Korti yaelezwa washtakiwa walivyomtenda mwanachuo mwenzao

Dar es Salaam. Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu imeelezwa jinsi mshtakiwa, Mary Matogolo (22) na wenzake wawili walivyomvua nguo Magnificant Kimario, kisha kumnyoa nywele kichwani kwa kutumia kisu, huku wengine wakimwagia maji mwilini na kumtukana.

Pia wanadaiwa kupasua simu ya Magnificant, kuchoma moto nguo alizokuwa amevaa pamoja na pochi ya mkononi, vyote vikiwa na thamani ya Sh1 milioni.

Hayo yameelezwa leo Jumatatu Agosti 4, 2025 na Wakili wa Serikali, Pancrasia Protas alipowasomea maelezo ya awali washtakiwa watatu ambao ni wanafunzi wa vyuo vikuu wanaokabiliwa na mashtaka manane, yakiwamo ya kutishia kuua, kutoa taarifa za uongo mitandaoni na uharibifu wa mali.

Washtakiwa wamesomewa maelezo mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Gwantwa Mwankuga baada ya upelelezi wa kesi hiyo kukamilika.

Mbali na Mary, ambaye ni mwanafunzi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), washtakiwa wengine katika kesi hiyo ni Ryner Mkwawili (22) wa Chuo Kikuu Ardhi Dar es Salaam na Asha Juma (22) wa Chuo cha Uhasibu, Dar es Salaam (TIA).

Kwa pamoja washtakiwa wanadaiwa Machi 14, 2025, eneo la Sinza wilayani Ubungo, Dar es Salaam walikula njama kwa nia ya kutenda kosa la kuchapisha taarifa za uongo.

Vilevile wanadaiwa siku na eneo hilo, Mary na Asha, walisambaza taarifa za uongo katika mtandao wa WhatsApp yenye maneno kuwa:  “Toa sauti umefanya mapenzi na mpenzi wangu Mwijaku lini na wapi.”

Akiwasomea maelezo hayo, wakili Protas alidai Mary na Magnificant walikuwa marafiki wakiishi pamoja eneo la Sinza.

“Hata hivyo, baadaye hawakuelewana ndipo Magnificant aliamua kuhama kwa Mary na kwenda kuishi sehemu nyingine,” amedai wakili.

Baada ya kuhama, Machi 14, 2025 inadaiwa Mary alimpigia simu Magnificant akimtaka aende kuchukua vitu vyake alivyobakisha.

Inadaiwa alikwenda akamkuta Mary akiwa na Asha na baada ya kuingia ndani, Mary alifunga mlango akamfunga kamba na kuanza kumpiga akimtuhumu kuwa mwizi, amemuibia mpenzi wake Mwijaku.

“Toa sauti umefanya mapenzi na mpenzi wangu Mwijaku lini? Na umefanya naye wapi?” amedai wakili Protas aliposoma maelezo ya Mary.

Inadaiwa wakati Mary akiendelea kumpiga mlalamikaji kwa kutumia chuma cha ufagio, Ryner aliungana naye kumpiga, huku Asha akifurahia kipigo hicho.

Mary anadaiwa alichomeka pasi kwenye soketi ya umeme ndani ya chumba hicho, huku Ryner na Asha wakimmwagia maji mlalamikaji, baadaye kumkata nywele kwa kutumia kisu na kisha kumpaka dawa ya kunyolea nywele kichwani.

Inadaiwa Mary alichukua simu ya mlalamikaji na laini zake mbili akazivunja.

“Vilevile, mshtakiwa alichukua mkoba wa Magnificant ambao ndani kulikuwa na chupa ya manukato, mafuta ya kupaka na nguo alizovaa, vitu hivyo alivichoma moto huku wenzake wakirekodi tukio hilo,” alidai.

Wakili Protas amedai baada ya kumaliza kurekodi, Ryner na Asha waliondoka eneo hilo na kumuacha mlalamikaji akiwa na Mary, huku wakimuonya endapo atasema walichomfanyia, basi picha zake watazisambaza kwenye makundi ya chuoni ya WhatsApp ili wanafunzi wenzake waone.

Machi 15, 2025 mlalamikaji alikwenda kituo cha Polisi ambako alipewa fomu ya Polisi namba tatu (PF3).

“Mshtakiwa baada ya kupata fomu hiyo alikwenda Hospitali ya Rufaa Mwananyamala kwa ajili ya kupatiwa matibabu baada ya kuvimba kichwani na kupata michubuko na majeraha sehemu mbalimbali za mwili yaliyotokana na shambulio la kudhuru mwili,” amedai.

Wakili Protas amedai video zilizorekodiwa na Ryner na Asha zilichapishwa kwenye mtandao wa kijamii wa Instagram na akaunti maarufu ya Instagram ya Mange Kimambi ambayo ina watazamaji zaidi ya milioni moja.

Amedai wakati wa uchunguzi wa kesi hiyo, simu tatu aina ya Iphone ambazo zilikuwa zinatumiwa na washtakiwa zilichukuliwa kwa ajili ya kusaidia uchunguzi.

“Wakati wa uchunguzi washtakiwa wote watatu walikiri kutenda makosa hayo, pia eneo alilokuwa anaishi Mary kulifanyika uchunguzi na kuchukuliwa baadhi ya vitu kwa ajili ya kukamilisha uchunguzi,” amedai.

Amedai baada ya uchunguzi wa awali kukamilika, Mei 30, 2025 washtakiwa walifikishwa mahakamani na kusomewa kesi ya jinai namba 13199/ 2025.

Washtakiwa baada ya kusomewa mashtaka walikubali wasifu wao na siku walipofikishwa mahakamani, huku wakikana mashtaka yanayowakabili.

Marekebisho hati ya mashtaka

Awali, kabla ya kuwasomea maelezo, upande wa mashtaka uliwasilisha ombi la kufanya marekebisho katika hati ya mashtaka. Ombi hilo liliwasilishwa chini ya kifungu 251(1) cha Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai.

Marekebisho hayo yanahusu tarehe wanayodaiwa kutenda makosa washtakiwa hao, ambapo awali ilisomeka Machi 16, 2025 na sasa kwa mujibu wa hati mpya, washtakiwa wanadaiwa kutenda makosa Machi 14, 2025 eneo la Sinza, wilayani Ubungo.

Upande wa mashtaka umedai utapeleka mashahidi kadri kesi hiyo itakapokuwa inaendelea na usikilizwaji.

Hakimu Mwankuga baada ya kusikiliza hoja hizo, ameahirisha kesi hadi Agosti 18, 2025 kwa ajili ya kuanza usikilizwaji. Washtakiwa wapo nje kwa dhamana baada ya kutimiza masharti.