Museveni aahidi mabilioni kwa nyota wa Uganda CHAN

Wakati timu ya taifa ya Uganda ‘The Cranes’ ikianza kupeperusha bendera ya taifa hilo kwenye Fainali za Chan 2024 dhidi ya Algeria, Rais wa nchi hiyo, Yoweri Museveni ametoa ahadi nono ya fedha kwa timu hiyo.

Taarifa iliyotolewa na Shirikisho la Mpira wa Miguu Uganda (Fufa) leo, imeeleza kuwa The Cranes itavuna Sh1.2 bilioni kwa fedha za Uganda (sawa na Sh850 milioni kwa fedha za Tanzania) katika kila mchezo wa CHAN ambao itaibuka na ushindi.

“Rais ametangaza bonasi kubwa ya ushindi ya Sh1.2 bilioni kwa timu kwa kila mechi kwenye Chan 2024,” amesema Rais wa Fufa, Moses Magogo.

Magogo ametoa taarifa hiyo leo Jumatatu, Agosti 4, 2025 wakati alipotembelea kambi ya timu hiyo iliyopo katika Hoteli ya Fufa.

Uganda itaanza harakati za kulisaka taji la Chan 2024 kwa kuikabili Algeria leo kwenye Uwanja wa Namboole, Kampala kuanzia saa 2:00.

Mchezo huo ni wa kundi B na utatanguliwa na ule wa kati ya Niger na Guinea utakaochezwa kuanzia saa 11:00 jioni uwanjani hapo hapo.

Hapana shaka Uganda ina hamu ya kuibuka na ushindi katika mechi hiyo ili ifuate nyayo za waandaaji wenza wa mashindano hayo mwaka huu, Tanzania na Kenya ambao wameanza kwa ushindi.

Tanzania ‘Taifa Stars’ ilifungua kwa kuibuka na ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya Burkina Faso na jana Kenya ‘Harambee Stars’ ikapata ushindi wa bao 1-0 dhidi ya DR Congo.