Chaumma mguu sawa kumpata mgombea urais Uchaguzi Mkuu 2025

Dar es Salaam. Chama cha Ukombozi wa Umma (Chaumma), kimeingia rasmi katika hatua ya mwisho ya mchakato wa kumpata mgombea wake wa urais kwa upande wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, kuelekea Uchaguzi Mkuu utakaofanyika Oktoba 29, 2025.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa leo Jumanne, Agosti 5, 2025 na Mkurugenzi wa Mawasiliano na Taarifa kwa Umma wa chama hicho, John Mrema, vikao mbalimbali vya kitaifa tayari vimeanza kufanyika tangu jana Jumatatu, Agosti 4, 2025.

Taarifa hiyo imeeleza kuwa mchakato huo wa vikao utaendelea hadi Agosti 7 na majina ya wagombea yatatangazwa rasmi katika Mkutano Mkuu wa Taifa wa chama hicho.

“Vikao vya Sekretarieti ya Taifa vilianza rasmi Agosti 4 na vimeendelea hadi leo Agosti 5, 2025 kwa ajili ya maandalizi ya vikao vya juu vya chama. Sekretarieti inaweka msingi wa ajenda muhimu zitakazojadiliwa na viongozi wa kitaifa wa chama,” imesema taarifa hiyo.

Taarifa hiyo imesema Agosti 6 (kesho), Kamati Kuu ya Taifa pamoja na Halmashauri Kuu ya Taifa zitakutana jijini Dar es Salaam kwa ajili ya kujadili na kupitisha ajenda zitakazowasilishwa katika Mkutano Mkuu wa Taifa.

“Hiki ni kikao muhimu kitakachoweka mwelekeo wa kisiasa wa chama hicho kuelekea uchaguzi mkuu,” imeeleza taarifa hiyo.

Kilele cha mchakato huo ni Mkutano Mkuu wa Taifa utakaofanyika Agosti 7, 2025, katika Ukumbi wa Mlimani City, jijini Dar es Salaam. Taarifa ya Mrema imeeleza mkutano huo unatarajiwa kuwa wa kihistoria kwa Chaumma, kwa sababu utafanya uteuzi rasmi wa wagombea wake wakuu wa urais, pia utatumika kuzindua Ilani ya Uchaguzi ya chama hicho kwa kipindi cha 2025 hadi 2030.

Kwa mujibu wa taarifa hiyo, Ilani ya uchaguzi ya Chaumma “inatokana na sauti ya wananchi na mahitaji ya Taifa kwa sasa,” kauli inayolenga kutoa ushindani mpya katika medani ya siasa nchini, hasa kwa wapiga kura wanaotafuta mabadiliko na sera mbadala.

“Katika mkutano huo, chama kinatarajiwa kutangaza wagombea wake watatu wakuu: Mgombea wa urais na mgombea mwenza wa Tanzania na mgombea wa urais wa Zanzibar.” Taarifa hiyo imeeleza kuwa mchakato mzima umezingatia taratibu za kikatiba ndani ya chama na unaongozwa na Mwenyekiti wa Taifa wa Chaumma, Hashim Rungwe.

Kwa mujibu wa wachambuzi wa siasa, hatua ya Chaumma kufanya mchakato mapema na kwa uwazi ni dalili ya kujitokeza kwa harakati mpya za kisiasa kutoka kwa vyama vidogo vinavyotaka kujenga nafasi ya ushindani dhidi ya vyama vikuu vya muda mrefu kama CCM, NCCR-Mageuzi, CUF, Chadema na ACT-Wazalendo.

Hata hivyo, taarifa hiyo haikueleza ni nani waliomba fomu za kutaka kuomba ridhaa ya chama ili kuwania nafasi hizo.

Endapo Hashim Rungwe atarudi tena kuwania urais kupitia Chaumma, hiyo itakuwa ni mara yake ya nne, hatua ambayo itaonyesha msimamo wake katika harakati za siasa nchini.

Tayari CCM kiko kwenye hatua ya mwisho ya uteuzi wa wagombea wake wa nafasi za udiwani na ubunge. Jana, Agosti 4, kura za maoni zilihitimishwa katika maeneo mbalimbali nchini, na sasa kinachosubiriwa ni vikao vya juu vya chama hicho kutangaza rasmi wagombea wa nafasi za udiwani, ubunge na uwakilishi.

Kwa muktadha huo, joto la kisiasa nchini linaendelea kupanda huku vyama vya siasa vikiingia kwenye hatua za mwisho za maandalizi ya uchaguzi mkuu, kila kimoja kikijipanga kuonyesha mwelekeo mpya kwa Watanzania.