Ripoti Maalumu: Nyumba yako ina mlango huu? Fahamu hatari yake

Dar es Salaam. Katika nyumba ya kawaida iliyopo pembezoni mwa mji kuna mlango mdogo ukutani ukielekea uani.

Mwenye nyumba anasema maisha hayatabiriki ni vyema kuwa na njia ya kutokea, iwapo kutaibuka majanga kama vile moto, uhalifu na mengine ya asili.

Katika maisha ya kila siku, huwaelimisha wanawe na mkewe umuhimu na matumizi ya mlango huo.

Miongoni mwa elimu anayotoa kwa familia yake ni kuwa, iwapo kuna harufu isiyo ya kawaida kama vile kuungua kwa plastiki au moshi basi watafute njia salama kuuelekea mlango huo.

Si hivyo pekee, huwafundisha iwapo kutatokea mazingira yenye kuashiria hatari mlango mkuu, wasiende eneo hilo bali wajongee kwenye ule wa dharura.

Haishii hapo, anawaeleza ikiwa kutakuwa na ishara za tetemeko basi waelekee eneo salama kisha kutoka nje kupitia mlango huo.

Wanawe na mkewe ni kama hawamuelewi, kuna wakati huweka vitu mbele ya mlango huo pasipo kutambua hakuna ajuaye lini janga linaweza kutokea.

Katika mazingira yenye migogoro, ajali na majanga ya ghafla, mlango wa dharura ni muhimu iwe kwa nyumba ndogo, kubwa au ghorofa.

Hata hivyo, ilivyo sasa nyumba nyingi zimejengwa kwa mtazamo wa kujilinda zaidi na uhalifu, ukiwamo wizi kuliko usalama wa wakazi wake wakati wa majanga.

Madirisha yamewekwa vyuma, milango huwa miwili, wa mbao na wa chuma ambayo hufungwa kwa funguo, komeo na hata makufuli.

Zipo nyumba zenye milango mikuu miwili kukuwezesha kuingia na kutoka mara nyingi huwa sebuleni na jikoni, lakini zipo zenye mmoja pekee.

Baadhi ya ghorofa zikiwamo zilizopo eneo la biashara lenye mkusanyiko wa watu wengi Kariakoo, jijini Dar es Salaam zimezungukwa na maduka zikiwa na eneo dogo la geti na korido kuelekea ziliko ngazi.

Wadau kadhaa waliozungumza na Mwananchi wanasema ujenzi haupaswi kufanyika pasipo kuwapo miundombinu ya usalama, ikiwamo milango ya dharura. Hata hivyo, la kujiuliza ni je, wangapi wanaotekeleza hili?

Said Omary, Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa wa Kariakoo Magharibi, jijini Dar es Salaam anasema ujenzi wa majengo mengi hauzingatii kanuni za usalama, ikiwamo milango ya dharura, yakiwamo yenye mlango mmoja pekee.

“Kwa sababu ya ukosefu wa milango ya dharura, nyumba nyingi zikiungua watu hushindwa kutoka haraka, wamejifungia ndani kana kwamba ni maghala hata majirani hawajui watapita wapi kwenda kuwasaidia,” anasema.

Anasema Serikali ya mtaa haina mamlaka ya moja kwa moja kuingilia masuala ya ujenzi au kutoza faini, lakini kupitia vikao vya Kamati ya Maendeleo ya Kata (WDC), wamekuwa wakitoa maoni na mapendekezo kwa mamlaka husika kuhusu ujenzi salama.

Ni mtazamo wa Siraji Shihili, mjumbe msaidizi wa Mtaa wa Mkunguni uliopo Kariakoo kwamba, ujenzi unafanyika ukilenga kudhibiti wezi.

Kwa upande wao, Hamidu Shemdoe, msimamizi wa jengo la biashara lililopo Kariakoo na Charles Maope, msimamizi na mlinzi wa ghorofa lililopo Mtaa wa Mkunguni, wanasema milango ya dharura imepewa kipaumbele katika majengo yao.

“Hii ni nyumba ya kuishi watu, kila anayekuja kupanga anauliza kuhusu usalama, hivyo kumewekwa madirisha na milango ya kutoka kwa haraka,” anasema Maope na kueleza wamekuwa wakiwaelimisha wakazi wa jengo hilo kuhusu milango hiyo ambayo haipaswi kufungwa wala kuzibwa.

Maoni ya wataalamu, mafundi

Profesa Geraldine Kikwasi kutoka Chuo Kikuu Ardhi anasema baadhi ya majengo yenye milango ya dharura imefungwa, huku mengine yakiwa hayana kabisa jambo lililo kinyume cha taratibu za ujenzi salama.

“Kuna majengo ukiyatembelea unakuta mlango mmoja tu wa kuingia na kutoka. Sehemu nyingine zote zimezibwa au zimepakiwa bidhaa. Kama moto ukitokea watu hawatakuwa na njia mbadala ya kujiokoa,” anasema.

