Mchakato wataka Urais CUF moto

Dar es Salaam. Kamati ya Uongozi ya Chama cha Wananchi (CUF) imekamilisha mchakato wa kuwahoji watiania wa urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, huku baadhi ya waliopitia mchujo huo wakieleza kuwa maswali walioulizwa yalikuwa magumu na yenye mitego.

Miongoni mwa waliotia nia ya kuwania nafasi ya urais, Kiwale Mkungutila, mmoja kati ya watiania watano waliohojiwa leo, Jumatatu, Agosti 4, 2025, amesema licha ya ugumu wa maswali, anaamini anastahili kupewa nafasi ya kupeperusha bendera ya CUF katika Uchaguzi Mkuu utakaofanyika Oktoba 29, 2025.

Mkungutila amesema baadhi ya washindani wake hawana uelewa wa kina wa itikadi ya chama kutokana na kuhama-hama vyama mara kwa mara.

Kwa upande wa Tanzania Bara, watiania waliohojiwa ni Rose Kuhoji, Gombo Gombo na Kiwale Mkungutila, huku kwa upande wa Zanzibar wakihojiwa Masoud Hamad Msaoud na Mohamed Khatibu.

Mtiania wa urais wa Tanzania kwa tiketi ya CUF, Rose Kahoji akishuka kwenye gari baada ya kuwasili makao makuu ya chama hicho, yaliopo Buguruni Jijini Dar es Salaam.



Mtiania mwingine, Mohamed Mnyaa, hakuhudhuria mahojiano hayo, lakini uongozi wa chama umethibitisha kuwa alitoa taarifa rasmi ya udhuru.

Kamati ya Uongozi iliyoendesha mchakato huo iliongozwa na Mwenyekiti wa CUF, Profesa Ibrahim Lipumba, ikishirikiana na Katibu Mkuu, Husna Abdallah pamoja na viongozi wengine waandamizi wa chama hicho.

Lengo la mahojiano hayo lilikuwa ni kuwapima watiania hao kabla ya majina yao kuwasilishwa katika Baraza Kuu la Uongozi linalotarajiwa kuketi Agosti 6 hadi 7, 2025.

Baada ya mahojiano hayo, kamati hiyo ilijifungia kwa takribani saa moja ili kuchambua taarifa na majibu ya kila mtiania kwa ajili ya kufanya tathmini ya mwisho.

Matokeo ya tathmini hiyo yatapelekwa mbele ya Baraza Kuu ambalo litakuwa na jukumu la kupendekeza jina moja kwa kila nafasi ya urais.

Akizungumza na Mwananchi, Mkungutila amesema: “Maswali yalikuwa magumu na ya mtego, lakini naamini ninastahili kuwa mgombea wa CUF. Wapinzani wangu hawana ufahamu wa kutosha kuhusu itikadi ya chama; wamekuwa wakihama vyama mara kwa mara, hivyo si wa kuaminika kupewa dhamana kubwa kama hii.”

Ameongeza kuwa amekuwa mwanachama mwaminifu wa CUF tangu mwaka 2000 na alishawahi kutunukiwa tuzo na Chuo cha Kampala, Uganda, kutokana na mchango wake katika sekta ya kilimo. Amesisitiza kuwa uzoefu wake wa ndani ya chama unamfanya kuwa chaguo bora zaidi.

“Wanachama wanaohama vyama wanatafuta madaraka tu, na wakikosa huondoka. Si watu wa kupewa nafasi nyeti kama urais,” amesema Mkungutila. Ameongeza kuwa anataka kuwatumikia Watanzania kwa sababu anazijua changamoto zao, zikiwemo ajira na rushwa.

Mtiania wa urais wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kwa tiketi ya CUF, Masoud Hamad Msaoud akiwasili makao makuu ya chama hicho, yaliopo Buguruni Jijini Dar es Salaam.



“Nimejipanga kuhakikisha chama hakifanyi makosa. Mimi ni kada mtiifu, nina elimu nzuri na uzoefu mkubwa. Watanzania wanahitaji kiongozi wa kweli, si wa kupiga porojo. Naahidi kupambana na rushwa na nitakapopewa nafasi, nitakuwa mtumishi wa wananchi, si mtawala,” amesisitiza.

Kwa upande wake, Mohamed Khatibu amesema mchakato huo ulienda vizuri na maswali yalikuwa na uzito wake, jambo alilosema ni la kawaida kwenye mahojiano ya aina hiyo. Ameongeza kuwa sasa wanasubiri uamuzi wa chama.

“Nimehojiwa kama ilivyopangwa, na kwa sasa uamuzi upo kwa chama. Tuna matumaini kuwa kila kitu kitaenda sawa,” amesema Khatibu.

Katibu Mkuu wa CUF, Husna Abdallah, amesema baada ya mahojiano hayo, kamati ilijifungia kuchambua taarifa zote na kufanya tathmini ya kila mtiania kwa lengo la kulisaidia Baraza Kuu kufanya uamuzi sahihi.

“Ni mchakato mzito, lakini tunashukuru tumefikia hatua hii. Tumewahoji kila mmoja na pia tuliwaandaa kisaikolojia. Wajumbe wa Baraza Kuu wana mamlaka ya mwisho. Yeyote atakayechaguliwa ni muhimu apate uungwaji mkono wa wenzake,” amesema Husna.

Naye Mkurugenzi wa Mawasiliano wa CUF, Mohammed Ngulangwa, amesema mchakato huo wa mahojiano ulikuwa na lengo la kuwafahamu watiania kwa undani zaidi kabla ya kuwasilisha majina yao mbele ya Baraza Kuu, Agosti 6 na 7, 2025.

“Kamati ya Maadili ya chama nayo itaketi kesho kupitia majina hayo na kuyapima upya kulingana na majibu waliyotoa wakati wa mahojiano,” amesema Ngulangwa.

Amebainisha kuwa mkutano wa Baraza Kuu utakuwa na jukumu la kuchuja majina ya wagombea wa udiwani na ubunge kutoka maeneo mbalimbali nchini, sambamba na kupanga majina ya watiania wa urais wa Tanzania na Zanzibar wasiopungua mmoja na wasiozidi watatu kwa kila upande.

“Baada ya hatua hiyo, majina hayo yatapelekwa kwenye Mkutano Mkuu wa CUF utakaofanyika Agosti 9, 2025. Wajumbe watachagua mgombea rasmi wa urais wa Tanzania na wa Zanzibar kwa tiketi ya CUF,” amesema Ngulangwa.