BoT yaainisha mikakati kukuza sekta ya kilimo yaainishwa

Dodoma. Benki Kuu ya Tanzania (BoT) imetenga Sh1 trilioni kama dhamana kwenye benki za maendeleo na zile za kibiashara, ili ziweze kuwakopesha wakulima waliokidhi vigezo vya mikopo lakini hawana dhamana.

‎‎Wakizungumza leo Jumanne Agosti 5, 2025 kwenye aonyesho ya wakulima, wafugaji na wavuvi (Nanenane) yanayoendelea mkoani Dodoma, wadau kutoka taasisi hizo wamesema mikopo hiyo imetolewa ili kuinua sekta ya kilimo ambayo awali ilionekana haikopesheki kutokana na kuwa na hasara, inayosababisha wakulima kushindwa kurejesha mikopo kwa wakati.

‎‎Mchumi kutoka BoT, LadslausSilydio amesema ili kuinua sekta ya kilimo, Benki Kuu ilifungua dirisha la mikopo ya wakulima kwa kutengwa Sh1 trilioni za dhamana kwa mikopo ambayo hutolewa na benki za maendeleo na zile za biashara.

‎Amesema BoT imeweka vigezo na masharti kwa benki zinazotoa mikopo kwa wakulima ambayo kama mkulima atakidhi vigezo na hana dhamana, fedha hizo zitatumika kwa dhamana ili mkulima atakaposhindwa kurejesha fedha, Benki Kuu iifidie benki husika.

‎‎”Tumekuwa tukifanya hivi tangu mwaka 2021 na kwa sasa sekta ya kilimo imeanza kukua tofauti na mwanzo ambapo ilikuwa haikui na kuonekana kuwa sekta ya kilimo siyo ya kukopesheka kutokana na hasara zilizopo,” amesema.

Amesema tangu mwaka 2021 mpaka sasa benki nyingi zimekuwa zikiomba fedha hizo na baada ya kukidhi vigezo vilivyowekwa na BoT zimekuwa zikiwakopesha wakulima na mwitikio ni mkubwa kwa wakulima kukopa.

‎Mkurugenzi wa ustawi na huduma jumuishi za fedha kutoka BoT, Michael Mwaifuka amesema wakulima wanaowekewa dhamana ya mikopo na BoT ni wanaofanya mauzo nje ya nchi na wajasiriamali wadogo na wa kati.

Amesema BoT inatoa dhamana ya asilimia 75 kwa mikopo ya muda mfupi na dhamana ya asilimia 50 kwa mikopo ya muda mrefu.

‎‎Amesema kupitia dirisha hilo wakulima wameshaanza kunufaika na mikopo kupitia benki, hasa wanaolima mazao ya biashara kama vile tumbaku, korosho na pamba.

‎‎”Mikopo hii ina masharti, hasa kwa upande wa riba zinazotozwa na benki ambazo zimeomba kuwakopesha wakulima, inatakiwa isizidi asilimia 10 ambapo udhamini wa BoT unakuwa kati ya asilimia 50 kwa miaka mitano hadi saba,” amesema.

‎Wakati huohuo, mfuko wa pembejeo umetoa hundi ya Sh8.5 bilioni kwa Benki ya Ushirika kwa ajili ya kuwakopesha vijana katika sekta ya kilimo kupitia programu ya Jenga Kesho iliyo Bora (BBT) ili kuwajengea uwezo kwenye kilimo-biashara.

‎‎‎Akipokea hundi hiyo kutoka mfuko wa pembejeo, Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya Ushirika, Godfrey Ng’urah amesema fedha hizo zitatumika kuwakopesha vijana ambao wapo kwenye mnyororo wa thamani wa kilimo- biashara kupitia BBT.

Amesema mikopo itatolewa kwa vijana wanaojishughulisha na uandaaji wa bidhaa, uzalishaji na huduma ili ziende sokoni.

‎Amesema mkopo huo ni awamu ya kwanza na kwamba Sh3.5 bilioni ni dhamana ya mikopo kwa ile ambayo watashindwa kuirejesha. Lengo ni kupokea Sh20 bilioni kutoka kwenye mfuko huo kwa ajili ya mikopo kwa vijana.

‎‎”Mpango wa kusimamia marejesho ya mikopo ni mzuri kwa kuwa yote itapitia kwenye vyama vya ushirika ambako vijana hao wana dhamana zao huko,” amesema.

Mnufaika wa mkopo kutoka BBT, Mercy Athanas ameziomba taasisi za fedha kutoa elimu kwa vijana kabla ya kuwapa mikopo ili waitumie kwa malengo yaliyokusudiwa badala ya kutumia kinyume chake na kushindwa kuirejesha.

‎‎Amesema licha ya kujishughulisha na kilimo-biashara, vijana wengi bado hawana elimu ya fedha.