Siha. Naibu Waziri wa afya, Dk Godwin Mollel amedai kutekwa na kupigwa kwa mke wake pamoja na msaidizi wake wakati wakitokea kumuona mgonjwa, huku akimtupia lawama mmoja wa wagombea wenzake kuhusika na tukio hilo.
Akizungumza na waandishi wa habari Agosti 3, 2025 mgombea huyo wa ubunge, Jimbo la Siha, mkoani Kilimanjaro amesema vijana hao walizingira gari la mke wake usiku wa kuamkia Agosti 3 na kuanza kuwashambulia na kupasua vioo vya gari.
Mbali na kupigwa kwa mke wake, Dk Mollel amedai uwepo wa gari kuchomwa moto na kutokuweka bayana gari hilo ni mali ya nani.
Alipotafutwa Mkuu wa Wilaya hiyo, ambaye ni Mwenyekiti wa kamati ya usalama, Dk Christopher Timbuka amesema jambo hilo lipo polisi na linachunguzwa.
“Haya masuala yapo polisi, na huwezi kusema gari limechomwa moto kwa sababu gari lilipata ajali. Gari liligonga kwenye kingo za calvati baadaye likaachwa pembeni na waliokuwepo walisema gari lilianza kupiga alamu lenyewe, na baadaye watu wakaona gari linawaka moto, kuthibitisha hilo ni mpaka wenzetu wafanye uchunguzi wa kipolisi,”amesema DC Timbuka
Endelea kufuatilia Mwananchi