Kipa wa KVZ azitosa mbili Bara

KIPA tegemeo wa KVZ anayeidakia pia timu ya taifa ya Zanzibar, Zanzibar Heroes, Suleiman Said Abraham amezikacha timu mbili za Ligi Kuu Bara, Tabora United na Pamba Jiji na kutua Namungo.

Namungo imefanikiwa kunasa saini ya kipa huyo, baada ya kuzizidi ujanja Tabora na Pamba ambazo nazo zilikuwa zikimwinda kwa muda mrefu.

Suleiman amemwaga wino kwa mkataba wa mwaka mmoja, ikielezwa imetokana na makubaliano ya dau la Sh25 milioni, ambapo Sh15 milioni zinaingia mfukoni mwa kipa huyo na zilizobaki zinaenda kwa klabu hiyo inayoshiriki Ligi Kuu Zanzibar (ZPL).

Akizungumza na Mwanaspoti, Suleiman amethibisha kukamilisha mazungumzo baina yake, uongozi wa KVZ na Namungo na rasmi msimu ujao ataichezea timu hiyo inayoshiriki Ligi Kuu Bara.

“Nimeshakamalisha taratibu zote za utiaji saini na timu hiyo na tayari wameshaniingizia nusu ya fedha ambazo tumekubaliana, kilichobaki kuingiza fedha kwa klabu,” alisema Suleiman.

Suleiman alikiri kutua kwake Namungo anaiona njia ya kufikia lengo lake kwa sababu hamu yake ni kucheza Ligi Kuu Bara, huku akiamini ipo siku atacheza miongoni mwa timu tatu kubwa ambazo ni Yanga, Simba na Azam.

Mbali na kutamani kuzichezea timu hizo, alisema hiyo ni njia itakayomvusha hadi nje ya Tanzania.

Alisema, licha ya kuzoea maisha ndani ya KVZ lakini amejipanga vizuri kuitumia fursa hiyo na atakahakikisha anaipigania Namungo kwa uwezo wake wote kwani hadi kufikia kumsajili wameshajenga imani nzuri kutoka kwake, hivyo hatawaangusha.

Alifunguka kuwa kati ya timu ambazo zilikuwa zinamtaka, Namungo pekee ndio iliyofanikiwa kuzungumza na yeye mwenyewe bila ya kupitia katika uongozi wake ndio maana imekuwa rahisi kufanikiwa kuondoka naye.

Alisema ubora ambao aliuonyesha msimu uliopoita katika Ligi Kuu Zanzibar ndio uliofanya klabu nyingi kuvutiwa naye kwa kuisaidia timu yake kumaliza ya pili.

Kipa huyo amemaliza msimu wa 2024-25 kwa kucheza mechi 22 kati ya 30 ya Ligi Kuu Zanzibar na kuvuna clean sheet 19 akiwa miongoni mwa makipa waliofanya vizuri, kwani KVZ ilipoteza mechi mbili kati ya 30 ilizocheza ambapo Mlandege ilibeba ubingwa wa Ligi hiyo.