Unguja. Baadhi ya wajumbe wa kupiga kura za maoni Jimbo la Mfenesini wamezuiwa kuingia ndani ya ukumbi kwa kile kilichoelezwa hawakuvaa sare za chama kama walivyoelekezwa
Wajumbe wa jimbo hilo wameanza kuingia ndani saa 3:00 asubuhi kwa ajili ya matayarisho ya upigaji kura za maoni kwa wabunge, wawakilishi na madiwani.
Jimbo hilo lenye wadi tisa ikiwemo ya Mfenesini, Mwakaje, Mwachealale, Kitundu, Bumbwisudi, Chuini, Kikaangoni na Kihinani.
Katika wadi hiyo wajumbe wote walitakiwa kuvaa sare za chama ikiwemo nyeusi na kijani, ambao hawakuvaa mavazi hayo hawakuruhusiwa kuingia ndani jambo ambalo liliwashangaza wengi na kusababisha mvutano wa maneno, wengine wakiondoka katika eneo hilo na baadhi yao kusubiria uamuzi utakaochukuliwa.
Hata wajumbe ambao wamevaa nguo za kijani zenye nembo za Chama cha Mapinduzi (CCM) hawakuruhusiwa kuingia ndani na walitakiwa kurudi makwao ili kuepusha usumbufu kwa sababu ilidaiwa kuwa tangazo ndivyo lilivyosema.

Baadhi ya wajumbe waliofika katika eneo hilo wakiwa na mavazi ambayo hayaruhusiwi walidai kuwa tangazo hilo lilichelewa kutoka na wengine wakidai kutolisikia kabisa.
Akizungumza na Mwananchi, Msimamizi Msaidizi wa wadi ya Mfenesini, Juma Mohamed Haji amesema sababu ya wajumbe hao kuzuiliwa kuingia ndani ya ukumbi huo ni kutovaa sare za chama zilizoelekezwa kwa mkutano huo.
Amesema licha ya kutovaa sare hizo, Lakini, wote waliofika hapo ni wajumbe halali hivyo busara ingetumika ili kura zisipotee kwa utaratibu huo.
“Katika hili tunapaswa kutumia busara na ustahimilivu ili kulinda kura zao kwa sababu hao wote ni wajumbe halali, bora waruhusiwe kwa sasa baadaye utaratibu mwingine ufuate, lakini sio busara kuwaacha waondoke,” amesema Juma.
Balozi wa wadi ya Kihinani, Abdalla Juma amesema kwa utaratibu uliowekwa kwa baadhi ya wajumbe ambao hawakuvaa sare kutoruhusika kuingia ndani litakuwa na athari kubwa katika mkutano huo, kwani wanapoteza kura na sio wajumbe.
“Jambo hili limeshatokea kilichobaki waruhusiwe watu wametoka mbali sio vizuri kurudi majumbani kwao na kukosa kupiga kura kwa kisingizio cha kutovaa sare walizoelekezwa,” amesema Abdalla.
Halima Suleiman ni miongoni mwa wajumbe ambao wamezuiwa kuingia ndani humo amesema: “Sote tuliozuiliwa kuingia ndani tumevaa sare za chama isipokuwa tu siyo kijani na nyeusi kama inavyosisitizwa hapa.”
“Tumeacha kazi zetu kwa ajili ya jambo hilo endapo hatutafanya maamuzi sahihi wataondoka,” amesema.
Mjumbe mwingine, Suhaila Khamis Juma amesema katoka kudhalilishwa na uzee aliokuwa nao anahitaji kupumzika na ingekuwa yeye sio mjumbe halali asingefika eneo hilo.
Hadi kufikia sasa bado wajumbe hao hawajaruhusiwa kuingia ndani ya ukumbi wa kupigia kura za maoni.