyo haikuwa na mamlaka ya kusikiliza kesi hiyo kwani mlalamikaji Katabazi alipaswa kukata rufaa Kamati ya Rufaa ya Maadili na kama asingeridhika angekata rufaa CAS kama Katiba ya TFF inavyoelekeza.

Katabazi hakuridhika na uamuzi huo, hivyo alikata rufaa Mahakama Kuu  pamoja na sababu nyingine, akidai kuwa  Mahakama ya Kisutu ilikosea kisheria kushughulikia pingamizi la wajibu rufani ambalo halikuwa na msingi wa kisheria na kwa kuzingatia ushahidi uliotolewa wakati wa usikilizwaji wa pingamizi.