Jamii Yakumbushwa Kutowatenga Wenye Kifafa: “Kifafa Sio Laana Wala Mkosi”

TAASISI ya Tanzania Epilepsy Organisation (TEO) imeitaka jamii kuwapa heshima, upendo, na haki sawa watu wenye ugonjwa wa kifafa, ikisisitiza kuwa hawapaswi kutengwa wala kunyanyapaliwa.

Akizungumza leo jijini Dar es Salaam, Agosti 4, 2025 wakati wa uzinduzi wa mradi maalum wa Ongea, Simama Imara, Suzana Mukoyi, aliyemwakilisha Mkurugenzi wa Taasisi hiyo, amesema mradi huo umeanzishwa kwa lengo la kuwasaidia wazazi na walezi wa watoto wenye kifafa kutambua haki zao za msingi, kupata elimu sahihi kuhusu ugonjwa huo na kutatua changamoto zinazowakabili katika malezi.

“Tumeanzisha mradi huu ili kuwajengea uwezo wale wanaolea watoto wenye kifafa na kuhakikisha jamii inaelewa kuwa watu hawa wana haki sawa na wengine,” alisema Bi. Mukoyi. Ameongeza kuwa, kwa sasa mradi umeanza katika Mkoa wa Dar es Salaam, ambako taasisi hiyo ina wanachama 1,000, huku matarajio yakiwa kufikia mikoa yote nchini. Alibainisha pia kuwa uelewa wa jamii kuhusu kifafa umeongezeka ikilinganishwa na miaka ya nyuma.

Suzana ameweka wazi kuwa mojawapo ya changamoto kubwa inayoikabili jamii ni uelewa mdogo wa walimu kuhusu ugonjwa wa kifafa na namna bora ya kuwahudumia wanafunzi wenye changamoto hiyo mashuleni.

“Baadhi ya walimu bado hawana elimu sahihi kuhusu namna ya kuwahudumia wanafunzi wenye kifafa, jambo linalowaweka hatarini watoto hawa,” ameeleza.

Kwa Upande wa Rebecca Lebi, mmoja wa wanachama wa Tanzania Epilepsy Organisation, ametoa wito kwa serikali na jamii kuhakikisha watu wenye kifafa wanapata huduma ya bima ya afya kwa urahisi, akieleza kuwa dawa nyingi zinazotibu kifafa hazipatikani kwa urahisi kupitia mifumo ya kawaida ya bima.

“Kifafa sio mkosi, sio laana, wala sio kurogwa. Ni ugonjwa kama magonjwa mengine na unaweza kumpata mtu yeyote. Huu ugonjwa hauambukizi, lakini baadhi ya jamii bado wanaamini kuwa majimaji yanayotoka kwa mgonjwa wa kifafa yanaambukiza, jambo ambalo si kweli,” amesema Rebecca kwa hisia.

Ameisisitiza jamii kutambua kuwa watu wenye kifafa wanaweza kupona na kuishi maisha ya kawaida kwa kutumia dawa na kufuata ushauri wa kitabibu.

Omary Vadenga na Elias Manade, ambao ni miongoni mwa waathirika wa kifafa, wameeleza kuwa kupitia TEO wameweza kupata elimu kuhusu namna ya kuishi na ugonjwa huo, kujitambua na kuchukua tahadhari mapema pindi dalili za kifafa zinapojitokeza. 

“Taasisi hii imetusaidia sana. Sasa tunajua dalili na tunaweza kujikinga kwa kukaa sehemu salama kabla kifafa hakijatupiga,” wamesema.

Kwa pamoja, wametoa wito kwa serikali kusaidia taasisi zinazotoa elimu kwa watu wenye kifafa, hususan mashuleni, wakisisitiza kuwa elimu hiyo huongeza ujasiri na uwezo wa kufanya kazi na kusoma kwa ufanisi. “Watu wenye kifafa wakielimishwa hujiamini, na wanakuwa na uwezo wa kushiriki kikamilifu katika shughuli za kijamii na kiuchumi,” wameeleza.