Urusi yamjibu Trump kuhusu siala za nyuklia Urusi ilisema Jumatatu kwamba kila mtu anapaswa kuwa “muangalifu sana” kuhusu matamshi ya nyuklia, ikijibu taarifa ya Rais wa Marekani Donald Trump kwamba alikuwa ameamuru kuwekwa upya kwa manowari za nyuklia za Marekani.
Katika majibu yake ya kwanza ya umma kuhusu maoni ya Trump, Kremlin ilipuuza umuhimu wake na kusema haikutazami kuingia kwenye mabishano ya umma na Trump.
Trump alisema Ijumaa kuwa ameamuru manowari mbili za nyuklia kuhamishwa hadi “maeneo yanayofaa” kujibu matamshi kutoka kwa rais wa zamani wa Urusi Dmitry Medvedev kuhusu hatari ya vita kati ya wapinzani hao wenye silaha za nyuklia.

“Katika suala hili, ni dhahiri kwamba manowari za Amerika tayari ziko kwenye jukumu la kupigana. Huu ni mchakato unaoendelea, hilo ndilo jambo la kwanza,” msemaji wa Kremlin Dmitry Peskov aliwaambia waandishi wa habari.
“Lakini kwa ujumla, kwa kweli, hatungependa kujihusisha na mzozo kama huo na hatungependa kutoa maoni juu yake kwa njia yoyote,” aliongeza. “Kwa kweli, tunaamini kwamba kila mtu anapaswa kuwa muangalifu sana na matamshi ya nyuklia.”
Kipindi hiki kinakuja wakati mgumu, huku Trump akitishia kuweka vikwazo vipya kwa Urusi na wanunuzi wa mafuta yake, ikiwa ni pamoja na India na Uchina, isipokuwa pale Rais Vladimir Putin atakubali ifikapo Ijumaa kumaliza vita vya miaka mitatu na nusu nchini Ukraine.