BINGWA mtetezi wa michuano ya Mataifa ya Afrika kwa Wachezaji wa Ligi za ndani (CHAN), Senegal imeanza vizuri kampeni za kutetea taji hilo baada ya kuifunga Nigeria ‘Super Eagles’, bao 1-0, katika pambano nzuri na la kuvutia baina ya miamba hiyo.
Pambano hilo la kundi D, lililochezwa kwenye Uwanja wa New Amaan Complex Zanzibar, lilishuhudia timu zote zikicheza soka la kushambuliana kwa dakika zote 90, ingawa ilikuwa Senegal iliyoibuka na ushindi.
Katika mechi hiyo iliyokuwa ya vuta nikuvute kwa timu zote mbili, Senegal ilipata bao la ushindi dakika ya 75, lililofungwa na nyota wa kikosi hicho, Christian Gomis, baada ya kuwazidi ujanja mabeki wa Nigeria.
Senegal ‘The Lions of Teranga’, inashiriki michuano hii kwa mara ya tatu baada ya kufanya hivyo mwaka 2011 na 2022 ilipotwaa taji hilo katika fainali ilipowafunga wenyeji, Algeria kwa mikwaju ya penalti 5-4, kufuatia miamba hiyo kutoka suluhu (0-0) dakika 120.
Kikosi hicho kinachoshika nafasi ya 18 katika viwango vya ubora wa FIFA, huku kikiwa kinafundishwa na Kocha, Souleymane Diallo, kilipata tiketi ya kushiriki michuano ya CHAN 2024, baada ya kuitoa timu ya Taifa ya Liberia kwa jumla ya mabao 4-1.
Kwa upande wa Nigeria, inashiriki michuano ya CHAN kwa mara ya nne kuanzia 2014, 2016, 2018 na 2024, huku ikiwa na benchi la ufundi chini ya Kocha Mkuu, Daniel Ogunmodede.
Kikosi hicho kilichoonyesha soka safi leo dhidi ya Senegal licha ya kupoteza, kilikata tiketi ya kushiriki michuano ya CHAN 2024 baada ya kuitoa Ghana kwa jumla ya mabao 3-1.
Ushiriki bora wa CHAN kwa timu hiyo ni wa mwaka 2018, ilipofika fainali na kukosa ubingwa mbele ya wenyeji Morocco, baada ya kuchapwa mabao 4-0, yaliyofungwa na Zakaria Hadraf aliyefunga mawili, huku Walid El Karti na Ayoub El Kaabi wakifunga moja moja.
Kabla ya leo, mara ya mwisho kwa timu hizo kukutana, ilikuwa ni mechi ya kirafiki ambapo Senegal ilishinda pia bao 1-0, katika pambano la kuvutia lililopigwa, Juni 16, 2019, huku mechi ya aina hiyo iliyopigwa Machi 23, 2017, zilitoka sare ya kufungana bao 1-1.
Kwa matokeo hayo Senegal inaongoza msimamo wa kundi D ikiwa na pointi tatu, huku Congo na Sudan zilizotoka sare ya bao 1-1, mechi ya kwanza zikiwa na pointi moja, wakati kwa upande wa Nigeria inaburuza mkia.