Mfanyabiashara Iringa adaiwa kupotea, mke asimulia

‎Iringa. Mfanyabiashara eneo la Mashine Tatu mkoani Iringa, John Changawa, ameripotiwa kutoweka katika mazingira ya kutatanisha tangu Julai 30, 2025.

‎‎Habari za awali zinadai kuwa, John alionekana mara ya mwisho akizungumza na watu waliokuwa ndani ya gari kabla ya kuwaaga jamaa zake waliokuwa jirani na ofisi yake kwamba, anatoka na atarejea muda mfupi ujao.

Akizungumzia kuhusu tukio hilo, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Iringa, Meloe Buzema ameahidi kufuatilia endapo zimekwishatolewa taarifa kwenye kituo cha polisi.

Mke wa John Changawa, Judith Luwago mkazi wa Kijiweni halmashauri ya Manispaa ya Iringa mkoani Iringa akizungumza na mwandishi wa habari leo Jumatatu Agosti 4, 2025. Picha na Christina Thobias.



‎Hata hivyo, mke wa John, Judith Luwago amesema alianza kuhisi kuna tatizo baada ya mumewe kutopokea simu kila alipojaribu kumtafuta.

‎“Tulikuwa tunawasiliana mara kwa mara, lakini ghafla simu ikawa haipokewi wala ujumbe mfupi haujibiwi, jambo ambalo sio kawaida yake,” amedai Judith.

“Baadaye simu yake ilipokewa na mtu aliyekuwa ofisini kwa John na akaniambia niende japo hafahamu mahali mume wangu alipokwenda.”

Bibi wa John Changawa, Anisea Mgaya mkazi wa mtaa wa mshindo halmashauri ya Manispaa ya Iringa akizungumza na mwandishi wa habari leo Jumatatu Agosti 4, 2025. Picha na Christina Thobias.



‎‎Kwa upande wake, shangazi wa mfanyabiashara huyo, Agnes Changawa, amesema familia itandelea kufuatilia suala hilo kwa ukaribu na kwamba, leo Jumatatu, Agosti 4, 2025 watakwenda Kituo Kikuu cha Polisi Iringa kwa hatua zaidi.

‎ Agnes amesema tukio la kutoweka kwa John limetolewa taarifa polisi na kupewa namba IRR/RB/2881/2025 huku wakiomba mwenye taarifa ama atayemuona kuwajulisha kupitia namba 0753706081 na 0678349113.

Endelea kufuatilia Mwananchi.