Changamoto kubwa anasema ni baadhi ya wamiliki kupuuza maelekezo ya Jeshi la Zimamoto na Uokoaji au kupata vibali bila kukaguliwa ipasavyo.

Profesa Kikwasi anasema kila jengo linapaswa kujitegemea kwa usalama bila kutegemea lingine lililo jirani ili kutoka au kupata msaada wa dharura.

“Ukuta wa kuzuia moto kati ya jengo na jengo unatakiwa uwe thabiti na usio na sehemu ya kupitisha moto au moshi, kila jengo lazima liwe na mfumo wake wa usalama,” anasema.

Mchora ramani za majengo, Patrick Lema anasema: “Katika maeneo ambayo hayajapangwa ni watu wachache wanaojenga kwa kutumia ramani zilizopitishwa na halmashauri, wengi wamejenga tu, hivyo ikitokea hatari wanashindwa kujiokoa.”

Anasema ni muhimu kila jengo kuwa na mpango wa usalama unaojumuisha njia za mawasiliano ya dharura, chumba cha siri au eneo la kukusanyikia na milango ya dharura ya kutokea.

Hamidu Ramadhani, fundi ujenzi mkazi wa Kigamboni anasema: “Watu wengi hawatilii maanani milango ya dharura, wanapojenga wanataka nyumba ifunikwe na kuwa na milango miwili iliyozoeleka, hawafikirii kuwa kuna siku inaweza kutokea hatari. Ukiwaeleza wanaona ni kuongeza gharama za ujenzi tu.”

Said Mwalimu, fundi wa kuunga vyuma mkazi wa Tabata, anasema hajawahi kupata mteja aliyemtaka kuweka mlango wa dharura kupitia dirisha.

“Wateja wengi wakileta maua ya madirisha au milango sijawahi kuambiwa hili jambo (mlango wa dharura) nafikiri kuna haja ya elimu kutolewa,” anasema.

Mhandisi wa majengo, Sophia Nyang’oro anasema mlango wa dharura unapaswa kuwa sehemu ya kila ramani ya nyumba, sawa na jinsi madirisha yanavyopangwa.

“Tunajenga nyumba zenye vioo vikubwa na balcony (roshani) nzuri, lakini tukisahau janga linaweza kutokea saa yoyote. Moto unaweza kuzuka jikoni au hitilafu ya umeme ikatokea usiku wa manane,” anasema.

Anasema nyumba za ghorofa ziko kwenye hatari zaidi kwa sababu wakazi wa juu hupata wakati mgumu kutoka endapo ngazi kuu zitafungwa kwa moshi au moto.

Kamanda wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji, Mkoa wa Ilala, Peter Mabusi anasema jukumu la kusimamia usalama wa majengo limeainishwa katika Sheria ya Jeshi la Zimamoto na Uokoaji ya mwaka 2007, Sura ya 427.

“Mtu yeyote anayetaka kujenga, kubomoa au kukarabati jengo anapaswa kuwasilisha michoro ya ujenzi kwenye jeshi letu, hii ni kwa ajili ya kuhakikisha michoro hiyo inazingatia usalama wa majanga, ikiwamo milango ya dharura,” anasema.

Kamanda Mabusi anasema majengo yenye mikusanyiko mikubwa ya watu kama vile shule, masoko, hospitali na nyumba za ibada yanatakiwa kuwa na njia za kutokea wakati wa dharura.

“Tofauti kati ya nyumba ya familia yenye watu watano na shule yenye wanafunzi 1,000 ni kubwa, ikitokea hatari kama moto wote wanahitaji njia za kutoka ambazo zimepimwa kwa urefu, upana na aina ya milango,” anasema.

Anatoa mfano wa tukio la moto la mwaka 2015 katika nyumba iliyopo Mtaa wa Ulam, Buguruni Malapa jijini Dar es Salaam ambayo iliteketea na kusababisha watu tisa kupoteza maisha kwa kushindwa kufungua mlango, huku mageti yakiwa yamefungwa kwa kufuli.

“Hili linaweza kuwa mfano maana jamii nyingi hujifungia kwa komeo ngumu na kusahau kuweka milango ya dharura, kwani hujilinda na wezi zaidi kuliko usalama wao,” anasema.

Kuhusu michoro ya ujenzi, anasema yote inapitia hatua mbalimbali kabla ya kupitishwa, huku jeshi hilo likiwa sehemu ya mchakato huo.

“Tunashirikiana na halmashauri kupitia ofisi zao za mipango miji baada ya mtu kupeleka ramani, wataalamu wetu waliopo huko hufanya kazi ya kuipitia na kutoa maelekezo ya usalama. Tunao maofisa wetu waliopo moja kwa moja kwenye ofisi hizo,” anasema na kuongeza kuwa hatua hiyo imeondoa usumbufu kwa wananchi kuhangaika kwenda ofisi tofauti ili kupata vibali vya ujenzi.

