CCM waitwa mahakamani kesi ya uteuzi wa Samia kugombea urais

Dar es Salaam. Mahakama Kuu Masjala Kuu Dodoma imekitaka Chama cha Mapinduzi (CCM) kufika mahakamani hapo leo Agosti 5, 2025 kuhusu kesi ya kikatiba inayokikabili, ya kupinga uteuzi wa Samia Suluhu Hassan kuwa mgombea urais katika Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 29, 2025.

Kesi hiyo imefunguliwa na mwanasiasa mkongwe, Dk Godfrey Malisa, mkazi wa Moshi mkoani Kilimanjaro, anayejitambulisha kuwa mwanachama wa CCM. Wadaiwa ni Wadhamini wa CCM waliosajiliwa na Katibu Mkuu wa CCM.

Samia, ambaye ni Rais na mwenyekiti wa CCM alipitishwa na Mkutano Mkuu wa CCM Taifa, Januari 19, 2025 kuwa mgombea wa urais kupitia chama hicho.

Dk Malisa amefungua kesi ya kikatiba kupinga uteuzi huo akidai ni batili kwa kuwa mchakato wake ulikiuka katiba ya CCM na Katiba ya Jamhuri ya mwaka 1977 na marekebisho yake mbalimbali.

Kesi hiyo namba 18925 ya mwaka 2025 imepangwa kusikilizwa na jopo la majaji Joachim Tiganga (kiongozi wa jopo), Everisto Longopa na Griffin Mwakapeje.

Mahakama imewaita wadaawa katika shauri hilo ikiwataka kufika mahakamani leo Agosti 5, 2025. Kesi imepangwa kutajwa.

Kwa mujibu wa hati za wito wa mahakama zilizosainiwa na Naibu Msajili wa mahakama hiyo Agosti mosi, 2025, wadaawa wametakiwa kufika mahakamani na kuwasilisha nyaraka wanazotarajia kuzitumia katika kesi hiyo.

“Fahamu kuwa kesi tajwa hapo juu imepangwa kwa ajili ya kutajwa kwa amri muhimu leo Agosti 5, 2025, saa 3:30 asubuhi mbele ya J. Tiganga, E. Longopa na G. Mwakapeje,” inaelezwa katika hati ya wito huo na kuongeza:

“Unatakiwa kufika katika mahakama hii kwa njia ya mtandao bila kukosa na unapaswa kutoa nyaraka zote unazokusudia kuzitumia kuunga mkono kesi yako.”

Dk Malisa anawakikishwa na wakili Denis Maringo anadai utaratibu uliotumika kumteua Samia kuwa mgombea urais wa chama hicho umemnyima haki ya kushiriki kikamilifu katika masuala ya kisiasa na haki za kidemokrasia.

Anadai haki hizo amepewa kwa mujibu wa Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania anapotaka kugombea nafasi mbalimbali za kisiasa ndani ya chama cha siasa kilichosajiliwa kwa mujibu wa sheria za Tanzania.

Anabainisha wadaiwa wamekiuka wazi Ibara za 39(1) (a), (b), (c), (d), (e), 104(7)(b) na pia Ibara ya 103(12)(b) za katiba ya CCM.

Pia anadai wamevunja Sheria ya Vyama vya Siasa ya mwaka 1992 (kama ilivyofanyiwa marekebisho) na kwa kufanya hivyo, wamevunja Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, 1977 (kama ilivyofanyiwa marekebisho).

Dk Malisa anadai Katiba ya nchi inaweka wajibu kwa wananchi na taasisi zote kuheshimu, kutii na kufuata sheria za nchi.

“Kwa kuzingatia muktadha na mazingira ya shauri hili, hakuna njia ya haraka ya kupata haki kwa uvunjifu uliodaiwa,” anadai.

Dk Malisa anadai: “Na njia zinazopatikana kama njia za rufaa ndani ya vikao vya chama cha wadaiwa (CCM) haziwezi kuwa za haki au za uhalisia kwa sababu walewale wanaolalamikiwa ndio wangeketi kusikiliza rufaa hiyo.”

Anadai jitihada za kutumia njia hizo za ndani zisingewezekana kwa vitendo kwa kuwa kipindi kilichobaki kabla ya majina kupelekwa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC) ni kifupi na mchakato wa ndani wa chama ungechukua muda mrefu na kusababisha maombi hayo kupitwa na wakati.

Shauri hilo limefunguliwa chini ya Ibara ya 30(3) ya  Katiba ya nchi na kanuni ya 4 ya Kanuni za Utekelezaji wa Haki za Msingi na Wajibu (Taratibu na Utaratibu wa Kesi, 2014).

Kesi hiyo imejengwa juu ya Ibara za 13, 21 na 38(2)(a) za  Katiba ya nchi.

Katika kiapo Dk Malisa anadai yeye ni mwanachama hai wa CCM, mwenye kadi ya uanachama namba C00004714-016-1 iliyotolewa Novemba 20, 2020.

Dk Malisa anadai uteuzi wa Samia ulikiuka Ibara ya 103(12)(b) ya katiba ya CCM ambayo inaitaka Kamati Kuu kupendekeza majina matatu ya wagombea wa nafasi ya urais.

Kwamba taratibu za mkutano huo pia zilikiuka Ibara ya 39(1)(a), (b), (c), (d), na (e) za katiba ya CCM na misingi ya haki asili (haki ya kusikilizwa, kanuni dhidi ya upendeleo), pamoja na kanuni za kura ya siri.

Dk Malisa anadai mchakato huo ulikiuka Ibara ya 38(2)(a) ya Katiba ya nchi inayotaka uchaguzi wa Rais mpya ufuatiwe na kuvunjwa kwa Bunge.

Anadai Februari 11 2025, alimwandikia barua Mwenyekiti wa CCM kumjulisha dhamira ya kufungua kesi dhidi ya chama hicho.

Dk Malisa anaiomba Mahakama itamke kuwa haki za msingi, uhuru na wajibu kwa mujibu wa Katiba ya nchi zinazopaswa kufurahiwa na wanachama wote wa CCM na wale wanaonuia kugombea nafasi mbalimbali za uongozi zimekiukwa na wadaiwa.

Pia uteuzi wa mgombea urais wa CCM uliofanywa na Kamati Kuu ya mdaiwa wa kwanza, Kamati ya Halmashauri Kuu ya Taifa na Mkutano Mkuu wa Taifa ni batili, tangu mwanzo haukuwa halali na ulikuwa kinyume cha taratibu.

Vilevile, anataka itoe amri ya kutengua uteuzi wa mgombea urais wa CCM na amri ya kuwalazimisha wadaiwa kufanya upya mchakato wa uteuzi wa mgombea wa urais kwa ajili ya uchaguzi mkuu ujao.

Amri nyingine anayoomba ni kuwataka wadaiwa kusitisha mara moja mchakato wa uteuzi wa wagombea wa ubunge na udiwani hadi pale kasoro zilizolalamikiwa katika shauri hilo zitakaporekebishwa, ikiwa ni pamoja na kuwa na taratibu huru na za haki katika mchakato wa uteuzi huo.