Dar es Salaam. Mkurugenzi wa Uchaguzi wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC), Ramadhani Kailima, amewahimiza waandishi wa habari kujisajili katika mfumo wa ithibati ya waandishi wa habari ili kutambuliwa na tume wakati wakitekeleza majukumu yao siku ya uchaguzi mkuu.
Akisisitiza kuhusu usajili wa waandishi wa habari kwenye mfumo wa tume, Mjumbe wa Bodi ya Ithibati (JAB), Dk Egbert Mkoko, amesema wanaotakiwa kujisajili kwenye mfumo huo wa INEC ni waandishi wanaotambuliwa na JAB.
“Niwaambie tu kwamba huwezi kusajiliwa na tume ili uripoti uchaguzi mkuu kama hujasajiliwa na JAB. Lazima uwe umethibitishwa na JAB kwanza, ndipo usajiliwe kwenye mfumo wa Tume ya Uchaguzi,” amesema Dk Mkoko.
Amewataka wanahabari kuzingatia weledi na maadili ya taaluma yao, huku akisisitiza umuhimu wa kuepuka habari zinazoweza kuwagawa Watanzania kwa misingi ya dini, kabila, jinsia au ukanda.
Akizungumza leo, Jumatatu, Agosti 4, 2025, kwenye mafunzo kwa wahariri na waandishi wa habari kutoka vyombo mbalimbali nchini kuhusu Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 2025 utakaohusisha vyama 18 vya siasa, Kailima amesema mfumo huo utaanza kuwasajili waandishi Septemba mosi, 2025.
Kailima amesema mfumo huo una lengo la kuwatambua waandishi wote wa habari watakaoripoti uchaguzi huo mkuu utakaofanyika Oktoba 29.
Amesema kama waandishi watajisajili katika mfumo huo, itawasaidia hata kupatiwa msaada pale watakapokumbana na changamoto yoyote wakati wanapotekeleza majukumu yao.
“Ninatoa wito kwenu kujisajili kwa wingi kwenye mfumo huo mara utakapoanza ili mpate fursa ya kuripoti uchaguzi mkuu bila bughudha yoyote,” amesema Kailima wakati akifungua mafunzo hayo kwa wahariri na waandishi wa habari.

Wakati huohuo, mkurugenzi huyo amewataka waandishi wa habari kuzingatia maslahi ya Taifa wakati wakiandika taarifa zao kwa sababu Tanzania ndiyo nchi yao, hivyo nao wana wajibu wa kuhakikisha amani inaendelea kuwepo kwa kutochochea vurugu wakati wa uchaguzi.
Amesisitiza kwamba ni muhimu kwa waandishi wa habari kufanya kazi zao kwa weledi ili kulinda maslahi ya Taifa, sambamba na kuepuka viashiria vyovyote vya uvunjifu wa amani wakati wa uchaguzi.
“Tukumbuke kwamba nchi hii ni yetu sote na tuna wajibu wa kuhakikisha amani tuliyonayo inaendelea kuwepo. Sisi, Tume ya Uchaguzi, tutawapatia kila aina ya ushirikiano kuhakikisha mnafanya kazi zenu vizuri,” amesema Kailima.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Usajili na Uzingatiaji wa Tume ya Ulinzi wa Taarifa Binafsi (PDPC), Stephen Wangwe, amesema tume inashirikiana na jumuiya mbalimbali za kimataifa ili kulinda anga mtandao na madhara kwa wananchi.
Wangwe amebainisha kwamba kutokana na kila nchi kuwa na utaratibu wake katika masuala ya mtandaoni, wameamua kubuni ushirikiano ili kukabiliana na changamoto za kimtandao ambazo hazitambui mipaka ya nchi.
“Kuna kitu kinaitwa anga ya kimtandao, ambayo haina mipaka ya kijiografia, na kulikuwa na changamoto ya usimamizi wake. Kumekuwa na uhitaji wa kuwa na sheria zinazofanana katika nchi zote.
“SADC wametengeneza sheria za mfano zinazotakiwa kutumiwa na nchi wanachama ili kuwe na usimamizi unaofanana katika masuala ya mtandao kwa lengo la kulinda anga ya mtandao,” amesema Wangwe.
Meneja wa Kitengo cha Huduma za Utangazaji kutoka Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA), Andrew Kisaka, amesema vyombo vya habari visipotumiwa kwa weledi katika kipindi cha uchaguzi, vinaweza kuchochea machafuko makubwa, kama ilivyotokea katika baadhi ya nchi za Afrika.
Amesisitiza kuwa waandishi wa habari na vyombo vyao wana jukumu kubwa la kuhakikisha taarifa zinazotolewa ni sahihi, za haki na zisizo na lengo la kuchochea vurugu au migogoro katika jamii.
“Nchini Nigeria, baada ya uchaguzi, watu zaidi ya 800 walipoteza maisha. Vilevile, nchini Kenya, zaidi ya watu 1,000 waliuawa na wengine takribani 600,000 kupoteza makazi yao. Hii yote ilitokana na uchochezi uliosambazwa kupitia vyombo vya habari,” amesema Kisaka.
Mmoja wa waandishi wa habari walioshiriki mafunzo hayo, Penina Malundo, amesema mafunzo hayo yatawaongezea weledi na kufanya kazi zao kwa ufanisi wakati wote wa kuripoti uchaguzi huo.
“Tunawashukuru INEC kwa mafunzo haya. Ninaamini kila mmoja wetu atafanya kazi kwa kuzingatia miiko ya taaluma yetu, pia kuweka uzalendo mbele ili maisha yaendelee baada ya uchaguzi,” amesema Malundo. “Tunawashukuru INEC kwa mafunzo haya, ninaamini kila mmoja wetu atafanya kazi kwa kuzingatia miiko ya taaluma yetu, pia, kuweka uzalendo mbele ili maisha yaendelee baada ya uchaguzi,” amesema Malundo.