TIMU za Madagascar na Mauritania zilitoka sare ya bila kufungana (0-0) katika mechi ya Kundi B ya Michuano ya CHAN PAMOJA 2024 iliyopigwa Jumapili usiku kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa.
Kundi hili lenye timu tano linaongozwa na wenyeji Tanzania wenye pointi tatu baada ya kuichapa Burkina Faso kwenye mchezo wa ufunguzi wa michuano hiyo ambayo kwa mara ya kwanza inafanyika ukanda huu wa Afrika Mashariki.
Madagascar ilionekana kuanza kwa kasi, ikiongozwa na kocha Romuald Rakotondrabe na nahodha wao mkongwe, Andriamirado “Dax” Andrianarimanana.
Hata hivyo, Dax alilazimika kuondoka uwanjani dakika ya 39 baada ya kuonyeshwa kadi ya pili ya njano, jambo lililoacha timu yake ikicheza ikiwa na wachezaji 10 kwa zaidi ya dakika 50.
Pamoja na kuwa pungufu, Madagascar iliendelea kuwa thabiti kiuchezaji. Kipa wao, Michel Ramandimbisoa, aling’ara kwa kuokoa mipira muhimu ikiwemo shuti la mapema kutoka kwa Mohamed Hawbott na jaribio jingine la hatari dakika za mwisho kutoka kwa Moulaye Al Khalil.
Kwa upande wa Mauritania, hii ikiwa ni mara yao ya nne kushiriki CHAN, walitawala umiliki wa mpira hasa baada ya Madagascar kuwa pungufu, lakini walishindwa kuvunja ukuta wa wapinzani wao.
Kocha Aritz López Garai alikuwa na matumaini ya kuanza mashindano kwa kishindo, lakini timu yake ilionekana kukosa makali ya mwisho licha ya kuwa bora eneo la kiungo.
Kwa Madagascar, iliomaliza nusu fainali ya CHAN 2022 na kushinda medali ya shaba, pointi moja inaweza kuwa ya matumaini ikizingatiwa ilikuwa na mchezaji pungufu.