Mfumo mpya kutoa taarifa za waharibifu, wezi mali za Tanesco

Dar es Salaam. Kutokana na uwepo kwa wizi wa mali na uharibifu wa miundombinu ya Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco), shirika hilo limeanzisha mfumo wa kupokea taarifa za siri (Whistle blower portal) ili kuwabaini wale wote wanaohusika na uhalifu huo.

Mfumo huo umeanzishwa ili kurahisisha upokeaji wa taarifa kutoka kwa wananchi, wafanyakazi wa Tanesco na wadau wengine kuhusu vitendo vya wizi wa mali za shirika, rushwa, hujuma za uharibifu wa miundombinu ya umeme, pamoja na vitendo vya unyanyasaji visivyofaa katika mazingira ya kazi.

Hata hivyo kwa mujibu wa shirika hilo, kiwango cha uharibifu wa mali na wizi ikiwemo transfoma, nyaya na mafuta kwa sasa kimepungua kutokana na juhudi zinazofanyika kupambana na hali hiyo.

Wakati wa uzinduzi wa mfumo huo katika Ofisi za Tanesco uliofanywa na Kaimu Mkurugenzi wa Mawasiliano na Huduma kwa Wateja wa shirika hilo, Irene Gowele, amesisitiza kuwa kutakuwa na usiri mkubwa wa kulinda watoa taarifa.

“Kwa kipindi kirefu Tanesco imekuwa ikipata changamoto mbalimbali zinazokwamisha wakati mwingine utoaji wa huduma endelevu ya umeme, kama vile wizi na uharibifu dhidi ya miundombinu ya umeme.”

“Vitendo vya rushwa kutoka kwa baadhi ya watumishi wasio waaminifu pamoja na upotevu wa mapato unaotokana na uharibifu wa miundombinu ya umeme unaoweza kuzuilika mapema,”amesema.

Amesema, ujio wa mfumo huu mpya ni hatua muhimu ya kimageuzi katika utendaji kazi wa shirika na una lenga kuimarisha uwajibikaji, kudhibiti uhalifu, kulinda watoa taarifa dhidi ya vitisho па kuongeza uaminifu wa umma kwa Tanesco.

Gowere amesema mfumo huo unaanza leo Agosti 4, 2025 kwa maana ya kurahisisha utoaji wa taarifa hizo kutoka kwa umma katika maeneo mbalimbali nchini.

“Mfumo huu utasaidia upatikanaji wa taarifa za kuweza kudhibiti na kupunguza uhalifu ambao umekuwepo kwenye mali na miundombinu ya shirika,” amesema Gowele na kuongeza…

Amesema mfumo utatoa taarifa za uhujumu/uharibifu wa miundombinu, wizi wa mali za Shirika, kupata taarifa za vitendo vya rushwa kwa baadhi ya watumishi wasio waaminifu kwa shirika pamoja na taarifa za unyanyasaji wa kijinsia katika maeneo ya kikazi.

“Kwa sasa kiwango cha uharibifu kimepungua hatujarekodi matukio hayo kwa siku hizi za karibuni. Kiwango kinapungua na tunaamini uzinduzi wa mfumo huu utakwenda kumaliza vitendo hivi kabisa,” amesema.

Gowele amesema wakati mwingine wananchi wamekuwa wakiogopa kutoa taarifa kwa kuhofia usalama wao, hivyo mfumo huo ni mwarobaini.

Pia, amesema wanaendelea kushirikiana na vyombo vingine vya ulinzi na usalama kwa ajili ya kushughulikia changamoto hiyo.

Akitaja njia zitakazotumika kuwasilisha taarifa hizo ni pamoja na kupitia tovuti ya Tanesco, www.tanesco.co.tz kwa kubonyeza kiungo cha Whistleblower Portal na utaweza kujaza fomu.

Pia, kupitia kupiga simu ya bila malipo ya namba 180, Shirika linauhakikishia umma kuwa taarifa zote zitakazopokelewa zitatunzwa kwa usiri mkubwa na kushughulikiwa.

Akizungumza na Mwananchi kuhusiana na hatua hiyo, Kamishna Msaidizi Mwandamizi mstaafu wa Jeshi la Polisi, Alhaj Jamal Rwambow amesema kama taarifa za siri zitawafikia watu kwa siri na zitafanyiwa kazi ufumbuzi utapatikana. Akatoa angalizo la kuwapo kwa motisha kwa watoa taarifa hizo.

“Watoe motisha ya kiasi cha fedha, kama nilivyofanya kipindi cha kumaliza matukio ya mauaji ya watu wenye ulemavu,” amesisitiza.