Kanuni za kutoboa Chan 2024

SHIRIKISHO la Soka Afrika (CAF), limezianika kanuni za mashindano ya CHAN 2024 upande wa kusaka timu mbili kutoka kila kundi zitakazofuzu hatua ya robo fainali.

Mashindano hayo yanayoshirikisha jumla ya timu 19 ambazo zimegawanywa katika makundi manne, yalianza Jumamosi ya Agosti 2 mwaka huu kwa mchezo wa ufunguzi kati ya wenyeji Tanzania dhidi ya Burkina Faso.

Kwa mujibu wa CAF, upangaji wa nafasi katika hatua ya makundi utafuata vigezo maalum vilivyowekwa ambavyo kwa kawaida timu yenye pointi nyingi inakuwa juu, lakini timu mbili zikiwa na pointi sawa, utaratibu ufuatao utatumika:

Kwanza itaangaliwa matokeo ya mchezo zilipokutana yalikuwaje.

Kipaumbele cha pili itaangaliwa tofauti ya mabao katika mechi zote za hatua ya makundi.

Huku kipaumbele cha tatu ni idadi ya jumla ya mabao yaliyofungwa katika mechi zote hatua ya makundi.

Endapo timu bado hazijatofautiana katika mambo yote hayo, itaangaliwa yenye nidhamu na itazingatiwa kwa mfumo wa makosa unaotoa pointi za adhabu kama ifuatavyo:

Kadi ya njano: Inapunguza pointi moja kutoka ulizonayo

Kadi nyekundu kutokana na kadi mbili za njano: Inaounguza pointi tatu kutoka ulizonazo

Kadi nyekundu ya moja kwa moja: Inapunguza pointi nne kutoka ulizonayo

Kadi ya njano na kadi nyekundu ya moja kwa moja: Inapunguza pointi tano kutoka ulizonayo

Iwapo bado hakuna utofauti, itachezeshwa droo chini ya Kamati ya Maandalizi ili kuamua nafasi.

Endapo timu zaidi ya mbili zitakuwa na pointi sawa, utaratibu utakuwa mrefu zaidi:

Kwanza, pointi zilizopatikana katika mechi kati ya timu hizo (zilizofungana) ndizo zitakazochukuliwa.

Halafu, tofauti ya mabao na idadi ya mabao yaliyofungwa baina ya timu hizo tu.

Iwapo baada ya hapo timu mbili bado hazijatofautiana, basi sheria zitarudi kutumika kwa timu hizo mbili pekee, kwa kutumia hatua zilezile kama ilivyotajwa awali.

Kama hakuna suluhisho, ndipo utendaji wa jumla wa kundi zima (tofauti ya mabao, mabao yaliyofungwa, pointi za fair play) utatumika kabla ya kuchukua hatua ya mwisho ya kuchezeshwa droo.

Mwisho wa hatua ya makundi, timu mbili bora kutoka kila kundi zitafuzu hatua ya Robo Fainali, ambazo zitaandaliwa kwa mpangilio ufuatao:

Mshindi wa Kundi A vs Mshindi wa Pili wa Kundi B

Mshindi wa Kundi B vs Mshindi wa Pili wa Kundi A

Mshindi wa Kundi C vs Mshindi wa Pili wa Kundi D

Mshindi wa Kundi D vs Mshindi wa Pili wa Kundi C