CHAN yafungua fursa ya jezi za Stars Zanzibar 

WAFANYABIASHARA wa jezi mjini Unguja wameelezea fursa zilizopo hususan katika Michuano ya Mataifa Ya Afrika kwa Wachezaji wa Ligi za ndani (CHAN), zinazoendelea kwa wenyeji Tanzania ikishirikiana na Kenya na Uganda.

Wakizungumza na Mwananchi Digital, wafanyabiashara mbalimbali hasa wa jezi wameeleza michuano ya CHAN inayoendelea  jinsi itakavyowanufaisha kutokana na mwitikio wa uhitaji hasa wa timu ya taifa ya Tanzania ‘Taifa Stars’.

Akizungumza mjini Unguja, Simba Dunia amesema mwitikio wa jezi ni mkubwa jambo linalowapa matumaini makubwa ya kunufaika na michuano ya CHAN 2024.

“Hadi muda huu nimeuza zaidi ya jezi 10 na ukiangalia hata mechi ya kwanza bad. Hii kwetu kama Wafanyabiashara inatupa morali ya kuendelea kuhakikisha tunatumia vyema michuano hii ya CHAN 2024,” amesema.

Dunia amesema baada ya mechi za leo kuisha ataianza safari ya kwenda Dar es Salaam kwa ajili ya kuziuza tena jezi hizo katika pambano la kikosi hicho cha Taifa Stars dhidi ya Mauritania.

“Leo usiku nitaondoka Ili kuiwahi tena timu yetu ya Taifa, lengo ni kufanya biashara lakini kuisapoti pia ili tufanye vizuri kama tulivyoanza mechi ya kwanza na Burkina Faso,” amesema.

Naye Ali Omar Masoud amesema mwitikio wa jezi za timu ya Taifa ni mkubwa kuliko ilivyozoeleka mwanzoni, kwa sababu alikuwa akiuza za Yanga na Simba zaidi tofauti na sasa.

“Jezi za Yanga na Simba tunauza ila ukiangalia tangu michuano ya CHAN 2024 imeanza, kumekuwa na muitikio kwa Taifa Stars, Jambo linaloonyesha uzalendo tulionao kwa timu yetu,” amesema.

Kwenye Uwanja New Amaan Zanzibar, leo zitachezwa mechi mbili za kundi D, ambapo Congo itacheza na Sudan kuanzia saa 11:00 jioni, huku bingwa mtetezi, Senegal ikipambana na Nigeria saa 2:00 usiku.