PZG, MCL wasaini MoU kuimarisha vipaumbele vya maendeleo ya Taifa

Dar es Salaam.Kampuni ya Mwananchi Communications Limited (MCL) na Kampuni ya mikakati, matokeo na uhusiano wa umma ya PZG, wamesaini Makubaliano ya Ushirikiano (MoU) yenye lengo la kuendeleza vipaumbele vikuu vya kitaifa vya maendeleo, kampeni, mipango ya uendelevu na ubunifu nchini Tanzania.

Makubaliano hayo yanaashiria dhamira ya pamoja ya pande zote mbili katika kuendeleza simulizi zenye mwelekeo wa kutekeleza programu za maendeleo zenye ufanisi.

Maeneo ya ushirikiano yanajumuisha ushirikiano wa kimkakati, matukio mbalimbali, tafiti za pamoja kuhusu maeneo muhimu ya sera kwa msisitizo maalumu katika kutumia fursa ya Soko Huru la Bara la Afrika (AfCTA), uwekaji wa malengo ya Maendeleo Endelevu (SDGs) katika muktadha wa ndani ya nchi na utekelezaji wa Dira ya Maendeleo ya Tanzania 2050, miongoni mwa mengine.


Ofisa Mkuu wa Madhumuni wa PZG, Prudence Zoe Glorious amethibitisha dhamira yake ya kuimarisha ushirikiano na wadau wa vyombo vya habari ili kufungua fursa zaidi za majadiliano na kusambaza ujumbe kuhusu masuala muhimu.

“MCL na PZG wanashirikiana kwa mtazamo unaotoa kipaumbele kwa athari, madhumuni na ushirikiano. Pamoja, tutajitahidi kukuza simulizi na hadithi za uendelevu, tukitumia utaalamu na rasilimali zetu kuimarisha uwezo, kuendesha mabadiliko muhimu, kukuza ubunifu na biashara ndani na nje ya Tanzania,”amesema.


Ushirikiano huo pia utahusisha kuangazia fursa ya kushirikiana na watu mashuhuri wa kimataifa ili kuandaa njia za kipekee za mawasiliano zitakazochochea majadiliano, sauti za kijamii na mwonekano zaidi kwa wanawake wa Kiafrika na majadiliano ya kizazi kwa kizazi yenye mwelekeo wa madhumuni.

Mkurugenzi Mtendaji wa MCL, Rosalynn Mndolwa-Mworia amesema kupitia ushirikiano huu wa kimkakati na PZG kama miongoni mwa mshirika muhimu kutoka sekta binafsi na wahisani wanaoshiriki maono ili kuunda simulizi zitakazochochea maendeleo na kuimarisha uwajibikaji.

“Katika Mwananchi Communications Limited, tumejikita kuleta athari chanya nchini Tanzania, Afrika na duniani kwa ujumla. Usimulizi shirikishi ndio msingi wa maendeleo endelevu kwa kuinua sauti za watu ambao mara nyingi husahaulika,” amesema Rosalynn.

Amesema ushirikiano huo wa kimkakati unatarajiwa kuleta athari kubwa katika mazingira ya maendeleo endelevu ya Tanzania kwa kutumia utaalamu na rasilimali za PZG na MCL.