Matumaini mapya wakazi wa Magomeni Kota

Dar es Salaam. Baada ya malalamiko ya kukithiri kwa uharibifu, uchakavu na wizi wa miundombinu katika nyumba za Magomeni Kota, Wakala wa Majengo Tanzania (TBA) umesema Sh1 bilioni zimetengwa kukarabati na kurejeleza vitu vilivyoibiwa.

Hata hivyo, wakala huo umesema ukarabati wa uchakavu na uharibifu na urejeshaji wa vilivyoibiwa, hautahusisha maeneo ya ndani ya kila nyumba ya mkazi, ukisisitiza mkazi husika ndiye mwenye wajibu huo.

Kauli hiyo ya TBA, imekuja siku kadhaa tangu Mwananchi iliporipoti kuhusu hali ya uharibifu, wizi wa miundombinu yakiwemo mabomba ya maji, waya za radi na uhaba wa maji uliokithiri katika nyumba hizo.

Uzuri wa majengo ya Magomeni Kota umebaki kwa kuyaangalia kwa mbali, tena ukiwa unapita, si kwa kuyasogelea karibu kutokana na uchakavu wake.

Katika habari hiyo ya kiuchunguzi, ilielezwa uhaba wa maji na uharibifu wa mazingira katika nyumba hizo, unasababishwa na baadhi ya wakazi wake kushindwa au kukaidi kulipa Sh30,000 za huduma jumuishi.

Kwa sababu ya uhaba wa maji, taarifa hiyo iliyoripotiwa na Mwananchi ilieleza, umesababisha wakazi watumie lifti zilizopo kupandishia maji kwenda hadi maghorofa ya juu (namba saba na nane) yanayochotwa kwenye mabomba na visima vilivyopo chini.

Nyumba hizo zilizopo chini ya TBA, zilikabidhiwa kwa wananchi hao Machi 23, 2022 na Rais Samia Suluhu Hassan, aliyeelekeza majengo kutunzwa, usafi kuzingatiwa na michango ya huduma jumuishi itolewe kwa faida ya kila mmoja.

Katika hotuba yake ya uzinduzi, Rais Samia alisema amezungukia katika nyumba hizo, ni nzuri, zimejengwa kisasa na zitakidhi mahitaji ya watakaishi hapo.

“Langu kwenu ni utunzaji wa nyumba hizi, maana tumefanya mnachohitaji. Kwa sababu nyumba hizi wanakaa watu wengi, usafi hasa maeneo ya korido na ngazi, unaweza kuwa changamoto,” alisema Rais Samia.

Akizungumza na Mwananchi, Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Miliki kutoka TBA, Ofisi za Makao Madogo, Dar es Salaam, Susan Ulula amekiri kuwepo kwa hali hiyo na kwamba wameshafanya ukaguzi na tathmini ya uharibifu uliojitokeza.

Tathmini hiyo, amesema imesababisha zitengwe Sh1 bilioni katika mwaka wa fedha 2025/26 kwa ajili ya kurejesha vitu vilivyoibiwa na kukarabati uharibifu wote hasa maeneo ya nje ya nyumba hizo.

“Tunakiri kutokea kwa wizi wa vifaa vya mabomba katika rooftop na nyaya za kinga ya radi katika majengo ya mradi wa Magomeni Kota. Katika mwaka wa fedha 2025/26 TBA imetenga Sh1 bilioni, kwa ajili ya ukarabati na sehemu ya fedha hiyo itatumika kurudishia vifaa vilivyoibiwa,” amesema.

Sambamba na hilo, amesema katika makabidhiano ya majukumu na kamati ya wanakota ilisisitizwa kuimarisha ulinzi wa eneo husika kwa kushirikiana na viongozi wa kila jengo kwa kuwatambua wageni wote wanaoingia na kutoka kwenye majengo.

Kuhusu uchakavu unaoshuhudiwa, Susan amesema unasababishwa na matumizi mabaya ya wakazi wenyewe, hivyo ukarabati utakaofanywa na TBA hautahusisha ndani ya vyumba.

“TBA imeandaa mpango wa ukarabati mkubwa na kutenga fedha kwenye bajeti ya mwaka 2025/26. Ingawa ukarabati huu hautajumuisha maeneo ya ndani ya kila nyumba ya mkazi, maeneo ya ndani ya nyumba yatafanywa na wakazi wenyewe,” amesema.

Kuhusu uhaba na upungufu wa maji, amesema hali hiyo imefanya wakazi kutafuta huduma hiyo katika vyanzo tofauti na kutumia lifti kuyapandisha katika sakafu za juu.

“Lifti zinaweza kuharibika, usambazaji wa maji safi kwenye eneo la mradi, awali ulitumia mfumo wa mita moja ambayo ilitumika kusambaza maji kwenye majengo yote. Lakini wakazi waliitaarifu Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira (Dawasa) kusitisha huduma ya maji, hadi pale Serikali itakapoweka mita za maji kwa kila mkazi,” amesema Susan.

Amesema hatua madhubuti zimechukuliwa na TBA kwa kutenga fedha katika bajeti ya mwaka wa fedha 2025/2026 kwa ajili ya kutenganisha mita za maji kwa kila mkazi.

Kuhusu kuharibika kwa bustani, amekiri na kufafanua: “Kabla ya uharibifu huo, huduma za bustani na usafi zilikuwa zikitekelezwa kupitia fedha zinazokusanywa kupitia mfumo wa huduma jumuishi na umoja wa wakazi.”

Kwa sababu wakazi wengi wanashindwa kuchangia gharama hizo, amesema huduma muhimu kama maji ya kumwagilia na watumishi wa usafi zilikwama.

“Hali hiyo ilisababisha uharibifu wa bustani na mandhari ya nje ya majengo. Kwa sasa, uboreshaji wa bustani na mazingira unategemea ushiriki wa moja kwa moja wa wakazi kwa kuwa suala hili ni sehemu ya majukumu yao katika kulinda na kutunza mazingira ya kuishi,” amesema.

Mwenyekiti wa Wakazi wa Magomeni Kota, George Abel amepokea ahadi ya fedha za ukarabati kwa matumaini, akisisitiza utekelezaji wake ufanyike haraka hasa huduma ya maji, kwani wameahidiwa mara nyingi.

“Serikali baada ya kutoa majibu hayo kwanza tunashukuru, lakini ombi letu utekelezaji ufanyike kwa haraka kwa sababu changamoto zimekuwa nyingi.

“Kuna viongozi wengi wamekuja hapa na kusema watatua ikiwemo shida ya maji, lakini hakuna kinachoendelea,” amesema George.

Amesema ukarabati huo utakaofanyika, uhusishe na marekebisho ya mfumo wa majitaka yaliyotuwama katika block namba moja, mbili, na tatu.

“Tulishaandika barua kwenda TBA muda mrefu kuelezea changamoto hii kwa kina na adha tunayopitia, kwa kuwa fedha zimeshatengwa ni matumaini yangu ukarabati huo utazingatia na eneo hilo,” amesema.

Kiu ya utekelezaji wa haraka wa ahadi hizo, imeonyeshwa pia na Subrina Siliwa katika nyumba hizo, aliyesema pamoja na majibu mazuri ya Serikali, imani yake itatokana na kuona utekelezaji ukianza.

“Unajua tumekuwa wepesi wa kupewa ahadi, lakini utekelezaji ni shida, wanakuja na kusema mengi ili watu tufurahi kwa muda, lakini tabu na shida zote wanatuachia,” amesema.