COPRA YATAKIWA KUIMARISHA UDHIBITI WA MAZAO YA VIUNGO

Farida Mangube, Morogoro

Mamlaka ya Udhibiti wa Nafaka na Mazao Mchanganyiko (COPRA) wametakiwa kuongeza kasi ya kusimamia na kudhibiti uuzwaji holela wa mazao ya viungo, ili kuwawezesha wakulima nchini, hususan wa Mkoa wa Morogoro, kuuza mazao yao kwa bei stahiki na kuinua kipato chao kiuchumi.

Wito huo umetolewa na Katibu Tawala wa Mkoa wa Morogoro, Dkt. Mussa Ali Mussa, alipotembelea banda la COPRA kwenye maonesho ya kilimo, mifugo na uvuvi (Nanenane) kanda ya mashariki yanayoendelea mkoani humo, ambapo alipata fursa ya kujionea shughuli mbalimbali zinazofanywa na mamlaka hiyo.

Dkt. Mussa amesema mkoa wa Morogoro kwa sasa unapiga hatua kubwa katika uzalishaji wa mazao ya viungo kama vile karafuu, pilipili mtama, mdalasini na hiliki, hivyo kuna haja kwa COPRA kuongeza nguvu katika kusimamia mwenendo wa soko ili kuwalinda wakulima dhidi ya unyonyaji na kupoteza thamani ya mazao yao.

“Mkoa huu una fursa kubwa kwenye mazao ya viungo. Tunahitaji COPRA kuwa macho zaidi, kudhibiti uuzwaji holela na kuhakikisha wakulima wetu wananufaika kwa kuuza mazao yao katika mifumo rasmi kwa bei nzuri. Wakati umefika sasa kuondoka kwenye kilimo cha mazoea na kufanya kilimo cha kisasa chenye tija,” alisema Dkt. Mussa.

Kwa upande wake, Kaimu Mkuu wa Mamlaka ya Udhibiti wa Nafaka na Mazao Mchanganyiko kanda ya mashariki, Bi. Mary Majule, amesema COPRA imeendelea kuweka mikakati ya kuhakikisha wakulima wa viungo wanapata taarifa sahihi za masoko na kuongeza thamani ya mazao yao kupitia mifumo ya kielektroniki na ushirikiano na taasisi nyingine.

“Tumekuwa tukitoa elimu ya kuongeza thamani ya mazao, tunashirikiana na TBS kuhakikisha ubora, na pia tunaendelea kuhimiza wakulima wauze kupitia masoko yaliyosajiliwa ili kuepuka dhuluma. COPRA tumejipanga kuhakikisha sekta hii ya viungo inakuwa tegemeo kubwa la uchumi,” alisema Bi. Majule.

Katika maonesho hayo, banda la COPRA limeendelea kuwavutia wakulima na wananchi kwa kutoa elimu kuhusu taratibu za biashara ya mazao, masoko, na namna bora ya kuhifadhi na kuongeza thamani ya nafaka na mazao mchanganyiko.