Dewji awaombea Stars mamilioni | Mwanaspoti

MFADHILI wa zamani wa Simba, Azim Dewji amewataka wafanyabiashara wakubwa na mashabiki wa timu ya Taifa ‘Taifa Stars’ kuonyesha uzalendo kuwapongeza wachezaji wa Stars kwa kuwapa maokoto katika mechi watakazoshinda.

Stars inashiriki michuano ya CHAN kwa mara ya tatu, huku ikiwa ni mara ya kwanza kwa Tanzania kuteuliwa kufungua  mashindano hayo.

Kikosi hicho kilichopo katika kundi B la mashindano hayo, kilicheza mechi ya kwanza dhidi ya Burkina Faso na kuichapa mabao 2-0 matokeo yaliyotoa matumaini makubwa.

Akizungumza na Mwanaspoti, Azim amesema licha ya Rais Samia Suluhu kuiahidi timu hiyo Sh1 bilioni kama itachukua ubingwa, lakini bado taasisi zingine na wafanyabiashara wana kitu cha kufanya kama motisha kwa wachezaji.

“Kweli mama alishatoa ahadi yake, ila bado na sisi ambao ni mashabiki tunaweza kufanya kitu ili kuwapa hamasa wachezaji. Nawaza hapa Tanzania kuna benki ngapi ambazo zinaweza kutoa milioni 10 tu. Kama Stars itakusanya milioni 100 kwa kila mechi ambazo itashinda, basi tutakuwa tumewatengenezea ari kubwa (wachezaji) na hata wao wataona jinsi ambavyo tunatamani timu ifike mbali,” amesema na kuongeza:

“Mama Samia amekuwa mstari wa mbele katika klabu zetu kuzisaidia ili kuzitia moyo katika mashindano makubwa, hivyo hili la Taifa inatubidi tuonyeshe uzalendo.

“Lakini pia TFF inatakiwa ifanye hamasa katika mechi zote hata za wageni zitakazochezwa hapa kwetu hata viingilio vikiwa vidogo, lakini katika michezo yote ya Stars mashabiki twendeni kwa wingi.”

Stars iko kundi moja na Mauritania, Afrika ya Kati, Burkina Faso na Madagascar katika kundi hilo na kwa sasa inashika nafasi ya kwanza ikiwa ndio timu pekee yenye alama tatu.