Majaliwa: Rushwa bado tishio nchi za SADC

Arusha. Licha ya maendeleo katika nchi za Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC), rushwa inatajwa kuwa tishio la usalama linalosababisha uhalifu uliopangwa, biashara haramu ya binadamu, ugaidi na mmomonyoko wa utawala wa sheria.

Hayo yamesemwa leo Jumatatu Agosti 4, 2025 na Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa wakati akizungumza kwa niaba ya Rais Samia Suluhu Hassan, katika warsha ya Wakuu wa Taasisi za Kuzuia na Kupambana na Rushwa kutoka nchi za SADC, unaofanyika jijini Arusha.

Amesema licha ya maendeleo katika nchi hizo bado rushwa inasalia kama tishio linalodhoofisha amani, taasisi na kuzuia maendeleo shirikishi katika nchi hizo, hivyo wanahitaji kuimarisha ushirikiano na wadau ikiwamo mashirika ya kiraia.


Amesema kutokana na ufisadi kuendelea kudhoofisha maendeleo, kuchochea ukosefu wa usawa, kuondoa imani ya umma kwa taasisi, viongozi hao wana wajibu wa kuhakikisha juhudi za kupambana na ufisadi zinakuzwa kupitia utashi wa kisiasa, rasilimali na ushirikiao imara.

“Tunahitaji kujenga ushirikiano na wadau, lazima tutoke kwenye sera hadi utekelezaji kwa kuhakikisha tuliyokubaliana yanaonekana na tuimarishe ushirikiano wa kuvuka mpaka hasa katika suala la uchunguzi wa pamoja na kurejesha mali pamoja kutoka hapa,” amesema.

Waziri Mkuu huyo amesema warsha hiyo ya kikanda inatoa jukwaa la kipekee na kwa wakati kwa nchi wanachama wa SADC kutafakari, kubadilishana uzoefu na kupanga njia ya kimkakati katika juhudi za pamoja za kupambana na rushwa.

Amesema tangu kuanza kutumika kwa itifaki ya SADC dhidi ya mapambano ya rushwa mwaka 2005, imelenga kuzuia na kupambana na rushwa katika sekta ya umma na binafsi, huku ikikuza utamaduni wa uwazi, uwajibikaji na uadilifu katika usimamizi wa masuala ya umma.


“Ufisadi unaendelea kudhoofisha maendeleo, kuchochea ukosefu wa usawa, na kuondoa imani ya umma kwa taasisi,” amesema.

Kuhusu Tanzania, amesema vita dhidi ya rushwa ni kipaumbele cha Taifa kutokana na umuhimu kwa maendeleo ya Taifa, usalama na kurejesha imani ya umma kwa taasisi.

Ametaja mikakati hiyo ni kuimarisha mifumo ya kisheria na kitaasisi,kupanua elimu ya umma na ushirikishwaji wa kiraia kwa sababu wanaamini raia aliye na ufahamu atakuwa hodari katika vita dhidi ya rushwa.

 “Katika miongo miwili iliyopita, tumeona pia maendeleo makubwa katika kuoanisha sheria za kitaifa na masharti ya Itifaki,nchi nyingi wanachama wa SADC, zimeimarisha sheria za kupambana na rushwa, zimewezesha taasisi za usimamizi,”amesema.


Amesema katika kipindi hicho nchi hizo zimeboresha ushirikiano wa kikanda na usaidizi wa kisheria wa pande zote, hasa katika kushughulikia rushwa ya mipakani na kuwezesha uchunguzi wa pamoja,mifumo ya sheria na sera iliyowianishwa, ambayo inaweka msingi wa majibu ya kikanda yenye umoja.

Katibu Mtendaji wa Sekretarieti ya SADC, Elias Magosi amesema warsha hiyo itawawezesha kujadiliana ushirikiano endelevu wa mtangamano wa kiuchumi, amani, usalama na utawala bora katika ukanda huo.

“Rushwa bado ni tishio kubwa kwa maendeleo ya kiuchumi na kijamii ya eneo hili kwani inamomonyoa uwazi,uwajibikaji na utawala wa sheria ambayo ni misingi ya utawala bora katika nchi za ukanda wa SADC,” amesema.

“Mapambano dhidi ya rushwa sio tu ya lazima ya utawala, wala sio tu suala la kijamii bali ni sharti la amani, usalama na maendeleo kwani rushwa inadhoofisha taasisi na kukwamisha utoaji wa huduma kwa usawa,” amesema.

Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), Crispin Chalamila amesema warsha hiyo inakwenda sambamba na maadhimisho ya miaka 20 ya utekelezaji wa itifaki ya SADC ya mapambano dhidi ya rushwa.

Amesema Kamati ya Kupambana na Rushwa ya SADC (SACC) ilianzishwa chini ya Ibara ya 11 ya Itifaki ya SADC dhidi ya rushwa,yenye jukumu la  kuandaa mikakati ya kupambana na rushwa ndani ya ukanda huo.

Amesema majukumu mengine ni kukuza na kuimarisha mifumo ya kuzuia, kugundua, kuadhibu na kutokomeza rushwa katika sekta ya umma na ya kibinafsi, pamoja na kukuza ushirikiano kati ya nchi wanachama.

Mkurugenzi huyo amesema katika wasrha hiyo ya wadau hao watajadiliana masuala kadhaa ikiwamo kuangalia hali ya rushwa na juhudi za kukabiliana nayo,mapitio ya utekelezaji wa itifaki ya SADC na kuandaa mapendekezo yanayoweza kutekelezeka kuhusu vipaumbele vya kimkakati.

Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Dk Stergomena Tax, amesema warsha hiyo ni muhimu kwa kuwa itasaidia kukabiliana na changamoto zinazosababishwa na rushwa inayoendelea kutishia mafanikio na amani katika ukanda huo.

Amesema Tanzania inaendelea kuwa imara katika kukuza utawala bora na utawala wa sheria kama nguzo muhimu katika mapambano dhidi ya rushwa.