:::::::
Mkutano wa 45 wa Wakuu wa Nchi Wanachama wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) umeanza Agosti 04, 2025 jijini Antananarivo, Madagascar na Kikao cha Wataalamu cha Maafisa Waandamizi cha kupitia Utekelezaji wa Mpango Mkakati Elekezi wa Maendeleo wa Kikanda 2030 (Regional Indicative Strategic Development Plan 2030-RISDP).
Tanzania inashiriki kikao hicho muhimu kwa maendeleo ya kikanda, huku ujumbe wake katika kikao hicho, ukiongozwa na Mkurugenzi wa Kikanda katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Bi. Talha Waziri.
Akifungua kikao hicho, Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Biashara za Kimataifa wa Zimbabwe, Balozi Albert Chimbindi alisema lengo la kikao hicho ni kufanya tathimini ya utekelezaji wa mpango wa RISDP ili kujua hatua iliyofikiwa na kubaini vikwazo vinavyokwamisha utekelezaji wake na kuvitafutia ufumbuzi wa pamoja.
Alisema licha ya taarifa mbalimbali kuonesha kuwa mpango huo unapata mafanikio, lakini bado jitihada za pamoja baina ya nchi wanachama zinahitajika ili kuharakisha utekelezaji wa mpango huo ambao umebakisha miaka michache ili ukamilike.
“Tunahitaji nchi wanachama wa SADC ziongeze jitihada za pamoja kuongeza kasi ya utekelezaji wa miradi ya miundombinu na kufanya biashara baina yao ambayo hadi sasa, licha ya takwimu kuonesha imeongezeka lakini sio katika kiwango kinachoridhisha”, Balozi Chimbindi alisema.
Naye, Naibu Katibu Mtendaji wa SADC anayeshughulikia Ushirikiano wa Kikanda, Bi. Angeles N’Tumba alisisitiza umuhimu wa nchi wanachama kubuni njia endelevu za kutafuta fedha kwa ajili ya kugharamia utekelezaji wa mpango huo. Alisema kuna haja ya kujifunza namna Jumuiya nyingine za Kikanda zinavyopata fedha za kutekeleza mipango yao ya maendeleo, na kutolea mfano wa ECOWAS kuwa ina mpango mzuri na endelevu wa kutafuta rasilimali za kuendeleza miradi yao.
Mkutano huo utahitimishwa kwa Mkutano wa Wakuu wa Nchi wa SADC utakaoanza Agosti 17, 2025 ambapo Tanzania itashiriki kikamilifu katika ngazi zote za mikutano hiyo.