Mkuu wa Kitengo cha Mipango Miji wa Jiji la Dar es Salaam, Maduhu Ilanga anasema ujenzi wa nyumba, hasa majengo ya makazi na biashara unatakiwa kuzingatia uwapo wa milango ya dharura kwa mujibu wa sheria.

Anasema kuna ongezeko la majengo yanayojengwa bila kufuata taratibu, huku yakikosa miundombinu muhimu ya kiusalama.

“Ili kuhakikisha kila jambo linakwenda kwa mujibu wa sheria upo utaratibu wa kupeleka ramani ili kufahamu kinachokwenda kujengwa. Kutokuwapo kwa baadhi ya vitu ambavyo ni matakwa ya kisheria ni udhaifu katika utekelezaji wake,” anasema.

Anasema katika kusimamia utekelezaji kuna mipango madhubuti ya kuanzisha kitengo maalumu cha udhibiti wa maendeleo ya miji, pia kushirikisha wachora ramani wa sekta binafsi, huku elimu ikitolewa kwa wananchi kuhusu sheria na kanuni za kufuata wakati wa ujenzi.

Ilanga anasema kupitia sheria zikiwamo za Serikali za Mitaa Sura ya 288 ya mwaka 1984, Mipango Miji Sura 355 ya mwaka 2007 na Ardhi Na 4 ya mwaka 1999, halmashauri zinapaswa kuhakikisha kila matumizi ya kipande cha ardhi yanapangwa kwa kuzingatia uhusiano wake na matumizi mengine.

Rai imetolewa kwa Serikali za mitaa na halmashauri kuhakikisha majengo yote mapya yanazingatia sheria za ujenzi na kwa yale ya zamani kufanyiwa ukaguzi upya, hasa maeneo ya biashara yenye mikusanyiko mikubwa ya watu.

“Kila mtu anayejenga awe mjini au kijijini anapaswa kujua kibali cha ujenzi si karatasi tu ya kuanza kuchimba msingi, bali ni makubaliano kuwa atahakikisha usalama wa maisha ya watu,” anasema Profesa Kikwasi.

Omary, mwenyekiti wa Serikali ya mtaa anapendekeza uwepo utaratibu wa pamoja kati ya Serikali za mitaa, wataalamu wa mazingira na taasisi za usalama ili kuhakikisha majengo yanajengwa kwa kuzingatia sheria na viwango.

Milango ya dharura iweje?

Mkaguzi na Ofisa Habari wa Jeshi la Zimamoto na Ukoaji, Damian Muheya anasema mlango wa dharura unategemea matumizi ya jengo kama ni shule, kanisa, ofisi au ukumbi wa mikutano ni lazima iwe isiyopungua miwili kulingana na idadi ya watu.

Anasema kwa majengo ya ghorofa, kila moja linatakiwa kuwa na mlango wa dharura unaoelekea njia salama ya kutokea ili kurahisisha uokoaji pindi dharura itakapojitokeza.

Kuhusu ukubwa wa milango, anasema inapaswa kuzingatia matumizi ya jengo husika, akitoa mfano wa mlango wa upana wa sentimita 90 unaweza kuruhusu watu 60 hadi 100 kutoka kwa haraka, lakini kwa majengo yenye watu wengi zaidi, mlango unapaswa kuwa kati ya mita 1.2 hadi 2.4 na huongezeka kutokana na ongezeko la watu.

“Kwa mfano, watu 500 wanahitaji milango mitatu au zaidi, watu 1,000 wanahitaji angalau milango minne, ambayo isiegemee upande mmoja wa jengo bali igawanywe mbele, nyuma na pembeni,” anasema Muheya.

Milango hiyo, anasema inapaswa kufunguka kwa nje ili kurahisisha kutoka kwa haraka bila msongamano na haipaswi kufungwa kwa kufuli za kawaida, bali itumie kifaa maalumu kuruhusu kufunguka kwa kuisukuma.

Muheya  anasema alama za kutoka (EXIT) zenye mwanga maalumu wa rangi ya kijani au nyeupe ni lazima ziwekwe juu ya milango hiyo ili kusaidia watu kuitambua hata wakati wa giza na kuwe na taa za dharura zinazowaka moja kwa moja pale umeme unapokatika.

“Ni muhimu kufanya majaribio ya mara kwa mara ili wakazi au wafanyakazi wa jengo wafahamu njia za kutoka pindi dharura itakapotokea. Tunasisitiza elimu kwa watumiaji wa majengo kutolewa,” anasema Muheya.

Kwa majengo yasiyo na nafasi ya kuweka milango ya dharura kwa kila ghorofa, anasema madirisha yanaweza kutumika kama njia mbadala, lakini ni lazima yawe na ukubwa unaoruhusu mtu kupita na kuwe na ngazi za nje au njia salama ya kushuka.

Milango hiyo, anasema inapaswa kutengenezwa kwa vifaa visivyoshika moto kwa haraka au kupakwa dawa maalumu kuzuia moto ili kutoa muda wa kutosha kwa watu kutoka na kuzuia moto kusambaa kwa haraka.